Je, unafahamu afya ya udongo wa shamba lako?
MAENEO yanayozalisha mahindi nchini kwa sasa yanakabiliwa na tatizo kubwa; kiwango cha juu cha asidi kwenye udongo.
Iwapo halitashughulikiwa, tatizo hili linaweza kulemaza juhudi za kuafikia ajenda ya kuangazia usalama wa chakula na njaa.
Kulingana na Shirika la Utafiti wa Kilimo na Mifugo Kenya, ndilo KALRO, taasisi ya kiserikali, karibu asilimia 65 ya udongo nchini ni wa asidi, hali inayotishia uzalishaji wa chakula.
Kaunti kama Trans Nzoia, Uasin Gishu, Bungoma, Narok, Nakuru, Kakamega, na Nandi zinajulikana kwa uzalishaji wa mahindi nchini.
Hata hivyo, udongo katika maeneo hayo unazidi kuwa na asidi.
“Udongo unaweza kuwa na virutubisho vinavyohitajika, lakini unaathirika kutokana na asidi,” anasema Dkt David Kamau, Mkurugenzi wa Mifumo ya Mazingira na Raslimali Asili KALRO.
Udongo wa Kenya hauko katika hali bora, suala linalopaswa kutathminiwa.
Tatizo la kudhoofika kwa udongo limeenea sana maeneo yanayozalisha mahindi hadi maeneo kame (ASAL), ambayo yanajumuisha zaidi ya asilimia 80 ya ardhi ya Kenya.
Kenya ina kaunti 23 za ASAL, na udongo katika maeneo hayo umeharibika kutokana na kiwango cha juu cha mifugo.
“Maeneo kame, udongo umedhoofika zaidi kwa sababu ya uwekaji mifugo kupindukia, na vilevile ukame,” Dkt Kamau anaeleza.
Mwaka 2022, Kenya ilikumbwa na ukame uliojatwa kuwa mbaya zaidi katika historia yake, na kusababisha upotevu wa mazao na mifugo yenye thamani ya mabilioni ya pesa.
Mengine yanayochangia kuharibika kwa udongo ni pamoja na mabadiliko ya tabianchi, mvua ya mafuriko inayosababisha mmomonyoko wa udongo, na matumizi kupita kiasi ya mbolea zenye kemikali.
“Wakulima wanategemea sana mbolea zisizo za kiasili, na tunapendekeza wazishirikishe na za kiasili,” Dkt Kamau anashauri.
Ili kuangazia matatizo haya, Dkt Kamau anahimiza wakulima kukumbatia teknolojia na bunifu za kilimo endelevu ili kurejesha afya ya udongo.
Mbinu kama vile kutumia matandazo (mulching), kulima kwa kiwango kidogo (minimum tillage), na kukuza kwa pamoja mimea ya familia tofauti ni muhimu kuboresha afya ya udongo na kuhakikisha usalama wa chakula, hasa kipindi hiki taifa na ulimwengu kwa jumla unaendelea kukeketwa na makali ya tabianchi.
Pia, Dkt Kamau anahimiza wakulima kupima udongo wao mara kwa mara, ili kufahamu hali yake.
Hata hivyo, kurejesha na kufufua udongo si kazi rahisi. Ni oparesheni inayochukua muda.
Dkt Kamau anasisitiza kuwa ni mchakato wa muda mrefu unaohitaji raslimali nyingi.
“Urejeshaji afya ya udongo huchukua muda. Mbali na kushirikisha teknolojia za kilimo endelevu, tunahimiza wakulima kuongeza laimu kwenye udongo wao,” anaelezea.
Wakulima wanashauriwa kutumia tani mbili za laimu kwa hekta moja, kila baada ya miaka miwili.
Kiwango bora cha asidi au alikali, ndio pH, kwenye udongo kinapaswa kuwa kati ya 6.5 na 7.5.
Udongo wenye pH zaidi ya 7.5 ni wa alikali, huku wenye pH chini ya 6.5 ni asidi.
Aidha, udongo wenye pH chini ya 5.5 unachukuliwa kuwa wenye asidi nyingi.
Ikizingatiwa kuwa wakulima wengi wanakosa mbolea ya bei nafuu, serikali mwaka 2023 ilianzisha mpango wa mbolea ya ruzuku ili kuwapiga jeki kuendeleza zaraa.
“Mpango wa mbolea ya bei nafuu umesaidia wakulima pakubwa, na tumeshuhudia ongezeko la mazao kama vile mahindi,” asema Dkt Kamau.
Licha ya Afrika kuwa na asilimia 65 ya ardhi inayofaa kuendelezwa shughuli za kilimo na asilimia 10 ya vyanzo vya maji safi, bara hili bado linategemea kwa kiasi kikubwa uagizaji wa chakula kutoka nje.
Dkt Kamau anadokeza kwamba udongo wenye afya bora, mavuno ya mahindi yanaweza kufikia hadi magunia 45 kila ekari kwa msimu, na wastani wa magunia 30.
Hata hivyo, wakulima wengi kwa sasa huzalisha wastani wa magunia 10 tu kwa ekari kwa sababu ya kuharibika kwa udongo.
Dkt Kamau anaonya kuwa matumizi ya mbolea zenye Nitrojeni huchangia sana kuongezeka kwa asidi kwenye udongo.
Afya ya udongo ni muhimu kwa uzalishaji wa chakula na mafanikio ya kilimo kwa ujumla.