Jamvi La Siasa

WALIOBOBEA: Kibaki alivyochukizwa na siasa duni

Na BENSON MATHEKA December 15th, 2025 Kusoma ni dakika: 2

STANLEY Emilio Mwai Kibaki, Rais wa nne wa Kenya, alionyesha mfano wa uongozi wa kipekee uliojikita katika ufanisi wa kiuchumi na mabadiliko makubwa katika elimu na demokrasia.

Kibaki alikataa siasa duni, akakumbatia kuboresha maisha ya wananchi na kuipeleka Kenya mbele kiuchumi, huku akiepuka utovu wa nidhamu kisiasa.

“Rais Kibaki alijulikana kwa mtindo wake wa utawala wa kisomi na kitaalamu, uliofanikisha miradi ya maendeleo, licha ya changamoto za kisiasa zilizokumba nchi wakati wa utawala wake,” unasema wasifu wake katika Kenya Year Book.

Aliingia madarakani mnamo Desemba 2002 kwa msaada wa wanasiasa waliokuwa wameasi chama cha Kanu. Licha ya mivutano iliyokuwepo wakati wa uchaguzi, Kibaki alifanya mageuzi makubwa katika siasa za Kenya.

Changamoto kubwa ya utawala wake ilikuwa ghasia za baada ya uchaguzi wa 2007. Kibaki alijizatiti kurejesha utulivu na kupambana na migogoro ya kisiasa kwa kutumia njia za kidiplomasia.

Miongoni mwa mafanikio yake makubwa ni mageuzi ya kiuchumi ambayo yaliathiri maisha ya kila Mkenya, kama vile ushirikiano wake na sekta ya kibiashara, ujenzi wa miundombinu, na kuanzisha mikakati ya maendeleo ya kiuchumi kupitia miradi kama vile barabara na hospitali.

Pia, Kibaki anakumbukwa kwa mafanikio makubwa katika mabadiliko ya kisheria. Mnamo 2010, aliongoza nchi kupitisha Katiba Mpya ya Kenya.

Katiba hii iliruhusu mageuzi ya kisiasa na kijamii, ikiwa ni moja ya mafanikio makubwa ya utawala wake.

Japo baadhi ya viongozi wamekuwa wakiahidi kuiga utawala wake, wanatenda tofauti kwa kukumbatia siasa za malumbano.

Katika zaidi ya miongo mitano aliyohudumu katika siasa, Kibaki alijulikana kwa kuepuka siasa duni.

Alikuwa kiongozi aliyejitahidi kuepuka migogoro isiyo ya lazima na mara nyingi aliishi kwa misingi ya nidhamu na umakini.

Hii ilimfanya kuwa kiongozi ambaye alikuwa na ushawishi mkubwa si tu kwa wananchi wa Kenya bali pia kwa viongozi wa kimataifa.

Alisifiwa na viongozi wa kimataifa kwa mchango wake katika maendeleo ya kiuchumi na utawala bora.

Inasemekana hata ghasia za baada ya uchaguzi wa 2007 zilitokana na misimamo mikali ya washirika wake waliotaka kulinda mamlaka na aliposhindwa kuvumilia kuona nchi ikielekea pabaya, alizingatia hatua za kidiplomasia.

Baada ya utulivu kurejea, alijikita zaidi katika masuala ya kiuchumi na maendeleo na kuleta mabadiliko makubwa na kuifanya Kenya kuwa moja ya nchi zilizoendelea kwa haraka licha ya kuwa aliingia mamlakani uchumi ulipokuwa ukiyumba.

Alizingatia utekelezaji wa miradi ya maendeleo kama vile ujenzi wa miundombinu ya kisasa. Hatua hii ilisaidia sana kukuza uchumi wa nchi na kupunguza umaskini kwa wananchi wengi.

Katika maisha yake ya kisiasa, Kibaki alijitahidi kutimiza malengo yake bila kujali changamoto alizokutana nazo. Alikuwa mtetezi wa maslahi ya wananchi, na alielekeza juhudi zake kutoa huduma bora za afya, elimu na miundombinu.

Rais Kibaki pia alitekeleza jukumu muhimu katika kupigania uhuru wa kisiasa. Alikuwa na maono ya taifa lenye demokrasia na haki kwa kila Mkenya, na alikataa siasa za dhuluma.

Katika kipindi chake cha uongozi, alijitahidi kuhakikisha kuwa wananchi wanapata haki zao za kikatiba na kisiasa. Hii ilikuwa ni hatua kubwa kuafikia demokrasia ya kweli katika taifa hili.

“Kibaki alikataa siasa duni za aina yoyote. Alijua kuwa siasa za matusi, ubinafsi, na migogoro hazikuwa na manufaa kwa taifa. Badala yake, alikusudia kuboresha utawala wa nchi, kuboresha huduma za umma, na kutoa fursa sawa kwa kila Mkenya. Katika kipindi chake cha utawala, alihimiza umuhimu wa maendeleo na usawa katika jamii,” asema mchanganuzi wa siasa David Kimengere.

Anasema licha ya pandashuka za utawala wake hasa ghasia za baada ya uchaguzi alipokuwa akisaka muhula wa pili, alionyesha uongozi wa kweli, alipanua uhuru wa raia na demokrasia na matokeo yakawa kuvutia uwekezaji na kuimarika kwa demokrasia.

“Hakuwa mtu wa maneno mengi. Siasa zake zilikuwa za kimkakati na kitaalamu. Alianzisha elimu bila malipo bila kukopa pesa na huo ukawa ufanisi wake mkubwa,” alisema.