Je, Kasmuel na Morara kuingia vyama vya kisiasa ni utetezi halali wa Gen Z au ulafi wa mamlaka?
KUNA hofu kwamba moto uliowashwa na vuguvugu la vijana wa kizazi cha Gen Z wa kuendeleza vita vya kutetea utawala bora nchini unahujumiwa na baadhi yao wanaojitafutia makuu.
Wamefanya hivyo kwa kuunda au kujiunga na vyama vya kisiasa vilivyoko sasa kinyume na msimamo wao wa awali wa kutojiegemeza na vyama vya kisiasa au makabila fulani.
Mnamo Septemba 16 mwaka huu mwanaharakati, Morara Kebaso alitangaza kuwa ameunda chama cha kisiasa kwa jina INJECT Political Party of Kenya (IPPK).
Na mnamo Oktoba 2, msajili wa vyama vya kisiasa Anne Nderitu alikijisajili rasmi chama hicho na kukiweka kwenye orodha ya vyama halali vya kisiasa nchini.
Na mnamo Jumapili Novemba 10, 2024 mwanaharakati mwingine wa Gen Z, Kasmuel McOure alitangaza kuwa amejiunga rasmi na chama cha Orange Democratic Movement (ODM) kilichoasisiwa mwaka wa 2005 na Raila Odinga.
Aliwarai vijana kujiunga na chama hicho cha Chungwa, akieleza kuwa ndicho chama kinachoweka mbele masilahi ya Wakenya na kupigania uwepo wa mazingira ya utawala ambamo watu wote wataheshimiwa.
“Ikiwa unalenga kujiunga na chama kinachosimamia haki na demokrasia na kinachothamini hadhi ya kila mtu basi chama hicho ni ODM- chama kikubwa katika Afrika Mashariki na Kati,” McOure akasema kupitia akaunti yake ya mtandao wa X (zamani Twitter).
Mwanaharakati huyo alisema hayo baada ya kukutana na mwenyekiti wa ODM Gladys Wanga mjini Homa Bay wakati wa sherehe ya kutoa shukrani tangu aliporithi kiti hicho kutoka kwa John Mbadi aliyejiondoa Julai mwaka huu. Hii ni baada ya kuteuliwa kwake kuwa Waziri wa Fedha katika serikali ya Rais William Ruto.
Baada ya kusajiliwa rasmi kwa chama chake Morara, 29, alielezea matumaini kuwa ataleta mageuzi katika uwanja wa siasa nchini aliodai umezongwa na ufisadi.
“Chama cha INJECT kitafagia, kama mafuriko, viti vya ubunge na vingine vyote cha kuchaguliwa. Watu wa Kenya, nyote mwaalikwa katika afisi yenu iliyoko mtaa wa Kahawa Sukari, Barabara ya Kiu River, 6th South Avenue. Pamoja Tujenge Chama,” akaandika katika akaunti yake ya mtandao wa X, saa chache baada ya Bi Nderitu kusajili rasmi chama chake.
Kebaso alipata umaarufu kutokana na kampeni zake za kuikosoa serikali kwa kunakili video zinazoonyesha miradi ya serikali iliyokwama sehemu mbalimbali nchini licha ya kutengewa mabilioni ya fedha na hata wanakandarasi kulipwa.
Hatua za Morara na Kasmuel kujihusisha na vyama vya kisiasa imepokea hisia mseto huku baadhi ya wadadisi wakiwataja kama wasaliti wa harakati za Gen Z kupigania mageuzi ya uongozi nchini.
Kulingana na Dkt David Okello, wawili hao wameonyesha wazi kuwa haja yao kuu ilikuwa ni kutumia wimbi la maasi ya Gen Z kupata jukwaa la kuendeleza masilahi yao.
“Kwa kuunda chama chake, Morara anaonyesha kuwa msukumo wa uanaharakati wake ni wa kuendeleza masilahi yake sio ya vijana wenzake. Hii ndio falsafa inayomwongoza McOure anapojinga na chama ambacho kinashirikiana na serikali ambayo imetumia vyombo vya dola kuwatesa na hata kusababisha vifo vya wengi wao,” anasema mchanganuzi huyo ambaye ni mhadhiri katika Chuo Kikuu cha Kenyatta.
Chama cha ODM kimesawiriwa kama msaliti kwa vijana wa Gen Z, kwa kuutumia uasi wao kujipenyeza ndani ya serikali ya Kenya.
Hatua hiyo ilichangia viongozi watano wa chama hicho kuteuliwa katika baraza la mawaziri kwa kile ambacho Bw Odinga na Rais Ruto walitaja kama “hatua ya kurejesha amani na utulivu nchini.”
Lakini Jumapili McOure alitetea uamuzi wake wa kujinga na ODM akisema utawezesha yeye na vijana wenzake kupata nafasi na jukwaa bora la kushawishi mkondo wa utawala nchini Kenya.
“Uamuzi wangu haufai kuchukuliwa kama usaliti. Kenya ni taifa linaloongozwa kupitia vyama vya kisiasa. Hivi ndivyo vyombo vinavyotumika kuendelea uongozi wa kidemokrasia nchini. Kwa hivyo, itakuwa vigumu kwetu kushiriki na hata kuwa na ushawishi au usemi kuhusu namna taifa hili linavyoongozwa ikiwa tutasalia nje ya vyama vya kisiasa,” akaeleza.
Ushindi wa kwanza wa umoja wa vijana wa Gen Z ulidhihirika mnamo Juni mwaka huu walipofaulu kushinikiza serikali ya Rais Ruto kuondoa Mswada wa Fedha 2024 uliosheheni mapendekezo ya kutoza ushuru bidhaa na huduma za kimsingi.
Walifanya hivyo, kupitia msururu wa maandamano ya amani jijini Nairobi na miji mingine nchini. Lakini maandamano hayo yaliingiwa na wahuni waliovamia majengo ya bunge mnamo Juni 25, 2024 na kuharibu mali ya thamani ya mamilioni ya fedha.
Hatimaye Rais Ruto alikataa kutia saini mswada huo na kuwaagiza wabunge wauzime kabisa.
Hata hivyo, alichukuwa hatua hiyo baada ya zaidi ya vijana 50 kuuawa katika makabiliano kati ya wandamanaji na polisi huku wengine wengi wakitejwa nyara.
Juzi, Inspekta Jenerali wa Polisi Douglas Kanja aliwaambia wabunge kwamba vijana 29 bado hawajulikani waliko tangu maandamano ya Gen Z kuanza mnamo Juni 18 mwaka huu.
Lakini licha ya vijana hao aliapata kuendeleza kutetea utawala bora kwa kupinga sera na sheria zinazowakandamiza raia.