Jamvi La Siasa

Winnie aonyesha ni mtoto wa simba kwa ujasiri wa Raila

Na CHARLES WASONGA December 8th, 2025 Kusoma ni dakika: 2

BINTIYE aliyekuwa kiongozi wa ODM, Hayati Raila Odinga, Winnie Odinga anazidi kujitokeza kama anayebeba sifa za kisiasa za kiongozi huyo aliyefahamika kama mwanamageuzi hodari na mtetezi sugu wa haki za wanyonge na demokrasia.

Winnie, anayehudumu kama Mbunge katika Bunge la Jumuiya ya Afrika Mashariki (EALA) amejichora kama jasiri, mkakamavu na mwenye kipawa cha kuvutia hadhira, hali inayoonyesha kuwa ndiye mrithi nambari moja wa siasa za babake zilizotawala taifa hili kwa zaidi ya miongo mitatu hadi alipofariki Oktoba 15.

Tangu wakati huo, Winnie ambaye ni kitinda mimba wa Raila, ameibua midahalo katika majukwaa ya kisiasa na kwenye mitandao ya kijamii kutokana na hotuba zake kali sawa na alizotoa babake nyakati za uhai wake.

Baada ya kifo cha babake, mbunge huyo alidiriki kuukosoa uongozi wa ODM, unaoongozwa na mjomba wake Oburu Oginga, kuhusiana na unavyosimamia ushirikiano wa chama hicho na mrengo wa Rais William Ruto katika Serikali Jumuishi.

Isitoshe, wakati wa sherehe za maadhimisho ya miaka 20 tangu kubuniwa kwa ODM zilizofanyika Mombasa mwezi jana, Winnie alitoa madai makali kwamba kuna njama ya baadhi ya vigogo kukiuza chama alichokianzisha baba yake.

“Wapo wanaotembea nasi mchana lakini usiku wanajadili chama katika mazungumzo ya faraghani.

“Hilo halitabadilisha lolote kwa sababu ODM haiwezi kumezwa. Hiki ni chama cha raia, na kilianzishwa kupigania maslahi yao kwa uwazi sio kisiri. Na ningependa kusema hapa kwamba ODM haitamezwa wala kuuzwa na yeyote,” akaongeza Bi Winnie.

Mbunge huyo wa EALA alipendekeza kuitishwa kwa Kongamano la Kitaifa la Wajumbe (NDC) wa ODM ili wanachama waamue yule anayefaa kusimamia uhusiano wake na serikali ya Rais Ruto.

Hapa alionekana wazi kuhoji uwezo wa mjomba wake, Dkt Oginga, kusimamia kile alichokitaja kama ‘mpango mgumu’. Alisema unahitaji ujuzi na weledi sawa na wa marehemu baba yake.

Pendekezo hilo na kauli zake kali katika jukwaa hilo la sherehe za ODM@20 ziliwaacha viongozi wengi wa chama hicho vinywa wazi akiwemo Dkt Oginga aliyemsema, “Jambo alilosema mtoto wangu Winnie tutalijadili kinyumbani.”

Msimamo mkali wa Winnie umemfanya kuonekana kuongea lugha sawa na viongozi waasi wa ODM wanaopinga serikali jumuishi kama vile Katibu Mkuu Edwin Sifuna na Mbunge wa Embakasi Mashariki Babu Owino, miongoni mwa wengine.

Waama, alipopewa nafasi ya kuhutubu Jumamosi katika ibada ya mazishi ya shangazi yake, Berly Achieng Odinga, Winnie alitumia fursa hiyo kutambua uwezo wa Bw Owino.

“Nataka rafiki yangu Babu Owino awapungie mkono mahala alipo. Ndiyo… ndiye yule aliyeketi pale,” akaeleza huku waombolezaji wakishangilia.

Wadadisi sasa wanafananisha ‘ukaidi’ wa Winnie dhidi ya uongozi wa ODM na ule wa Raila dhidi ya uongozi wa Ford Kenya mnamo 1994 baada ya kifo cha babu yake, Jaramogi Oginga Odinga.

Kulingana na Martin Andati, Winnie, sawa na babake aliyepambana na marehemu Wamalwa Kijana nyakati hizo, anataka kutegemea uungwa mkono kutoka kwa umma katika kukabiliana na uongozi wa sasa wa ODM anapopania kuubeba mwenge wa kisiasa wa Raila.

“Winnie ni kivuli cha Raila kwani amerithi sifa zote za kisiasa za mwendazake na sasa anaonekana hata kumsukuma mjombake ambaye sasa ndiye kiongozi wa ODM. Ikumbukwe kuwa hivi ndivyo Raila alivyomtikisa marehemu Wamalwa Kijana aliyerithi uongozi wa ODM baada ya kifo cha Jaramogi,” akaeleza.

Wakati wa mazishi ya Beryl, Winnie pia alidhihirisha sifa nyingine ya Raila kuhusu historia ya familia yao.

Alitaja hatua kwa hatua asili ya kizazi chao kutokea kwa Wanga hadi kwa babu yake Jaramogi Oginga Odinga.

“Kuna watu wanaodhani kuwa sisi kama vijana hatujui historia na masuala mengine mengi. Ningependa kuwaambia kuwa tunajua mengi na ndio maana tunapigania nafasi yetu katika uongozi wakati huu,” akaeleza.