Jamvi La Siasa

Visiki vya safari ya Ruto kupeleka Wakenya Singapore

Na JUSTUS OCHIENG',BENSON MATHEKA January 4th, 2026 Kusoma ni dakika: 2

RAIS William Ruto ametaja mwaka huu wa 2026 kama “mwaka wa utekelezaji.” Wapinzani wake, kwa upande mwingine, wamepanga mwaka huu kuwa wa kuhakiki utawala wake; kwa vyovyote, 2026 unaweza kuwa mgumu au muhimu zaidi kwa urais wake.

Ingawa kalenda ya kisiasa ya Kenya inaashiria 2027 kama wakati wa kuamua, wakati wananchi watapiga kura, kwa Rais Ruto, mapambano halisi yanaanza mwaka mmoja mapema.

“Kwa mara ya kwanza kwa muda mrefu, hatubahatishi. Hatuchezi kamari. Tumepanga malengo yetu. Tumeanza safari. Na sasa tuna ramani wazi ya kufanya mwaka wa 2026 uwe wa kipekee katika historia ya Kenya,” alisema Rais Ruto katika hotuba yake ya Mwaka Mpya.

Rais alisema mwaka huu utakuwa “mwaka wa kihistoria katika hadithi ya Jamhuri yetu. Wakati wa mabadiliko kutoka ahadi hadi ustawi. Mwaka ambao vizazi vijavyo vitat uangalia na kusema; hapo ndipo Kenya ilibadilisha mwelekeo.”

Wachambuzi wa siasa wanasema mwaka huu ahadi zinakutana na uvumilivu, uchumi unaimarisha siasa, na matokeo ya utekelezaji yatakuwa lugha pekee ya msingi wa kampeni.

Rais Ruto ameupatia jina “mwaka wa utekelezaji” wakati mabadiliko yataimarishwa, miradi mikubwa itaanza kuonekana, na Wakenya hatimaye “wataona picha kamili” ya serikali yake.

“Tuwe wazi kuhusu malengo yetu. Tumejipanga kwa kazi inayopimika kitaifa; kupunguza nusu ya idadi ya Wakenya maskini zaidi, kuinua mamilioni kuishi kwa heshima na kupunguza ukosefu wa ajira kwa nusu, kuhakikisha kuwa mamilioni ya raia wetu wanakuwa na uzalishaji, kipato, na michango,” alisema Rais.

Lakini wachambuzi wanasema kisiasa, maandalizi haya yanaonyesha mkakati wa kawaida wa wanasiasa walio madarakani.

Historia inaonya kwamba serikali hazihukumiwa kwa nia au ratiba, bali kwa uzoefu halisi wa wananchi. Kwa kipimo hicho, 2026 unaweza kuwa si mwaka wa kuimarisha, bali mwaka wa kumchambua Rais Ruto, kama anavyosema mchambuzi Prof Gitile Naituli wa Chuo Kikuu cha Multimedia.

“Utekelezaji si kifaa kinachoweza kubadilishwa katika mwaka wa nne wa muhula,” anasema. “Matokeo ya maendeleo ni mfululizo. Chaguo za awali zinazoleta maumivu zinaweza kufanya ahadi za baadaye kushindwa kubadilisha hisia za wananchi.”

Rais Ruto aliingia madarakani wakati wa hali ngumu ya uchumi na mara moja alibadilisha mwelekeo wa sera kupitia kuondoa ruzuku, kupanga vipaumbele vya fedha kulingana na matarajio ya wakopeshaji wa kimataifa.

Baadhi ya marekebisho haya yanaanza kuleta matokeo, huku Rais akisisitiza kwamba mfumuko wa bei umepungua, shilingi imekuwa thabiti, na akiba ya fedha za kigeni imeimarika.

Lakini siasa haziishoi kwenye hesabu tu. Prof Naituli anasema“Wakenya wanapata uchumi kwa meza jikoni. Chakula, kodi, usafiri, ada za shule na huduma za afya. Hapo ndipo uchaguzi huwa unaamuliwa.”

Ushuru mkubwa na kupungua kwa mapato kumeacha familia kwenye mateso.

Rais Ruto ameahidi kuharakisha upanuzi wa barabara, kupanua reli ya kisasa kutoka Naivasha hadi Kisumu na hatimaye Malaba, na kuanza ujenzi wa uwanja wa ndege wa kisasa ili kuimarisha biashara na utalii.

Hata hivyo, ukweli wa kifedha ni mgumu. Ulipaji wa deni unashindana na matumizi ya maendeleo, ulinzi wa kijamii na huduma muhimu. Kila mradi mpya huibua maswali: “Nani atalipa? Nani anafaidika?

Wachambuzi na wapinzani wanachukulia uchumi kama changamoto kubwa zaidi kwa Rais Ruto. Ingawa takwimu zinaonyesha ukuaji, familia zinakabiliana na bei za chakula zinazoendelea kupanda, mafuta ghali, kodi kubwa, na kuendelea kupungua kwa mapato.

“Ni mwaka ambapo utulivu wa uchumi lazima uonekane katika maisha ya kila siku,” anasema kiongozi wa Safina, Jimi Wanjigi.