Wabunge chipukizi waapa kukomboa Kenya, watadhamini mgombeaji urais 2027
MRENGO wa Kenya Moja, unaoshirikisha wabunge chipukizi, sasa unaahidi kudhamini mgombeaji urais katika uchaguzi mkuu ujao huku ukiahidi kuleta “ukombozi wa tatu nchini”.
Wanachama wa vuguvugu hilo, waliochaguliwa kwa tiketi za vyama vya ODM, UDA, Ford Kenya na DAP-K, wanasema wanataka kuleta mabadiliko ya kweli yanayoakisi matarajio ya kizazi cha kisasa cha Wakenya almaarufu Gen-Z.
“Sisi kama viongozi wa kizazi cha sasa, tuko tayari kuchukua uongozi wa taifa hili mwaka wa 2027 kwa kudhamini mgombeaji wa urais.
“Kenya Moja si mrengo wa tatu jinsi wengine wanavyodai; huu ndio mrengo mkuu kwa sababu Wakenya wa umri wa chini ndio wengi zaidi nchini,” akasema Mbunge wa Embakasi Mashariki, Babu Owino, ambaye ni mmoja wa nyota wa vuguvugu hilo.
“Angalia Burkina Faso, (Ibrahim) Traore alikuwa rais akiwa na miaka 32. Gaddafi alipata urais akiwa na miaka 28. Sisi vijana wa Kenya tumechelewa,” akaongeza kwenye mahojiano na NTV.
Bw Owino alikuwa akirejelea Rais wa sasa wa Burkina Faso Ibrahim Traore, anayesifiwa kwa kuleta mageuzi makuu nchini na aliyekuwa Rais wa Libya Muamar Gaddafi aliyeacha rekodi nzuri ya uongozi.
Mbio za kuwania urais wa Kenya mwaka wa 2027 zimeanza kushika kasi, huku kikundi cha viongozi chipukizi kikijitokeza na kuanza kuvutia hisia za Wakenya, hususan vijana.
Kwa mujibu wa viongozi hao, Kenya Moja inalenga kuleta mabadiliko ya kweli kwa kuondoa hali wanayoiita uongozi wa kizazi kilichoshindwa kutimiza matarajio ya wananchi kwa miaka mingi.
Wanasisitiza kuwa vijana sasa wamekomaa na wako tayari kuchukua hatamu za uongozi kuanzia mwaka wa 2027.
Wabunge hao wanasisitiza kuwa mrengo wao si wa kugawa upinzani, bali ni wa kuunganisha Wakenya wanaotaka mabadiliko ya kweli.
Wanasema kama Wakenya wanataka wachukue hatua zaidi kama kuunda chama rasmi au kumteua mgombea urais, wako tayari kufanya hivyo.
“Kama wananchi watatuambia tusimame kuwa sauti yao, tuko tayari. Tukiamriwa tuunde chama, tutafanya hivyo. Sisi tunaitikia tu wito wa wananchi,” alisema Caleb Amisi (Mbunge wa Saboti).
Naye Bi Gathoni Wamuchomba (Githunguri) alisisitiza kuwa lengo lao ni kuwapa wananchi suluhu kwa changamoto wanazopitia, na wala si kutafuta umaarufu wa kisiasa.
“Kama kushirikiana na (Seneta Edwin) Sifuna na Babu kutaleta suluhu kwa vijana, wanawake, wakulima na Wakenya kwa jumla – basi tuko tayari. Na kama hilo litageuka kuwa chama au muungano rasmi, iwe hivyo,” akasema.
Hata hivyo, wachanganuzi wa kisiasa wameonya kuwa endapo Kenya Moja haitajitofautisha kwa sera na mwelekeo wa kisiasa wa maana, huenda ikachukuliwa kama muungano mwingine wa kisiasa wa muda mfupi unaotegemea tu maneno ya kisiasa.
Licha ya hayo, viongozi wa Kenya Moja wamejitetea wakisema wana nia safi na uwezo wa kuleta mabadiliko ya kweli.
Wameitaka serikali kuachia uongozi kizazi kipya chenye maono na taaluma bora.
“Huwezi kumwamini rubani wa miaka 65 kukupeleka angani, kwa nini umwamini mwanasiasa wa miaka hiyo kuongoza maisha yetu?” aliuliza Bi Wamuchomba.
“Ajenda kuu ya Kenya Moja ni kuondoa azimio lililoshindwa. Tunataka kuonyesha maana halisi ya uongozi,” aliongeza Babu.
Hata hivyo, wadadisi wa masuala ya kisiasa wanashuku uwezo wa wanachama wa Kenya Moja kujidumisha kisasa kivyao kwani hawajajijengea umaarufu katika pembe zote za nchi.
“Wanasiasa hawa ni makinda waliolelewa kisiasa na wanasiasa wakuu na itakuwa vigumu kwao kujisimamia kivyao katika uchaguzi mkuu ujao. Mbali na kutokita mizizi kote nchini, wanasiasa hao hawana nguvu za kifedha za kuwawezesha kusuka vuguvugu la kudhamini mgombeaji mahiri,” anasema Profesa Gitile Naituli.
Pili, wataponzwa na siasa za kikabila nchini, kwa kusawiriwa kama wasaliti wa makabila yao,” anasema Profesa Gitile Naituli.
Kulingana na mtaalamu huyo, tayari wabunge hao wameanza kung’amua ukweli kuhusu upungufu huu ndiposa wiki jana walidokeza kuwa wako tayari kushirikiana na mrengo wa aliyekuwa Naibu Rais Rigathi Gachagua na kiongozi wa Wiper Kalonzo Musyoka.
Akiongea katika Kanisa la Jesus Teaching Ministry, eneo la Embakasi Mashariki, Nairobi Mbunge wa Kitutu Chache Kusini Antony Kibagendi alisema ushirikiano huo ndio utawawezesha kufanikisha ajenda yao ya kuhakikisha Rais William Ruto anahudumu kwa muhula mmoja pekee.
“Tumeamua kushirikia kuokoa taifa hili kutoka kwa utawala dhalimu wa Kenya Kwanza. Hii ndio maana nawaomba wenzangu hapa kwamba tushirikiane na Kalonzo Musyoka, Rigathi Gachagua, George Natembeya, Fred Matiang’i na viongozi wote wa upinzani ili tukomboe nchi yetu,” akasema.
Pamoja naye walikuwa mwenyeji wao, Bw Owino, Seneta wa Nairobi Edwin Sifuna (ODM), Caleb Amisi (Saboti, ODM), Clive Gisairo (Kitutu Masaba, ODM) na Obadiah Barongo (Bomachoge Borabu, ODM).