Makala

Jepkosgei Chemwoia kutoka Baringo aibuka mwalimu bora Afrika

Na FRANCIS MUREITHI September 12th, 2025 Kusoma ni dakika: 2

MWALIMU Mkenya ndiye mshindi wa Tuzo ya Umoja wa Mataifa kuhusu Mwalimu Bora Barani.

Bi Jepkosgei Chemwoia, 40, ambaye ni mwalimu wa Hisabati na Fizikia katika Shule ya Upili ya Emining Boys, Kaunti ya Baringo, hakuamini jina lake lilipotajwa kuwa mmoja kati ya walimu bora zaidi barani Afrika.

Alikuwa amehudhuria kongamano katika Chuo Kikuu cha Egerton, Bewa la Njoro, alikosomea, bila kufahamu kwamba maisha yake yangechukua mkondo mpya.

“Nilimvuta nje afisa wa TSC aliyekuwemo kwenye ukumbi huo kuthibitisha ikiwa nilichokuwa nasoma ni kweli,” alisimulia.

“Nilikuwa katika hali ya kutoamini. Kupokea habari hizo nikiwa Egerton ilikuwa baraka kubwa. Nitaishi kukumbuka maisha yangu yote.”

Bi Jepkosgei amejinyakulia nafasi miongoni mwa walimu bora zaidi barani. Tuzo ya Umoja wa Mataifa kuhusu Mwalimu Bora Barani ilianzishwa 2019 kuinua taaluma ya ualimu, kuwasherehekea walimu bora na kupigia debe ualimu kama taaluma inayovutia zaidi kote Afrika.

Tuzo hii iinahusiana kwa karibu na Ajenda ya AU 2063 na Mikakati ya Elimu kwa Afrika Barani (CESA), inayoashiria taswira ya Afrika inayoendeshwa na maarifa, ujuzi na ubunifu.

Washindi huteuliwa kwa makini kuhusu weledi wao kwenye somo husika, kujitolea kuwashirikisha wanafunzi, kanuni za kinidhamu, kuhusika katika shughuli za kijamii, na hususan mchango wao katika kuunda mustakabali wa wanafunzi wachanga.

Bi Jepkosgei alisema hakuwahi kufikiria kwamba kazi yake mashinani ingeweza siku moja kutambulika kwenye jukwaa la kimataifa.

“Nakumbuka nilipowaona washindi waliotangulia na kushangaa ni vipi walikwea jukwaa la ushindi. Nikifunza shule ya kijijini, kamwe sikufikiria kuna mtu mahali ananitazama kwa umbali na kutambua ninachopenda kufanya kwa fahari kubwa.”

Safari ya kuelekea jukwaa la kimaeneo haikuwa rahisi.

Bi Jepkosgei aliteuliwa na Tume ya Kuajiri Walimu (TSC) baada ya mchakato wenye ushindani mkali uliohusisha walimu zaidi ya 370,000 kutoka kote nchini.

Ni walimu wawili pekee waliofanikiwa kufika fainali za kimaeneo, kuashiria uteuzi makinifu unaohakikisha ni walio bora pekee wanaowakilisha taifa.

Safari yake kama mwalimu inasawiri mshawasha, kujitolea mhanga na ukakamavu.

Janga la COVID-19 lilipotatiza elimu 2020, alifanya hima kufundisha kimtandao.

Pasipo mafunzo yoyote hapo mbeleni kuhusu elimu kimtandao, aliweza kuwafikia wanafunzi zaidi ya 10,000, wengi wao watahiniwa waliokuwa wakijitayarisha kwa mitihani muhimu ya KCSE.