JAMVI: Mwamko mpya Pwani wabunge wakiazimia kuzindua chama kipya
Na SAMUEL BAYA
Baada ya kugundua kwamba huenda eneo la Pwani likabakia nyuma kimaendeleo, wanasiasa wa eneo hilo sasa wameamua kufufua upya kundi la wabunge wa Pwani maarufu kama Coast Parliamentary Group (CPG).
Hatua hiyo sasa inatarajiwa kuwa mwanzo mpya ambao hatimaye utafanya eneo hilo kuongea kwa sauti moja baada ya mgawanyiko ambao ulitokea kufuatia mwafaka wa ushirikiano kati ya Rais Uhuru Kenyatta na kiongozi wa upinzani Bw Raila Odinga mwaka jana.
Akitihitibisha mchakato huo, mbunge wa Kinango Bw Benjamin Tayari alisema kuwa jukumu la kuimarisha tena CPG limepatiwa Seneta wa Kilifi Bw Stwart Madzayo na mwenzake wa Mombasa Bw Mohamed Faki kutayarisha mkataba wa maelewano kati ya viongozi wote wa Pwani.
“Tuliketi chini na baada ya kuona kwamba Pwani inayumba kimaendeleo kutokana na siasa, tuliamua kufufua tena umoja wetu kupitia kwa kundi la CPG. Tayari jukumu hilo la kutuleta pamoja litaongozwa na Maseneta hao wawili kwa sababu wao ni mawakili na wenye uzoefu,” akasema Bw Tayari.
Siku chache tu baada ya Rais Kenyatta na Bw Odinga kuamua kuzika tofauti zao na kushirikiana, mgawanyiko ulizuka kati ya viongozi wa Pwani. Mgawanyiko huyo ulianza kujitokeza baada ya ziara za naibu wa Rasi katika eneo la Pwani ambapo alianza kujizolea umaarufu na kupata uungwaji mkono kutoka kwa baadhi ya wabunge wa Pwani.
Jambo hilo likapelekea kuchipuka kwa makundi mawili moja likiunga mkono Bw Ruto na lingine likiunga mkono Bw Odinga. Makundi hayo mawili yalianza kusutana na kuanza kuibua migawanyiko ambayo Bw Tayari alikiri kwenye mahojiano na Jamvi la Siasa kwamba iliathiri azimio la viongozi hao kuongea kwa sauti moja.
“Kile ambacho wakazi wa Pwani wamezoea kujionea kwa sasa ni kupigana kumbo kwa viongozi wao. Kwa mfano Bw Raila akifika hapa, wale viongozi washirika wake wataongea wakilaumu wale wanaounga mkono Naibu Rais. Vivyo hivyo naibu wa Rais akifika huku Pwani, wanaomuunga mkono wataanza kurushiana vijembe na kudharau wale wengine. Kwa namna hii, ni vigumu kuungana,” akasema Bw Tayari.
Hata hivyo, alisema kuwa azimio hili jipya sasa linatarajiwa kupalilia pondo umoja wao kama viongozi.
“Baada ya kukubali kwamba tumegawanyika, sasa ni kusonga mbele kwa sababu ajenda tuko nayo isipokuwa ilikuwa ikiyumbishwa na siasa,” akasema Bw Tayari.
“Tuko na fursa sasa ya kuamsha muungano wetu kisha ikiwezekana lengo kamili liwe la kuanzisha chama chetu ambacho tutatumia kuwania Urais.’’
Wabunge wanaomuunga mkono naibu wa Rais Bw William Ruto ni pamoja na mbunge wa Kaloleni Bw Paul Katana, Owen Baya (Kilifi Kaskazini), Aisha Jumwa (Malindi), Kassim Tandaza (Kinango), Ali Mbogo (Kisauni), Mohamed Ali (Nyali) miongoni mwa wabunge wengine wa Pwani.
Mbunge wa Msambweni Bw Suleiman Dori ambaye ndiye mwenyekiti wa CPG alikuwa akiunga mkono ajenda ya Naibu Rais lakini baadaye akageuza nia. Jambo hilo lilipelekea yeye kusamehewa na chama cha ODM lakini mbunge mwenzake wa Malindi Bi Jumwa akiendelea kupambana na mpango wa chama hicho kutaka kumtoa kwa madai ya kumuunga mkono Bw Ruto.
Kundi linalomunga mkono Bw Raila na Gavana Joho ni pamoja na Teddy Mwambire (Ganze), Ken Chonga (Kilifi Kusini), Mishi Mboko (Likoni), Omar Mwinyi (Changamwe) miongoni mwa wabuge wengine.
Kwenye mahojiano na Jamvi la Siasa, Bw Katana alikiri kwamba ukosefu wa umoja miongoni mwao umewaathiri.
“Kama viongozi wa siasa, tumejikita zaidi katika masuala ya vyama na kujisahau. Tunachukua muda mchache sana kuangalia hatima yetu. Kwangu mpango wa kuongea kwa umoja kama kundi la Pwani ni mzuri na ndio suluhu pekee,” akasema Bw Katana.
Mbunge huyo wa Kaloleni alisema kuwa bila wao kuungana, basi kupata keki ya maendeleo itakuwa vigumu sana.
“Kama tunataka eneo hili la Pwani lipate hadhi na heshima basi ni lazima tuanze sisi wenyewe kuheshimiana na tutaanza kwa kuungansiha kundi la CPG ambalo ni kweli lilikuwa limegawanyika sana,” akasema Bw Katana.
“Ni hatari kwa kundi la CPG kukumbwa na mgawanyiko kwa sababu ya siasa za vyama wakati ambapo linahitajika kutuweka pamoja kwa minajili ya maendeleo,” akasema Bw Katana.
Kulingana na mbunge wa Jomvu Bw Badi Twalib, bila kuwa na muungano wa viongozi thabiti, itakuwa vigumu kuhimiza umoja wa maendeleo.
“Mimi ninaunga mkono wazo la kufufua umoja wetu kama wabunge kwa sababu tumegawanyika sana na hili ni tishio kubwa la kimaendeleo,” akasema Bw Twalib.
Akiongea na jarida hili, mbunge wa Magarini Bw Michael Kingi alisema kuwa Pwani inafaa kuwa na chama chake cha kisiasa mbali na kuwa na muungano kama wabunge.
“Tumeshuhudia maendeleo haba kwa sababu tangu uhuru, bado hatujaweza kuongea kwa sauti moja kama viongozi wa Pwani. Jambo la umoja kamwe sio la kutiliwa mzaha na linahitaji ushirikiano mkubwa kwa sasa,” akasema Bw Kingi.
Aidha mbunge huyo alisema kuwa licha ya gavana wa Mombasa Bw Hassan Joho na mwenzake wa Kilifi Bw Amason Kingi kuwa mibabe wa siasa Pwani, wawili hao wameanza kuvuta katika njia tofuati.
“Ukiangalia wazo la Gavana Kingi kwanza ni kuwaunganisha viongozi wote wa Pwani kuwa kitu kimoja kabla ya kuanza mchakato wa kumtoa Rais wa kutoka Pwani.
Lakini kwa upande mwengine tayari Gavana Joho amesema atawania Urais mwaka wa 2022, azimio ambalo linaonekana kuwapata wakazi kwa mshangao. Je, huu si mgawanyiko,” akasema Bw Kingi.
Hata hivyo alikiri kwamba umoja wa Pwani utafanikiwa wakati ambapo kutatokea mmoja wa vigogo hao wawili kuwa kichwa cha Pwani.
“Ukiangalia viongozi kama akina Kalonzo Musyoka, Raila Odinga na Musalia Mudavadi, wao bado hawajakuwa Marais lakini wana ushawishi mkubwa sana kwa sababu ni viongozi wa kitaifa. Hilo ndilo ambalo tunataka kufanya kuhusu viongozi wetu,” akasema Bw Kingi.
Mbunge wa Kilifi Kaskazini ambaye alikuwa mshiriki mkubwa wa Bw Raila kabla ya kumuacha na kuingia upande wa Ruto, alisema kuwa umoja wa viongozi wa Pwani ni muhimu. Hata hivyo, alisema kuwa ili kupata maendeleo ni lazima viongozi wawe ndani ya serikali.
Mbunge wa Ganze Bw Teddy Mwambire alisema kuwa viongozi wa Pwani lazima wajilaumu kwa kukosa kuwa na sauti moja.
Alisema kuwa kuwa kuongea kwa sauti tofauti tofauti ni kero kubwa ambalo litazidi kuacha eneo hili likiyumba bila msaada wowote.
“Katika uchaguzi uliopita, tulipigia kura upinzani kisha baada ya kura baadhi ya wabunge wakakimbilia upande wa serikali na malumbano yakaanza. Tunaposema kwamba tunaungana kama viongozi, lazima sauti zetu ziwe na uwazi,” akasema Bw Mwambire.