Wabunge wanavyotafuna hongo bila kujali raia
Ingawa Kanuni za Kudumu za Bunge zinawataka wabunge wote kuwa na nidhamu na uadilifu wanapotekeleza majukumu yao, hali halisi ndani ya majengo ya Bunge haifanani kabisa na mahitaji hayo ya kisheria.
Licha ya rekodi rasmi kuwaonyesha wabunge wakijadili hoja nzito kwa niaba ya Wakenya milioni 53, ndani ya vivuli vya majengo hayo, baadhi ya wabunge wa sasa na wa zamani wamekiri kuwa Bunge limegeuka kuwa ‘soko la dili’ ambapo pesa zina thamani zaidi kuliko masilahi ya wananchi.
Madai ya rushwa miongoni mwa wabunge yamekuwepo kwa muda mrefu lakini mara chache sana yamewahi kuthibitishwa kikamilifu, huku washukiwa wengi wakiwa wameepuka adhabu hata katika hali ambapo maamuzi ya Bunge yalienda kinyume na matakwa ya umma.
Kwa baadhi ya wabunge, kupiga kura ya “ndiyo” au “la” kunahusiana tu na kiasi cha fedha kinachotolewa. Hata hivyo, baadhi ya vyanzo vyetu vinaeleza kuwa bado kuna wabunge waadilifu wanaofanya kazi kwa moyo wa dhati kwa ajili ya wananchi.
Rais William Ruto, alipohutubu katika Kongamano 12 la Ugatuzi, aliwaomba wabunge waache tabia ya kudai hongo kutoka kwa watu wanaoitwa kufika mbele ya kamati za Bunge. Kauli hiyo ilifungua ukurasa mpya kuhusu tabia hii ambayo sasa imeonekana kuota mizizi Bungeni.
Ingawa baadhi ya wabunge walijibu kwa njia tofauti, idadi ya waliokiri kuwepo kwa tatizo hilo ni ishara kuwa rushwa imekita mizizi kiasi cha kutishia demokrasia ya wananchi.
Baada ya kupitishwa kwa Mswada wa Fedha wa 2024 licha ya upinzani mkali wa wananchi na wataalamu, madai ya rushwa yalizuka tena. Mnamo Juni 23, 2024, Mbunge wa Juja, aliibua madai kuwa kila mbunge aliyepiga kura ya “ndiyo” alipewa Sh 2 milioni, na kudai kuwa alikataa pesa hizo.
Naibu rais wakati huo, Rigathi Gachagua alikanusha madai hayo wiki moja baadaye. Hata hivyo, mwezi uliofuata, naye pia alidai kuwa wabunge walihongwa ili kuandaa njama ya kumng’oa madarakani.
Chanzo kutoka Bunge la Kitaifa kilisema kuwa wale wanaoitwa mbele ya kamati hulipia huduma hiyo bei ikiwa kati ya Sh100,000 hadi Sh10 milioni kulingana na uzito wa suala. Maswali hupeanwa mapema, na mara nyingine anayeitawa huruhusiwa kuandaa maswali yake mwenyewe kupitia maafisa wa wabunge.
Kamati kama za Uhasibu wa Umma (PAC) na Uwekezaji wa Umma (PIC) zinatajwa kuwa “yenye faida zaidi” kwa wabunge.
Uenyekiti wa kamati hizo huvutia malipo makubwa zaidi, huku viongozi wa mashirika ya serikali wakidaiwa kukusanya fedha kutoka kwa idara zao za fedha ili “kuwahudumia” wabunge.
Katika mojawapo ya kesi ambapo gavana alinusurika kuondolewa madarakani, inadaiwa alitumia zaidi ya Sh300 milioni, kuwashawishi maseneta waikatae hoja ya kumtimua. Kundi lililopanga kumng’oa lilikuwa limekusanya Sh110 milioni pekee.
Hii inaonyesha kuwa wakandarasi wa kaunti walilazimishwa kuchangia hadi Sh10 milioni kila mmoja, kwa ahadi kuwa wangepata zabuni baada ya gavana kurudi kazini.
Iwapo Waziri, Katibu au kiongozi wa shirika la serikali anatazamiwa kuondolewa, orodha mbili huandaliwa: wale wanaounga mkono na wanaopinga hatua hiyo. Orodha hizo hutumiwa kuwakamua wahusika fedha ili hoja hiyo ipuuzwe.
Waziri mmoja wa zamani alikumbuka:’Waliniletea orodha mbili wakitaka pesa ili hoja ya kuniondoa ifutiliwe mbali. Nilikataa.’
Mtaalamu wa masuala ya utawala, Barasa Nyukuri, alisema kuwa nia ya kuhoji viongozi wa serikali ni njema, lakini imegeuzwa kuwa chombo cha kuwatisha na kuwaibia maafisa wa serikali.
Aliyekuwa Mbunge wa Shinyalu, alisema kuwa visa vya rushwa bungeni ni vya muda mrefu na serikali pia huchangia. Alisema katika enzi za serikali ya muungano, pesa kutoka Ikulu zingesambazwa kupitia mawakala na viranja wa vyama ili kushawishi kura.
Kwa maneno yake:’Wakati Serikali inataka kupitisha mswada, hutuma pesa kwa viranja na wao huwapa wabunge maagizo ya namna ya kupiga kura. Ukiwa mbishi, wanakufuata binafsi na kuongeza.”
Alifichua pia kuwa wakati mwingine wabunge hutafuta pesa kutoka kwa mashirika ya serikali kwa madai kuwa fedha hizo uhitajika kwa niaba ya kamati nzima, kisha kamati hiyo huchapisha ripoti tofauti – hata ikipendekeza kushtakiwa kwa waliotoa hongo.
Spika wa Bunge la Kitaifa Moses Wetang’ula, naye alikiri bungeni kuwa baadhi ya wabunge wanadai pesa kutoka kwa mashirika ya serikali, jambo lililomfanya aelemewa na malalamishi.
Maseneta Moses Kajwang’ (Homa Bay), Godfrey Osotsi (Vihiga), na Mbunge wa Bumula Wanami Wamboka wamepuuzilia mbali madai ya Rais William Ruto kuwa wabunge hudai hongo kutoka kwa watu wanaofika mbele ya kamati za Bunge.
“Ninakubaliana na Rais kuwa ufisadi ni adui, lakini hatuwezi kulaumiwa kwa kazi ambazo hufanywa na Mhasibu Mkuu au EACC. Sisi si wachunguzi, ” Seneta Kajwang’, ambaye ni mwenyekiti wa Kamati ya Usimamizi wa Matumizi ya Fedha za Kaunti (CPAC), alisema.
Viongozi wengine, wakiwemo aliyekuwa Mwanasheria Mkuu Justin Muturi, Seneta wa Kisii Richard Onyonka, na Seneta wa Nairobi Edwin Sifuna, walimtaka Rais kuwasilisha majina ya wabunge waliopokea hongo kwa Tume ya Maadili na Kupambana na Ufisadi (EACC).
Msemaji wa EACC, Stephen Karuga, alifichua kuwa hadi sasa hawajapokea malalamishi rasmi ya wabunge kupokea hongo. Hata hivyo, alisisitiza kuwa ikiwa malalamishi yenye ushahidi yatapokelewa, uchunguzi utafanyika bila upendeleo.
“Tatizo ni kuwa wengi hutoa tuhuma za jumla bila ushahidi. Lakini tukipokea malalamishi ya kweli, hata wabunge tutawachunguza,” alisema Karuga.