Jamvi La Siasa

Wazee Mlimani wataka wenzao Rift Valley wakome kuwapimia hewa

May 24th, 2024 Kusoma ni dakika: 2

NA MWANGI MUIRURI

WAZEE wa Mlima Kenya wameteta kuhusu tabia ya wandani wa Rais William Ruto kujitwika wajibu wa kunyapara ndoa ya kisiasa ambapo viongozi wazawa wa maeneo hayo mawili walilishana yamini ya uwaniaji urais mwaka 2022 na wakafaulu.

Mwenyekiti wa Baraza la Agikuyu Bw Wachira Kiago akihutubu katika kikao cha Mei 23, 2024, katika Mkahawa mmoja ulioko Kaunti ya Kiambu alisema kwamba “wanafaa kupunguza kasumba ya kutupa mwongozo na wao”.

“Kuna wanasiasa wa mrengo wa Rais ambao wanajichukulia kama nyapara wa Mlima Kenya ndani ya hiyo ndoa iliyowaleta pamoja Rais Ruto na Naibu Rais Rigathi Gachagua,” akasema Bw Kiago.

Bw Kiago alisema kwamba “huko kuchambuliwa sisi wa Mlimani tukianza mikakati ya kuungana ili tujipe mwelekeo wa 2027 halafu tunaambiwa tuko na ukabila si sawa”.

Alidai kwamba ndoa hiyo ya kisiasa yam waka 2022 hata haikusajiliwa popote na haina cheti wala mahari.

Bw Gachagua tayari ashakiri kwamba Mlima Kenya haukutia saini mkataba wowote wa uhusiano wa awamu ya 2022 hadi 2027.

“Hapakuwepo na haja ya kuweka maelewano yetu ndani ya mkataba rasmi kwa kuwa Rais Ruto ni muungwana, mstaarabu na mwadilifu,” aliwahi kusema Bw Gachagua.

Bw Kiago sasa anadai kwamba ndoa ya aina hiyo haina ukwe ulio na mikakati na ndio sababu “kila kuchao tunawaona wandani wa Rais Ruto wakizidisha njama za kumhujumu Bw Gachagua kupitia kutumia badhi ya wenzetu wa papa hapa Mlimani”.

Bw Kiago alisema haifai baadhi ya viongozi wa kutoka Rift Valley, ambako ni ngome ya Rais, kuchukua maikrofoni hadharani “kutuzomea eti tunakutana kikabila”.

Bw Kiago aliongeza kwamba hadi sasa ndoa ya 2022 ya kisiasa imeanza kumkosea heshima bi harusi kutoka Mlimani.

“Ni lazima tuanze kukutana ili tupange namna ya kujinusuru, tuondoke ikibidi na kisha tuoge turejee kwa soko,” akasema.

Aliwataka wanasiasa hao waelewe kwamba jamii yoyote iko na uhuru wa kupanga mikakati yake ya baadaye pasipo nwingilio wa nyingine.

“Wakutane kivyao, wajipange na kisha sisi tufanye hivyo kivyetu kisha tukutane kila mmoja kwa mavuno ama sokoni 2027,” akasema.