JAMVI: Wimbo wa #WajingaNyinyi utachochea Wakenya kuleta mabadiliko ya kisiasa?
Na WANDERI KAMAU
HATUA ya mwanamuziki Kennedy Ombina maarufu kama King Kaka kutoa wimbo ‘Wajinga Nyinyi’ imeongeza midahalo ambayo imekuwepo kwa muda mrefu kuhusu ikiwa nyimbo zinaweza kushinikiza mageuzi ya kisiasa nchini.
Wimbo huo ambao ulitolewa Jumamosi iliyopita uliiteka nchi nzima na kuzua hisia mseto miongoni mwa wadau mbalimbali, ila swali kuu ni ikiwa utachangia lolote katika ulingo wa kisiasa nchini.
Kufikia sasa, wimbo huo umetazamwa na watu zaidi ya milioni mbili katika mtandao wa YouTube, hali inayoashiria umaarufu wake mkubwa.
Hata hivyo, swali lililopo miongoni mwa wachanganuzi wa masuala ya kitamaduni ni ikiwa Wakenya watakumbatia wimbo huo kimatendo, ikizingatiwa si wa kwanza kuwa na ujumbe kama huo.
Baadhi ya nyimbo za awali ambazo zilizua msisimko wa kisiasa nchini ni Nchi ya Kitu Kidogo wake Eric Wainaina, Wanasiasa wa kundi la Kitu Sewer, Siasa Duni wa mwanamuziki Susumila, Tujiangalie wa kundi la Sauti Sol na Nyashinski, Utawala wa Juliani kati ya zingine.
Wanasiasa kadhaa wamejipata lawamani kwa kutajwa kuhusika katika sakata za ufisadi, baadhi yao wakiwemo magavana Anne Waiguru (Kirinyaga), Ferdinard Waititu (Kiambu) na Mike Sonko (Nairobi).
Kulingana na Dkt Joyce Nyairo, ambaye ni mchanganuzi wa siasa na masuala ya kitamaduni, msisimko ulioletwa na wimbo huo unapaswa kuwazindua wanamuziki nchini kujiepusha kukita nyimbo zao katika uenezaji wa chuki za kikabila.
Dkt Nyairo anasema kuwa wanasiasa huwa wanawatumia wanamuziki katika nyakati za uchaguzi, kwani muziki una nguvu sana ikilinganishwa na aina zingine za sanaa.
“Ujumbe ulio katika muziki huwa rahisi kuwafikia watu wengi kwa urahisi kwani miziki hiyo inachezwa katika majukwaa mbalimbali yanayowafikia watu wengi,” asema.
Wadadisi wanasema kuwa hatua ya Bi Waiguru kutoa tishio za kumfungulia mashtaka King Kaka ilitokana na umaarufu mkubwa ambao wimbo huo umepata.
Gavana huyo alikuwa ametishia kumshtaki mwanamuziki kwa madai ya “kumharibia sifa.”
Wanaeleza kuwa Bi Waiguru alihofia kwamba huenda akajipata mateka wa vitisho vyake mwenyewe.
Prof Evans Mwangi ambaye ni mhadhiri wa Fasihi na Utamaduni katika Chuo Kikuu cha Northwestern, nchini Amerika, asema kuwa kutokana na uwepo wa mitandao ya kijamii, ni rahisi sana kwa jumbe zilizo katika muziki kuwafikia watu wengi, hata ikiwa nyimbo hizo hazitachezwa katika vyombo vya habari.
“Kinyume na enzi ya utawala wa Rais Mstaafu Daniel Moi, ambapo wimbo ‘Nchi ya Kitu Kidogo’ ulipigwa marufuku na mwanamuziki Eric Wainaina kukamatwa, hali ni tofauti sana wakati huu kwani kila mtu anaweza kuupata wimbo huo kwa njia ya simu,” asema.
Kulingana na wachanganuzi, umaarufu wa muziki katika siasa ndiyo uliyofanya nyimbo kama “NASA Tibim” na “Tano Tena” kutumika na muungano wa NASA na Chama cha Jubilee (JP) kwenye uchaguzi mkuu wa 2017.
Wimbo wa “NASA Tibim” ulitungwa na mwanamuziki Onyi Jalamo, huku kibao “Tano Tena” kikitungwa na msanii Ben Githae kutoka eneo la Kati.
Wimbo wa NASA unakisiwa kumsaidia sana mwaniaji urais wa NASA Bw Raila Odinga kujizolea umaarufu miongoni mwa wapigakura, hasa katika maeneo ya Nyanza na Magharibi.
Nao wimbo wa “Tano Tena” unakisiwa kumsaidia sana Rais Uhuru Kenyatta kujizolea umaarufu mkubwa wa kisiasa, hasa miongoni mwa jamii za Wakikuyu, Ameru na Aembu.
Licha ya hatua hizo, wachanganuzi wanakosoa mtindo wa baadhi ya wanamuziki kutoka maeneo ya Mlima Kenya na Nyanza kutunga nyimbo za kueneza ukabila na chuki za kisiasa.
Katika eneo la Mlima Kenya, baadhi ya wanamuziki wamefunguliwa mashtaka kwa madai ya kutunga nyimbo za kueneza chuki za kikabila.
Baadhi ya wanamuziki ambao wamejipata lawamani ni marehemu John De Mathew, Kamande wa Kioi, Muigai wa Njoroge kati ya wengine.
Watatu hao walifunguliwa mashtaka ya uchochezi mnamo 2012 kwa utunzi wa nyimbo ‘Wituite Hiti’ (Umejifanya Fisi), ‘Uhuru ni Wiitu’ (Uhuru ni Wetu) na ‘Hague-Bound.’
Na ingawa mashtaka hayo yalifutiliwa mbali, hali hiyo imeendelea kudhihirika katika eneo hilo, ambapo sasa wanamuziki wanatunga nyimbo za kuwasifu ama kuwakashifu Rais Kenyatta, Bw Odinga na Naibu Rais William Ruto.
Baadhi ya wanamuziki wanatunga nyimbo za kumsifu Dkt Ruto, wakisisitiza kuwa jamii za eneo hilo “zitalipa deni la kisiasa” kwa kumpigia kura mnamo 2022.
Wengine wanatunga nyimbo za kusifu handisheki kati ya Rais Kenyatta na Bw Odinga.
Miongoni mwa wanamuziki waliotunga nyimbo za kumsifu Dkt Ruto ni Kimani wa Turaco, Peter Kigia “wa Esther”, Bw Kioi, De Mathew huku kundi lingine likisifu handisheki.
Kwenye mahojiano, mwanamuziki Wainaina anasema kuwa ilipofikia, “wao wametekeleza majukumu yao” na ni upande wa Wakenya sasa kuchukua hatua kuzingatia jumbe zilizo katika nyimbo hizo.