Winnie akoroga siasa kwa kauli ya urais 2027
KAULI ya Mbunge wa Bunge la Jumuiya ya Afrika (EALA) Winnie Odinga kuwa ODM itakuwa na mwaniaji wa urais 2027 imeibua taharuki kuhusu ushirikiano baina ya chama hicho na UDA katika uchaguzi mkuu ujao.
Aidha, tangazo lake hilo linatarajiwa kuchemsha siasa za ukanda wa Luo Nyanza ikiwa imesalia miezi 18 kabla ya uchaguzi mkuu wa 2027.
Bi Winnie, mwanawe Waziri Mkuu wa zamani marehemu Raila Odinga wikendi alisema chama hicho kitakuwa na wawaniaji katika ngazi zote za uongozi mnamo 2027 ikiwemo urais.
“Madhumuni ya chama chochote kile cha kisiasa ni kuchukua mamlaka yote na ninaamini kuwa lazima ODM iwe na wawaniaji kila mahali. Hiyo ndiyo sababu ya kuwa na chama cha kisiasa na hiyo ndiyo demokrasia, si lazima watu wote wafikirie kwa njia inayofanana,” akasema Bi Winnie, akizungumza katika Shule ya Wasichana ya Pioneer ambayo inamilikiwa na bwanyenye Peter Munga.
“Watu sharti washindane na lazima ODM iwe tayari kushindana na pia nasi tuwe tayari,” akaongeza.
Kauli ya ODM kuwania urais inajiri baada ya Bi Winnie kusema kuwa kulikuwa na baadhi ya wanasiasa ambao walikuwa wakipanga kuuza ODM.
Alisema hayo wakati wa maadhimisho ya miaka 20 ya uwepo wa ODM mwezi uliopita.
Bi Winnie ameonekana kumakinikia siasa za ODM kuwasilisha mpeperushaji wa urais baada ya kutaka pia chama kiwe na mwakilishi wa kushauriana na Rais Ruto ndani ya Serikali Jumuishi kutokana na kutokuwepo kwa Raila.
“Ushirikiano ndani ya Serikali Jumuishi kwa sasa ni mgumu. Je wanaousimamia wanaweza? Kuna Baba Raila Odinga mmoja tu ambaye angeuweza,” akasema wakati wa maadhimisho ya ODM.
Alitoa wito wa kuandaliwa kwa Kongamano la Kitaifa la Chama (NDC) ili wanachama waamue kuhusu mwelekeo wa ushirikiano wa ODM na UDA.
Baada ya kuonekana kutofautiana kimaoni na amu yake, Dkt Oburu Oginga, ambaye ni kiongozi wa ODM, Bi Winnie wikendi alikanusha kuwa kuna uhasama wowote wa kisiasa ndani ya familia ya Bw Odinga.
“Ni ami yangu na ndiye baba pekee niliyebaki naye. Tunaweza kutofautiana kimaoni lakini ukweli ni kwamba sote tuko pamoja katika kuimarisha chama cha ODM,” akasema akiwa Kaunti ya Murang’a.
Dkt Oginga mwenyewe aliashiria kuwa ODM iko tayari kushirikiana na Rais Ruto 2027 na akasema wadhifa wa chini zaidi ambao wanaweza kuukubali ni ule wa mgombeaji mwenza.
Kauli ya Winnie vilevile inatarajiwa kuchemsha siasa za Luo Nyanza ambako baadhi ya wanasiasa wakuu tayari wamesema watamuunga mkono Rais William Ruto mnamo 2027.
Waziri wa Kawi Opiyo Wandayi na mwenzake wa Fedha John Mbadi wamekuwa mstari wa mbele kumpigia debe Rais Ruto kurejea ikulu 2027.
Wawili hao wamekuwa wakishikilia kwamba hakuna mwanasiasa ambaye anatosha kuvalia viatu vya Raila na anayetosha kuwania urais 2027.
“Mtu pekee alisimama na Raila na hata kusulubishwa kwa kufanya hivyo ni William Ruto. Ukisema ODM inaweza kutoa mwaniaji wa urais, hakuna mtu amekuzuia, endelea,” akasema Bw Wandayi wiki jana akiwa eneobunge la Gem.
“Ukitaka kuwania urais kupitia ODM tafadhali endelea na tuone utapata kura ngapi? Sisi kama jamii ya Waluo tumeamua kumuunga mkono Rais Ruto, ukitaka kuwania urais, endelea mbele lakini nakuhakikishia hutafanikiwa,” akaongeza.
Waziri huyo alisisitiza kuwa ataongoza kampeni za Rais William Ruto, Kaunti ya Siaya, akisisitiza kwa sasa hakuna mwanasiasa mwenye uwezo na rasilimali za kufanya kampeni za urais alivyofanya Raila.
“Ruto ndiye rais wa kwanza kuhakikisha maendeleo yanafika hapa Nyanza. Njia pekee kwa watu wetu kuendelea kunufaika ni kumuunga mkono Rais Ruto 2027,” akasema.
Bw Mbadi naye alisema analenga kuwania urais 2032 baada ya Rais Ruto kumaliza hatamu yake.
“Tuwaambie watu wetu ukweli kwa sababu hii ndiyo serikali ambayo imetufikiria. Sisi tutamuunga mkono Rais 2027 kisha 2032 tujiandae kuchukua urais. Kwa sasa hakuna mwanasiasa hapa Nyanza ambaye anaweza kuwania urais,” akasema Bw Wandayi.