Jamvi La Siasa

Wetangula afufua ndoto ya umoja wa Magharibi

Na BENSON MATHEKA September 28th, 2025 Kusoma ni dakika: 3

Spika wa Bunge la Taifa Moses Wetang’ula amefufua tena wito wa muda mrefu wa kuunganisha jamii za Magharibi, akihimiza viongozi na wananchi kuungana chini ya ajenda moja kuelekea uchaguzi mkuu wa 2027.

Akizungumza katika eneobunge la Lugari, Kaunti ya Kakamega, wakati wa hafla ya kuwawezesha wanawake iliyoandaliwa na Mbunge Nabii Nabwera, Wetang’ula alisema ni wakati wa jamii ya Waluhya kuwa na sauti moja, yenye mshikamano na malengo ya pamoja.

Wetang’ula alisema kwamba yuko tayari kufanya kazi kwa karibu na viongozi kama Musalia Mudavadi na Wycliffe Oparanya, akisema “umoja wa makusudi hauna mipaka.”

“Umoja wa jamii ya Magharibi sio tu wa kisiasa bali ni wa kimaendeleo. Ni lazima tuunge mkono serikali ya Rais Ruto kwa sababu inaweka maslahi ya taifa mbele,” alisema Wetang’ula.

Alitaja mafanikio mbalimbali yaliyopatikana chini ya utawala wa Kenya Kwanza, ikiwemo ujenzi wa barabara ya Musikoma–Mung’ang’a, barabara ya Turbo–Naitiri–Sikhendu–Endebes inayounganisha kaunti nne, pamoja na ukarabati wa Uwanja wa Masinde Muliro. Aidha, alitaja juhudi za kufufua viwanda vya sukari na ajira kwa walimu kama mifano ya serikali inayojali eneo hilo.

Wito wake uliungwa mkono na Mbunge wa Navakholo Emmanuel Wangwe na mwenzake wa Kimilili Didmus Barasa, wakisema jamii hiyo itapata heshima ya kitaifa endapo itaungana.

“Tukiwa na sauti moja, tutakuwa na nguvu ya kushawishi mustakabali wa taifa hili. Lakini tukigawanyika, tutajipoteza kisiasa,” alisema Barasa.

Licha ya kauli hizi za mshikamano, wachanganuzi wa siasa wanaonya kuwa umoja huo si kazi rahisi, kutokana na migawanyiko ya kiitikadi na matakwa ya kisiasa miongoni mwa viongozi wa eneo hilo.

Moja ya vikwazo vikubwa ni kuibuka na umaarufu wa vuguvugu la ‘Tawe’ linaloongozwa na Gavana wa Trans Nzoia, George Natembeya. Vuguvugu hili limekuwa likilaumu vigogo wa kisiasa kama Wetangula na Mudavadi kwa kutojali maslahi ya jamii za magharibi mwa nchi.

Wachambuzi wanasema kuwa Natembeya amepata umaarufu mkubwa, hasa miongoni mwa vijana, kwa sababu ya lugha yake ya moja kwa moja na msimamo wa kutokuwa mnafiki kisiasa.

“Ukitazama idadi ya watu wanaomwamini Natembeya kama sauti ya kisasa ya Magharibi, ni dhahiri kuwa Wetang’ula anakabiliwa na upinzani mkali wa umaarufu,” alisema mchambuzi wa siasa Tom Wekesa.

Seneta wa Nairobi Edwin Sifuna pia ameanzisha mchakato unaoitwa Kenya Moja, ambao unasisitiza haki za kijamii, mageuzi, na kujitokeza kwa uongozi mpya wa vijana kutoka Magharibi.

Sifuna na wanasiasa wengine vijana wanakosoa serikali ambayo Wetangula anaunga.

Wachambuzi wanasema kuwa Kenya Moja inavutia sehemu ya wapiga kura vijana wanaohisi hawawakilishwi ipasavyo katika miundo ya sasa ya kisiasa.

Aliyekuwa Waziri wa Ulinzi na kiongozi wa chama cha DAP-K, Eugene Wamalwa, amekuwa akieleza wazi nia yake ya kuwania urais mwaka 2027. Wamalwa, ambaye yuko katika upinzani, amekuwa akikosoa Wetang’ula.

Wachanganuzi wanaona kuwa tamaa ya vigogo wa kisiasa inaweza kuathiri mpango wowote wa kuunda umoja wa Magharibi anaopigania Wetang’ula.

“Kila mmoja anataka kuwa dereva wa gari la Magharibi. Ikiwa hakutakuwa na mwafaka kuhusu nani aongoze, basi gari hilo litalemaa,” anasema Dkt Edward Barasa wa shirika la uchambuzi wa sera za umma.

Kwa sasa, matarajio ya umoja wa Magharibi yanategemea uwezo wa viongozi kuweka kando maslahi binafsi na kuja pamoja kwa msingi wa maendeleo.

Kulingana na wachambuzi, Wetang’ula bado ana nafasi ya kufanikisha wito wake endapo atatambua na kushirikisha sauti zote zenye ushawishi wakiwemo akina Sifuna, Natembeya, Wamalwa na wengine; atawezesha kuwepo kwa mchakato huru wa kuamua msemaji mmoja wa jamii; na kuhimiza ajenda ya pamoja ya maendeleo, badala ya kugawanya jamii kwa misingi ya mirengo.

“Ni kweli, Wetang’ula ana nguvu ya kikatiba na ushawishi wa kiutawala, lakini atahitaji kujenga daraja la kisiasa kati ya makundi hasimu,” asema Wekesa.

Wachambuzi wanasema wito wa Wetang’ula ni wa maana hasa kwa jamii ambayo kwa muda mrefu imekuwa ikilaumiwa kwa kukosa mwelekeo mmoja wa kisiasa.

“Lakini kwa sasa, njia ya kuelekea umoja huo bado ina miiba. Mirengo ya Natembeya, Kenya Moja ya Sifuna, na azma ya urais ya Wamalwa — zote ni vikwazo kwa ndoto ya umoja wa Magharibi,” asema mchanganuzi wa siasa Peter Wanyama.

Anasema ili Wetang’ula afanikishe azma yake, itamlazimu kuwa mpatanishi, msikivu, na mbunifu zaidi ya kuwa msemaji. La sivyo, eneo litaendelea kugawanyika kisiasa mwaka 2027.