Jamvi La Siasa

Wachache walikuwa wamesikia habari za Oketch Salah, jamaa aliyekuwa na ukaribu na Raila

Na JUSTUS OCHIENG' December 15th, 2025 Kusoma ni dakika: 3

NI watu wachache tu Kenya walikuwa wamesikia habari za Oketch Salah kabla ya kifo cha aliyekuwa waziri mkuu Raila Odinga.

Mtu huyu ambaye alikuwa na hadhi ya chini sasa amekuwa na mtindo wa maisha wa kutumia helikopta, kushiriki mikutano ya kibinafsi na marais na kupata ushawishi ambao umewashangaza wengi.

Kadri safari ya kisiasa ya Odinga ilivyokaribia kumalizika, Salah alijitokeza kwenye jukwaa la kisiasa. Kabla ya wakati huo, jina lake halikuwa na maana kubwa zaidi ya mji wa Migori, ambapo alikulia kama mtoto wa mfanyabiashara Ali Salah.

Katika miezi iliyofuata kifo cha Odinga, Salah amekuwa mmoja wa watu wanaozungumziwa sana lakini wasioeleweka sana nchini.

Wachache walikuwa wamesikia chochote kumhusu hadi hali ya afya ya Odinga ilipokuwa ikidhoofika na kumlazimu kiongozi huyo wa Chama cha Orange Democratic Movement (ODM) kutumia muda mrefu zaidi katika Falme za Kiarabu na India akitibiwa.

Ni wakati wa miezi hii nyeti ambapo Salah, ambaye alikuwa na urafiki wa muda mrefu na Odinga, alikuwa ubavuni pake.

Alipanga safari, akaungana na madaktari, akapeleka wataalamu, na alikaa usiku mrefu kando ya kitanda cha hospitali cha Odinga, kulingana na familia.

Lakini kujitokeza kwa Salah kwenye umma hakukutokana na simulizi za alivyokuwa akizunguka hospitalini bali mtindo wake wa maisha ulioonekana ghafla – safari za helikopta, ziara za kimataifa na picha akiwa na marais.

Helikopta iliwasili Bondo, Kaunti ya Siaya wakati wa mazishi ya dada wa Odinga, Beryl Achieng, Desemba 6.

Salah alishuka akiwa amevaa mavazi ya kistaarabu, akawakaribia wafiwa kwa urahisi wa mtu aliyezoea taratibu za VIP.

Kwa wengi huko Bondo, ilikuwa mojawapo ya mara chache walizomuona baada ya mazishi ya Odinga, akitokea kwa mtindo wa kipekee wa wale waliokubalika na madaraka.

Mitandao ya kijamii ya Salah inaonyesha safari za mara kwa mara na mikutano ya hadhi ya juu.

Ikiwa helikopta ziliibua maswali, mikutano yake na marais ilifanya siasa kuwa kali.

Mnamo Jumanne, Desemba 9, Bw Salah alichapisha picha akiwa amesimama kando ya Rais wa Zimbabwe, Emmerson Mnangagwa, akiwa na binti yake: “Tulifanya majadiliano ya manufaa kuhusu fursa za kibiashara katika uchimbaji madini, nishati na kilimo,” aliandika kuhusu picha hiyo.

Mkutano wa kibinafsi wa Mkenya na rais wa nchi za kigeni kuhusu biashara na maendeleo si jambo la kawaida.

Hii inaashiria hadhi, ushawishi na mitandao ambayo inazidi mipaka ya Kaunti ya Migori au familia ya Odinga.

Mnamo Desemba 2, Salah alikaribishwa katika Ikulu na Rais William Ruto kwenye hafla ya kusherehekea ushindi wa wagombeaji wa ODM na United Democratic Alliance (UDA) katika uchaguzi mdogo wa Novemba 27.

Mbali na kiongozi wa ODM, Oburu Oginga, hakuna kiongozi mwingine wa chama aliyehudhuria tukio hilo.

“Nashukuru uongozi wa Rais William Ruto na Dkt Oburu Oginga,” alichapisha kwenye mitandao ya kijamii.

Ujumbe ulikuwa wazi kwamba Salah yuko katikati ya makubaliano ya kisiasa kati ya Ruto na Odinga.

Kadri umaarufu wa Salah ulivyoongezeka, ndivyo kizungumkuti kilivyokuwa kikikua. Hakuna aliyesema hilo kwa uwazi zaidi kuliko dada wa Odinga, Ruth, ambaye pia ni Mbunge wa Kisumu.

“Simjui. Nilipoenda India kumuona Raila, yeye alirudi Kenya. Sijui kwa nini. Sasa yuko kila mahali na Dkt Oburu Oginga. Nimeulizwa ni nani na siwezi kueleza. Lazima upate kujua ni nani,” alisema.

Umaarufu wa Salah haujakuwa bila utata. Mnamo Novemba, alichapisha picha akiwa kwenye hafla ambayo alitaja kama ya familia – harusi ya mwana wa Mkurugenzi wa Huduma za Ujasusi za Taifa, Noordin Haji.

“Ni heshima kushiriki na Dkt Oburu Odinga katika kusherehekea mtoto wa binamu yangu Noordin Haji,” aliandika.

Majibu yalikuja papo hapo. Bw Haji alikanusha dai hilo kwa nguvu siku ya Alhamisi: “Hapana. Tunaweza kufanya DNA.”

Hilo liliongeza tu siri kuhusu Salah na mitandao yake, na kuibua maswali kuhusu watu anaoshirikiana nao na kwa nini.

Mahojiano na wale wanaomjua baba yake wanasema Abdi alikuwa na mmiliki wa Salah Bakery, mojawapo ya biashara za zamani za mji huo, na alihusikika kujenga jengo la kwanza la ghorofa Migori katika miaka ya 1970 – jambo lililothibitisha hadhi ya familia hiyo kama wazoefu wa mji.

“Tulikuwa na Oketch Salah katika Shule ya Upili ya Migori katika miaka ya 1990 lakini aliondoka. Siwezi kusema alimalizia wapi masomo yake ya sekondari,” alisema mmoja wa waliosoma naye shuleni.

Sehemu kubwa ya umaarufu wa hivi karibuni wa Salah ilianza karibu na wakati wa harusi ya mtoto wake Abdinoor Oktoba 25, takribani siku 10 baada ya kifo cha Odinga.

Sherehe hiyo katika Hoteli ya Serena ilikuwa hafla tulivu lakini ya nguvu, iliyohudhuriwa na Dkt Oginga, Waziri wa Kawi na Petroli James Opiyo Wandayi na viongozi wengine.

Ni katika tukio hili ambapo Dkt Oginga alifichua uhusiano wa Salah na Odinga.

“Oketch Salah alikuwa rafiki mzuri na mtoto wa Raila. Alimtunza Raila hadi siku alipopumua. Sasa Raila akiwa ameondoka, nimemrithi kama mtoto wangu,” alisema seneta wa Siaya.

“Raila aliacha ODM katika serikali jumuishi. Tunaendelea kufanya kazi na Rais Ruto kutekeleza ajenda ya vipengele 10.”

Maneno haya yalithibitisha umuhimu wa Salah. Yalimuweka ndani ya muundo wa ushirikiano wa kisiasa unaoibuka nchini Kenya.