Jamvi La Siasa

Wamalwa aapa heri baridi katika upinzani, kuliko joto serikalini ya Ruto

Na BENSON MATHEKA December 21st, 2025 Kusoma ni dakika: 1

KIONGOZI wa chama cha Democratic Action Party–Kenya (DAP-K), Eugene Wamalwa, anadai kuwa Rais William Ruto alijaribu kumpa wadhifa wa Waziri wa Ulinzi ili kumvuta upande wake kuelekea uchaguzi wa 2027.

Akizungumza katika mahojiano na kituo kimoja cha redio humu nchini mnamo Alhamisi, Bw Wamalwa alisema kuwa baada ya Aden Duale kuhamishwa kutoka wizara hiyo kufuatia mabadiliko ya Baraza la Mawaziri, rais alimtumia wajumbe kumrai achukue nafasi hiyo.

Bw Wamalwa alisema alikataa na kumwambia rais kuwa hana nia ya kujiunga na serikali, akichagua kubaki katika upinzani.

Alidai kuwa rais, akitambua nguvu inayoongezeka ya Muungano wa Upinzani ni tishio kwa azma yake kupata muhula wa pili wa mwaka 2027, amekuwa akitumia mbinu tofauti kuwarai viongozi wa upinzani kujiunga na serikali.

“Rais William Ruto amekuwa akituma watu kwetu ili tujiunge na serikali yake. Baada ya Duale kuondoka Wizara ya Ulinzi, alitaka nichukue nafasi yake lakini nilimwambia siwezi,” alisema Bw Wamalwa.

Alisisitiza kuwa lengo la Muungano wa Upinzani ni kuzuia kuchaguliwa tena kwa Rais Ruto mwaka 2027, kurejesha sera zilizokuwa maarufu kama Linda Mama na NHIF zilizotekelezwa wakati wa utawala wa Uhuru Kenyatta, na kubatilisha sera kandamizi za serikali ya sasa.

Kauli yake inajiri siku chache baada ya fununu kusambaa kuwa yeye na kiongozi wa Wiper, Kalonzo Musyoka, walikuwa wakishawishiwa kujiunga na serikali.

Hii ilimfanya aliyekuwa Naibu Rais Rigathi Gachagua kusema kuwa ikiwa Rais Ruto anataka kuzungumza na Kalonzo au Eugene, lazima apitie kwake kwa kuwa wote ni “binamu.”

Alidai kuwa vyama vidogo vidogo vinasajiliwa ili kupunguza nguvu katika ngome za upinzani.