Jimmy ‘Barbecue’ Cherizier: Polisi wa zamani anayeongoza magenge ya uhalifu nchini Haiti
WANDERI KAMAU Na MASHIRIKA
JE, ni nini kiini cha makabiliano makali ambayo yamekuwa yakiendelea nchini Haiti baina ya vikosi vya serikali na magenge ya uhalifu?
Ni nani kiongozi wa makundi hayo?
Hayo ni baadhi ya maswali ambayo yamekuwa yakiibuka, hasa Kenya na mataifa mengine kadhaa yanapojitayarisha kutuma kikosi maalum cha polisi kuisaidia serikali ya Haiti kukabiliana na magenge hayo.
Taifa Jumapili imeelekeza darubini yake nchini Haiti, na kumwangazia kiongozi mkuu wa magenge hayo hatari—Jimmy ‘Barbeque’ Cherizier.
Cherizier aliwashangaza wengi majuzi alipomwambia Waziri Mkuu Ariel Henry kutorudi katika taifa hilo, baada ya kuondoka wiki iliyopita kuzuru mataifa kadhaa, ikiwemo Kenya.
Cherizier, 46, ni afisa wa zamani wa polisi, na ni kiongozi wa makundi kadhaa ya uhalifu.
Alipohudumu kama polisi, inadaiwa aliongoza kwenye msururu wa visa vya mauaji ya kikatili, kikiwemo kisa ambapo zaidi ya watu 70 waliuawa katika eneo la La Saline, jijini Port-au-Prince mnamo 2018.
Kwenye kisa hicho, zaidi ya makazi 400 yalichomwa, kulingana na maelezo yaliyotolewa na Umoja wa Mataifa (UN).
Cherizier ni miongoni mwa viongozi watano wa magenge ya uhalifu ambaye amewekewa vikwazo na UN na Amerika.
Anatoka katika eneo la Delmas, jijini Port-au-Prince.
Mnamo 2020, alileta pamoja magenge tisa katika jiji hilo na kubuni muungano unaoitwa G9 Family and Alliances, anaoongoza hadi leo.
Kundi hilo liligonga vichwa vya habari duniani, baada ya kuchukua udhibiti wa kituo kikuu cha mafuta nchini humo, kufuatia mauaji ya Rais Jovenel Moise mnamo 2021.
Hatua ya kundi hilo ilisimamisha shughuli muhimu katika taifa hilo ndogo lililo katika eneo la Carribean.
Hali hiyo ilivuruga pakubwa sekta ya uchukuzi na utoaji matibabu katika hospitali muhimu. Kundi liliondoka kwenye kituo hicho baada ya mwezi mmoja.
Henry alichukua uongozi baada ya mauaji ya Rais Moise, na alifaa kung’atuka mamlakani mnamo Februari. Hata hivyo, maandamano makali yalizuka mwezi Februari, huku waandamanaji wakimtaka kuondoka uongozini.
“Ikiwa Ariel Henry hatajiuzulu na ikiwa ataendelea kusaidiwa na jamii ya kimataifa, kutazuka vita vikali katika taifa hili. Hakutakuwa na njia nyingine,” akasema Cherizier.
Ameapa ‘kuwakomboa’ raia wa Haiti kutoka kwa “masaibu ambayo wamekuwa wakipitia chini ya uongozi wa Henry”.