JAMVI: Mitego inayoweza kufanya Ruto yatima wa kisiasa
Na BENSON MATHEKA
NAIBU Rais William Ruto, anakabiliwa na hatari ya kuwa ‘yatima’ kisiasa asipodilisha mbinu zake, wadadisi wanasema.
Wanasema mwelekeo ambao siasa za Kenya zinachukua huenda ukamfanya kutengwa zaidi na kufifisha azima yake ya kugombea urais kwenye uchaguzi mkuu wa 2022.
Kulingana na mchanganuzi wa siasa, Profesa Makau Mutua, Dkt Ruto anaweza kujikwaa kwa sababu ya tabia yake ya kujipiga kifua badala ya kubadilisha mbinu zake za kisiasa.
“Anakimbia sana kuelekea Ikulu hata zaidi ya wanariadha maarufu kutoka jamii yake, amepuuza wengi na hawezi kuona mitego ya wazi iliyo mbele yake,” Profesa Mutua alisema.
Wadadisi wanasema kwa sababu ya kupuuza ushauri na kuwa na kiburi, amekosa kugundua ujanja na mitego ya kisiasa aliyowekewa na Rais Uhuru Kenyatta na wapinzani wake wa kisiasa.
“Inasemekana kuwa mnamo 2013, Uhuru Kenyatta alimuahidi Ruto kwamba atamuunga mkono awe mrithi wake kwenye uchaguzi mkuu wa 2022. Kwamba Kenyatta angetawala kwa miaka kumi na kisha ampishe Ruto atawale kwa miaka mingine kumi. Inawezekana kuwa hii ilikuwa sehemu ya kampeni ambapo wanasiasa huwa wanaahidi mambo makubwa yasiyoweza kutimizwa au lilikuwa tamko la kuchangamsha jamii ya Wakalenjin wakati huo,” anaeleza.
Hata hivyo, anasema kwamba Dkt Ruto ni mwanasiasa mwenye uzoefu mkubwa kuamini matamshi yanayotolewa wakati wa kampeni.
Kulingana na Profesa Mutua, kilicholeta Uhuru na Ruto pamoja ni masaibu waliyokuwa wakipitia 2013 kwa kushtakiwa katika Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu (ICC).
Anasema Ruto alichoamini ni kuwa kuungana kwao kulinuia kumaliza chuki kati ya jamii zao jambo ambalo lingemwezesha kushinda urais kwa urahisi.
“Hivi ndivyo alivyokuwa akiamini Dkt Ruto hadi Machi 2018 Uhuru aliposalimiana na kiongozi wa upinzani Raila Odinga. Mambo yamebadilika sasa na Ruto ameachwa kama yatima jangwani,” alisema.
Licha ya siasa kuchukua mwelekeo tofauti baada ya handisheki, Dkt Ruto aliendelea kuonyesha kiburi chake na kuwavuta wanasiasa kadhaa kutoka ngome ya Rais Kenyatta upande wake.
Wanasiasa hao ambao amekuwa akizunguka nao maeneo tofauti wanasisitiza kuwa Rais Kenyatta hana budi kutimiza ahadi yake ya kumuunga Dkt Ruto kwenye uchaguzi mkuu wa 2022.
“Kauli zao kwamba Uhuru ni lazima amuunge Dkt Ruto, zimemkwaza kiongozi wa nchi na akaamua kuwazima kwa kuwatenga na serikali yake alivyofanya alimpofuta kazi Waziri wa Kilimo Mwangi Kiunjuri,” anaeleza Profesa Mutua kwenye makala yake ya kila wiki katika gazeti la ‘Sunday Nation‘.
Anasema kuwa Dkt Ruto ana haki ya kugombea urais lakini akaonya wandani wake kwamba hawafai kulazimisha Wakenya wamchague.
“Katika demokrasia, hakuna aliye na haki ya kutawala. Dkt Ruto ana uhuru wa kuomba kura lakini anafaa kuelewa kuwa kiburi na vitisho huzua hofu ya udikteta. Hata kama Rais Kenyatta aliahidi kumuunga mkono, ukweli ni kwamba kura yake ni moja na ni Wakenya watakaoamua,” aeleza.