Jamvi La Siasa

Viongozi wapanga kutoroka Ruto 2027, waanza manung’uniko ya wazi

Na MOSES NYAMORI, COLLINS OMULO July 23rd, 2025 Kusoma ni dakika: 3

MLIPUKO mkubwa wa kisiasa unatazamiwa kukumba chama cha United Democratic Alliance (UDA) cha Rais William Ruto, huku baadhi ya viongozi wake wa juu wakianza kupanga mikakati ya kuondoka kabla ya uchaguzi mkuu wa 2027.

Baadhi ya viongozi hao—ambao wanashikilia nyadhifa muhimu ndani ya chama na pia Bungeni—wameibuka kuwa wakosoaji wakuu wa serikali ya Rais Ruto, hususan kutokana na madai ya kukandamizwa kwa wapinzani kupitia kesi za ugaidi na utekaji nyara unaodaiwa kufanywa na maafisa wa serikali.

Wengine wameanza kutoa matamshi yanayokinzana hata katika masuala yanayohitaji msimamo wa pamoja, jambo linaloashiria uwezekano mkubwa wa kuhamia upinzani.

Dalili za kuhama kwa wingi zimechochewa zaidi na matamshi ya wazi kutoka kwa viongozi waliochaguliwa kwa tiketi ya UDA wanaohusishwa na aliyekuwa Naibu Rais Rigathi Gachagua na aliyekuwa Waziri wa Usalama wa Ndani, Dkt Fred Matiang’i.

Viongozi kadhaa wa kisiasa kutoka eneo la Mlima Kenya tayari wametangaza kumuunga mkono Bw Gachagua, huku baadhi ya wanasiasa kutoka eneo la Gusii walio UDA nao wakitangaza kumuunga mkono Dkt Matiang’i kuelekea uchaguzi wa 2027.

Vyanzo vimeeleza kuwa baadhi ya wabunge walioteuliwa na madiwani kutoka maeneo mbalimbali, hususan Mlima Kenya, wanasubiri wakati mwafaka wa kujiondoa UDA.

Hali hii ndiyo inafanya chama hicho kuchukua hatua kali dhidi ya viongozi walioteuliwa. Tayari UDA imemfukuza aliyekuwa Seneta wa kuteuliwa Gloria Orwoba, na sasa imo katika mchakato wa kuwatimua madiwani wa kuteuliwa Joy Mwangi (Nairobi) na Ann Thumbi (Nyeri) kwa madai ya kuunga mkono upinzani.

Kiongozi wa Wengi katika Seneti, Dkt Boni Khalwale (Kakamega), Gavana wa Murang’a Irungu Kang’ata, Mbunge wa Kiharu Ndindi Nyoro na Mbunge wa Nyali Mohammed Ali, wamekuwa wakosoaji wakuu wa serikali ya Kenya Kwanza kutoka ndani ya chama hicho.

Mbunge wa Mugirango Kaskazini, Joash Nyamoko, pia ametangaza hadharani kuwa atamuunga mkono Dkt Matiang’i dhidi ya mgombea wa UDA katika uchaguzi wa urais wa 2027.

Nyamoko hakujibu maswali kuhusu mipango yake ya kisiasa. Dkt Khalwale, mmoja wa waasisi wa UDA, amesema chama hicho “kimekufa” katika eneo la Magharibi.

“Nilianzisha chama cha UDA Kakamega na maeneo mengine ya Magharibi, na kwa sasa siwezi kusema chama bado kipo,” alisema.Kuhusu iwapo atagombea kwa tiketi ya UDA, alisema atakamilisha “mkataba wake wa kijamii” na wananchi, na atafanya uamuzi kulingana na hali itakavyokuwa mwaka 2027.

“Hata Rais Ruto mwenyewe hana uhakika kama atatumia tiketi ya UDA. Tangu Katiba ya 2010 ianze kutumika, hakuna rais aliyewahi kugombea muhula wa pili kwa tiketi ya chama alichotumia muhula wa kwanza,” alisema.

Gavana wa Embu, Cecily Mbarire, ambaye pia ni kaimu mwenyekiti wa UDA, mnamo Juni 1, 2025, alilalamikia kile alichokiita njama za baadhi ya maafisa wa serikali kuu kumdhoofisha kisiasa—lalama ambazo zilionekana kumlenga Naibu Rais Kithure Kindiki.

Profesa Kindiki, hata hivyo, alikana kuwepo kwa mzozo kati yake na Bi Mbarire, akisema uhusiano wake na viongozi wa Embu ni wa muda mrefu na una msingi thabiti.

Mnamo Julai 11, 2025, Gavana Kang’ata alitoa kauli kali dhidi ya serikali akisema imetukosea sana kwa kuuua vijana.Ameendelea kukosoa serikali kupitia safu yake ya maoni katika gazeti la Saturday Nation, japo hajafichua msimamo wake wa kisiasa kuhusu uchaguzi wa 2027.

Ndindi Nyoro, ambaye aliondolewa kutoka wadhifa wa mwenyekiti wa Kamati ya Bajeti katika Bunge la Taifa, alitoa matamshi makali mnamo Julai 10, 2025, akitaja serikali kuwa “isiyo na mwelekeo”.

“Serikali inayoua watu bila kujuta, bali kutoa amri ya ‘piga risasi kuua’, ni hatari. Serikali inafadhili sana taasisi za kijasusi lakini imeshindwa kulinda maisha na mali ya wananchi.”

Mbunge Mohammed Ali, ambaye hapo awali alikuwa mtetezi mkubwa wa Rais Ruto, sasa amekuwa mkosoaji mkubwa wa serikali ya Kenya Kwanza. Tangu 2024, ameanza kujitenga na shughuli nyingi za Rais, ikiwemo kutohudhuria hafla za umma.

Wafuasi wa Gachagua, ambao sasa wameanza kujiunga na chama chake kipya, Democracy for the Citizens Party (DCP), ni pamoja na Wabunge Edward Muriu (Gatanga), Benjamin Gathiru (Embakasi Central), Jayne Kihara (Naivasha), John Methu (Seneta wa Nyandarua), Karungo Thangwa (Seneta wa Kiambu), James Gakuya (Embakasi North), Gathoni Wamuchomba (Githunguri), Njeri Maina (Mwakilishi wa Wanawake – Kirinyaga), Joe Nyutu (Seneta wa Murang’a), na James Murango (Seneta wa Kirinyaga).

Muriu alisema kuna njama ya baadhi ya watu walio karibu na Rais Ruto kutumia vyama vingine vidogo vinavyohusishwa na kanda ya Mlima Kenya ili kugombea 2027, lakini akasema watawafichua viongozi hao:“Chama chochote ambacho hakihusiani na DCP kitatambuliwa kama wilibaro lililopakwa rangi nyingine.”