Makala

Jinsi Aga Khan alianzisha gazeti la ‘Taifa Leo’

Na WANGETHI MWANGI February 6th, 2025 Kusoma ni dakika: 2

NI vigumu kuamini kwamba kampuni kubwa ya habari tunayoifahamu sasa kama Nation Media Group Plc ilianza kama gazeti dogo tu la Kiswahili liitwalo Taifa Leo.

Muadhamu the Aga Khan ambaye aliaga dunia Jumanne, Februari 4, 2025 akiwa na umri wa miaka 88 alikuwa amechukua mapumziko kutoka kwa masomo yake nchini Amerika mwaka wa 1957 akatembelea Afrika Mashariki huku akijiandaa kuchukua hatamu kama kiongozi wa kiroho wa Waislamu wa Ismaili kufuatia kifo cha babu yake.

Alikuwa tu na umri wa miaka 20 lakini alihisi wimbi la mageuzi ambalo lingebadilisha kila kitu katika siasa za bara Afrika.

Kama Gerry Loughran anavyoandika kwenye kitabu chake, The Birth of a Nation: The story of a newspaper in Kenya, Muadhamu “tayari alikuwa anatazama mbali na kuwazia mustakabali wa Afrika Mashariki. Uhuru, kama alivyoamini, ulikuwa lazima utimie.”

Gerry, ambaye alikuwa mhariri mwanzilishi katika Nation, anasema pia kwamba wakati wa ziara yake hiyo Afrika Mashariki, Aga Khan alitilia maanani usemi wa mshauri wake wa habari, Michael Curtis, kuhusu “ubora duni wa magazeti Kenya na Uganda ambayo kimsingi yalikuwa sauti ya mkoloni”. Jambo hilo lilipanda mbegu akilini mwake ambayo ilimea upesi mno.

Pindi baada ya kukamilisha masomo yake, alitangaza nia yake ya kuanzisha gazeti na muda mfupi baadaye, akanunua ‘kagazeti kadogo’ ka Kiswahili kutoka aliyekuwa Kamisha wa Wilaya Charles Hayes na mshirika wake wa kibiashara Athea Tebbut, mwaka wa 1959. Mara moja akabadilisha gazeti hilo kuwa la kila siku, huku Sunday Nation akiianzisha Machi 1960, halafu sasa Daily Nation ikazaliwa Oktoba mwaka huo huo.

Sauti mpya ya Wakenya ikapatikana. Muadhamu alionekana kuwa aliyekuwa anaongozwa na haja ya kuanzisha jukwaa ambalo lingezungumzia matamanio ya wasio na sauti, ambao walikuwa Waafrika wengi. Taifa, ikiwa chini ya kampuni ya East African Newspapers (EA), Msururu wa Nation, ikafika sokoni Aprili 28, 1959. Toleo lake la kwanza liliuza nakala 15,000. Mwenzake wa kila siku, Habari za Leo Taifa, lilizinduliwa Januari 15, 1960, na kuwa gazeti la kwanza la kila siku Afrika Mashariki.

Ukuaji wa gazeti hilo ulionyesha pengo ambalo lilikuwa linasubiri kujazwa. Rekodi zinaonyesha kwamba toleo la kwanza liliuza nakala 14,000, kisha nakala 10,000 siku iliyofuata. Kufikia Desemba mwaka huo, mauzo yalikuwa yamefika nakala 37,000 na gazeti hilo liliendelea na ukuaji hadi kugonga nakala 60,000.

Katika kitabu, Birth of a Nation, Gerry Loughran anaelezea kwamba Aga Khan alianzisha Taifas kama mkakati kabambe wa kujibu haja ya kuwepo kwa chumba cha habari kilichotilia maanani matamanio ya Mkenya wa kawaida.

Muadhamu alitambua kwamba Kiswahili hakikuwa tu kinazungumzwa sana Kenya, bali pia kilikuwa miongoni mwa sehemu muhimu ya utambulisho wa kijamii. Aliamini kwamba chapisho lililoandikwa vizuri kwa Kiswahili lingependwa na umma na kusaidia kupatikana kwa urahisi kwa habari.

Tamanio lake kubwa lilikuwa kuwezesha hadhira ya Afrika kwa kutoa habari katika lugha ambayo walihisi nyumbani hivyo basi kusaidia kuunda umma ulio na uwezo wa kushiriki michakato ya kidemokrasia wakati ambapo kulikuwa na mavuguvugu ya kudai uhuru kutoka kwa Mkoloni.

Miaka ya baadaye na mabadiliko mengi, bado yalithibitisha kwamba Muadhamu alikuwa na maono katika uanahabari Afrika. Aliona uanahabari kuwa kifanikishi cha kijamii na kiuchumi kote barani na kwamba uanahabari mzuri unaweza kusaidia kutatua changamoto za kijamii na kuendeleza ukuaji.

“Ambia walioko mamlakani ukweli,” alipenda sana kutukumbusha, “lakini usikosoe tu bila sababu,” alisema huku akitetea uhuru wetu wa vyombo vya habari licha ya shinikizo za kuzima habari zilizochukuliwa kuonyesha walioko serikali katika mwanga mbaya.

-Wangethi Mwangi ni Mhariri Mkurugenzi wa zamani wa Nation Media Group PLC

-Imetafsiriwa na Fatuma Bariki