Jamvi La Siasa

WALIOBOBEA: Njonjo alimtetea Moi… kisha wakawa maadui

Na BENSON MATHEKA December 7th, 2025 Kusoma ni dakika: 2

SIR Charles Mugane Njonjo alipohudumu kama Mwanasheria Mkuu wa Kenya, mabadiliko mengi ya Katiba yalipitishwa Bungeni na kuchangia kile kilichokuja kujulikana kama urais wa kifalme kutokana na mamlaka makubwa aliyopewa Rais.

Katika kusukuma mageuzi hayo na kutekeleza maamuzi magumu ya Serikali, Njonjo alikabiliana vikali na upinzani mkali kutoka kwa kundi la wabunge vijana saba aliowatwika jina la utani “Seven Bearded Sisters.”

Wabunge hao walikuwa Koigi wa Wamwere, Mwashengu wa Mwachofi, James Orengo (sasa gavana wa Siaya), Chelagat Mutai, Abuya Abuya (baadaye kamishna wa IEBC), Onyango Midika na Lawrence Sifuna.

Akieleza baadaye, Njonjo alisema: “Bunge wakati mwingine lilikuwa la kuchekesha; baadhi walidhani wangeweza kufanya lolote bila kuwajibika. Niliwakabili moja kwa moja. Hawa vijana saba walikuwa werevu, lakini sikuweza kuruhusu werevu wao kugeuka kiburi cha kuwaongoza wengine.”

Mamlaka yake yalitokana na nguvu za urais, kiasi kwamba aliweza kusukuma marekebisho ya Katiba kwa siku moja ili kuruhusu Mzee Jomo Kenyatta kumwondolea adhabu Paul Ngei, ambaye alikuwa amezuiwa na mahakama kugombea uchaguzi kutokana na kosa la uchaguzi.

Njonjo alitetea msimamo wake wa kumshtaki mbunge yeyote aliyepatikana na makosa, akijivunia jinsi alivyoendesha uchunguzi dhidi ya Jesse Gachago na Muhuri Muchiri walionaswa katika biashara haramu ya magendo ya kahawa kutoka Uganda miaka ya 1970.

Kwa wanaozingatia sheria, Njonjo alikuwa ngao; kwa wavunjaji wa sheria, jina lake pekee lilitosha kuwatetemesha.

Marafiki zake wa karibu kisiasa walikuwa wachache—miongoni mwao Rais Moi, Waziri Msaidizi G.G. Kariuki na Waziri wa Fedha Mwai Kibaki (ambaye baadaye walitofautiana).

Alihusika kwa karibu zaidi na watumishi wa umma wa ngazi ya juu Geoffrey Kareithi, Jeremiah Kiereini na mkuu wa ujasusi James Kanyotu, aliyekuwa pia mshirika wake wa kibiashara.

Kuhusu urithi wa uongozi baada ya Kenyatta, Njonjo alisema alifuata Katiba kikamilifu, kwani ilielekeza Makamu wa Rais kuchukua hatamu kwa siku 90 kabla ya uchaguzi mpya.

Alipinga vikali njama zilizokuwa zikifanywa na baadhi ya wanasiasa kuchelewesha kutangazwa kwa kifo cha Kenyatta.

“Nilihakikisha mwili ulipowasili Nairobi kutoka Mombasa, kifo kilitangazwa na Moi akateuliwa Kaimu Rais,” alifichua.

Alisumbuliwa sana na mauaji ya viongozi Tom Mboya (1969) na J M Kariuki (1975), akisema uchunguzi ulivurugwa na siasa.

Kuhusu Kamati ya Bunge iliyoongozwa na Elijah Mwangale, Njonjo alisema: “Niliwaambia waache CID ifanye kazi. Lakini walisisitiza kumhoji hata Moi na mimi mwenyewe. Lau uchunguzi ungeachwa kwa CID, tungelifikia ukweli.”

Njonjo alioa akiwa na umri wa miaka 52, mnamo Novemba 20, 1972. Anasema alichelewa kuoa kwa sababu alikuwa “ameolewa na kazi yake.” Lakini shinikizo la Kenyatta na wazazi wake lilimfanya ajitafutie mchumba.

Mnamo 1976, kundi la wanasiasa kutoka Mlima Kenya, Bonde la Ufa na Mashariki lilizindua kampeni ya kubadilisha Katiba ili kuzuia Moi kurithi urais endapo Kenyatta angefariki.

Njonjo, mshirika imara wa Moi, alikabili vikali kampeni hiyo akisema ilikuwa “kosa la jinai hata kufikiria kifo cha Rais.” Hatimaye Kenyatta aliitisha kikao na kukomesha mjadala huo.

Baada ya Kenyatta kufariki 1978, Njonjo ndiye aliyehakikisha Moi alichukua madaraka kikatiba. Lakini miaka mitano baadaye, mtu huyo huyo aliyemsaidia akawa adui yake mkuu.

Baada ya kujiuzulu wadhifa wa Mwanasheria Mkuu na kuchaguliwa Mbunge wa Kikuyu, Njonjo aliteuliwa Waziri wa Sheria na Masuala ya Katiba.

Lakini 1983 alishutumiwa kupanga “kumpindua Moi.” Tume ya Jaji Cecil Miller ilimchafua hadharani na kumaliza kabisa taaluma yake ya kisiasa.

Alikumbuka tuhuma hizo kama “porojo za watu waliotaka kuniondoa kwenye mpangilio wa mamlaka.”

Anasema angekuwa na nia ya kweli ya kumzuia Moi 1976, angeungana tu na kundi lililotaka Katiba ifanyiwe marekebisho wakati huo kumzuia makamu rais kuingia mamlakani iwapo rais angefariki.

“Nilitoka nikiwa nikijionea fahari, licha ya majaji waliokiuka sheria,” alisema.

Baada ya kuporomoka kisiasa kufuatia tofauti zake na Moi, Njonjo alizamia katika biashara hadi alipofariki Januari 2, 2022 akiwa na umri wa miaka 101.