Jamvi La Siasa

Visiki mbele ya Ruto kuelekea uchaguzi wa 2027

Na JUSTUS OCHIENG April 17th, 2025 Kusoma ni dakika: 2

KUCHAGULIWA tena kwa Rais William Ruto katika uchaguzi mkuu wa 2027 kunakumbwa na visiki vingi vinavyohusisha misukosuko ya ndani ya muungano wa Kenya Kwanza, migawanyiko ya kisiasa, hali ngumu ya kiuchumi, uasi wa vijana, na mikakati ya upinzani kuungana kumpinga.

Tangu achukue uongozi mwaka wa 2022, Rais Ruto amekuwa akilenga muhula wa pili, lakini juhudi zake zimekumbwa na changamoto kutoka kwa washirika wake wa karibu na viongozi wa upinzani wanaoungana.

Kwa sasa, Rais anakabiliwa na hali tata ya kisiasa inayohitaji usawazishaji wa haraka, la sivyo atumbukie katika mtego wa kutokuwa na ushawishi mkubwa wa kitaifa ifikapo 2027.

Muungano wa Kenya Kwanza ambao ulimwezesha Rais Ruto kushinda 2022 umeanza kudhoofika. Hadi sasa, ni chama kimoja tu—ANC cha Musalia Mudavadi—kilichokubali kuvunjwa na kumezwa na UDA.

Vyama vingine, kama Ford Kenya cha Moses Wetang’ula na Democratic Party kinachohusishwa na aliyekuwa Mwanasheria Mkuu Justin Muturi, vimekataa kuvunjwa, huku vingine vikionyesha dalili za kujiondoa kabisa kutoka muungano huo.

Chama cha Ford Kenya kilichokutana hivi majuzi katika Kaunti ya Nakuru, kilitangaza kuwa hakitavunjwa na kitaendelea kujijenga chenyewe kuelekea 2027, kikiapa kusimamisha wagombeaji wake katika uchaguzi mdogo ujao maeneo tofauti nchini.

Hili linaweka mazingira ya ushindani mkali ndani ya Kenya Kwanza na kudhoofisha juhudi za Rais.

Zaidi ya hayo, kusambaratika kwa ushirikiano kati ya Rais Ruto na aliyekuwa Naibu wake Rigathi Gachagua kumeibua sintofahamu kubwa, hasa katika eneo la Mlima Kenya ambalo lilimpa kura nyingi mwaka wa 2022.

Gachagua ameapa kuanzisha chama kipya na kupigania maslahi ya eneo hilo, jambo ambalo linaweza kugawanya kura za Mlima Kenya.

Huku hayo yakijiri, upinzani unaonekana kuimarika kwa kasi.

Kiongozi wa Wiper Kalonzo Musyoka, Martha Karua wa Narc Kenya, Eugene Wamalwa wa DAP-K, Gachagua na viongozi wengine wametangaza azma ya kusimamisha mgombeaji mmoja dhidi ya Ruto. Ushirikiano wao unaweza kuwa tishio endapo watafanikiwa kushirikiana na kutatua tofauti zao mapema.

Licha ya hatua ya ODM inayoongozwa na Raila Odinga kutia saini makubaliano ya ushirikiano na UDA, bado kuna mashaka ndani ya ODM kuhusu kuunga mkono Ruto.

Viongozi kama Edwin Sifuna, James Orengo na Godfrey Osotsi wameonya kuwa makubaliano hayo hayawezi kutekelezwa ikiwa serikali haitaheshimu masuala ya msingi waliyokubaliana.

Mbali na siasa, Rais Ruto pia anakabiliwa na shinikizo la kiuchumi. Malalamishi ya wananchi kuhusu gharama ya juu ya maisha, ukosefu wa ajira kwa vijana, na sera tata za ushuru zimeifanya serikali kupoteza uungwaji mkono, hasa miongoni mwa Gen Z.

Maandamano ya 2024 dhidi ya Mswada wa Fedha yalionyesha hasira na kukata tamaa kwa vijana wengi.

Wachambuzi wa siasa kama Prof Gitile Naituli na Dismas Mokua wanakubaliana kuwa Rais Ruto ana kazi kubwa mbele yake.

Anafaa kurejesha matumaini ya wananchi kwa kutoa maendeleo ya kweli, kupunguza bei ya bidhaa muhimu, na kuimarisha ushawishi wake katika maeneo yaliyompa kura nyingi 2022.

Ingawa ana muda wa kurekebisha makosa, ushindani unaotarajiwa 2027 utakuwa mkali, huku wapinzani wakijipanga vyema na wananchi wakitathmini utendakazi wake kwa miaka mitano ya kwanza.

Kwa sasa, njia ya Rais Ruto kuelekea kuchaguliwa tena ina matuta mengi na inahitaji maamuzi ya kisiasa ya busara, uongozi thabiti, na sera za kweli za kuimarisha maisha ya Wakenya kuinyoosha.