Wabunge wageuza Bunge jukwaa la kukemea viongozi wa kidini
WABUNGE wamewasuta viongozi wa makanisa, wakiwaambia waachane na siasa na kuzingatia wajibu wao wa kulisha waumini chakula cha kiroho.
Wabunge hao waliwashutumu viongozi wa kidini kwa kuwapiga marufuku kuchanga pesa makanisani na kuwahusisha na ufisadi huku wakidai wameshindwa kushauri jamii na badala yake kujihusisha na siasa.
Kiongozi wa Wengi Kimani Ichung’wah aliwakemea vikali viongozi wa kidini akisema hawawezi kuwatishia wanasiasa ili wakome kuchangia maendeleo ya kanisa kwani ni viongozi hao hao wa kanisa wanaowaalika.
“Sijawahi kuona mwanasiasa akijialika kuchanga pesa kanisani; viongozi wa kidini wasifanye ionekane kuwa tunajialika makanisani ili kuchanga pesa, tuna maeneo mengine mengi tunayoweza kupeleka pesa hizi,” Bw Ichung’wah alisema.
“Tusiogope kuwaambia viongozi wetu wa dini kwamba tunapofanya mema na kutoa sadaka kanisani hatufanyi hivyo ili kuwafurahisha maaskofu, wachungaji au waumini wa kanisa, tunafanya hivyo kwa sababu inampendeza Mungu,”aliongeza.
Akirejelea michango iliyotolewa na Rais William Ruto katika kanisa Katoliki la Soweto, Nairobi, Bw Ichung’wah alisema ni viongozi wa kanisa hilo walioomba msaada.
“Nilikuwa na Rais na tulipokuwa tunakunywa chai, viongozi wa dini ndio walioomba msaada wa kujenga nyumba ya mkuu wa parokia. Nilipoona Askofu Mkuu akiandika barua kwamba watarudisha pesa, nilishtuka lakini naweza kuthibitisha kuwa hakuna hata senti moja iliyorudishwa, na wakirudisha kuna mamia ya makanisa yanayozisubiri,” Bw Ichung’wah. alisema.
Kiongozi wa Wachache Junet Mohamed alisema ni lazima viongozi wa kidini waheshimu viongozi waliochaguliwa na kwamba wanapaswa kuzungumzia masuala mahususi na wabunge badala ya kuwalaani kwa jumla kwenye vyombo vya habari.
Kiranja wa Wengi Silvanus Osoro aliwashutumu maaskofu akidai wananyamaza kuhusu mambo muhimu yanayoathiri jamii kama vile mauaji ya wanawake.
IMETAFSIRIWA NA BENSON MATHEKA