• Nairobi
  • Last Updated May 11th, 2024 3:59 PM
Jinsi ahadi hewa za wanasiasa na mwingilio wa makateli umeweka wakulima katika utumwa usioisha

Jinsi ahadi hewa za wanasiasa na mwingilio wa makateli umeweka wakulima katika utumwa usioisha

NA MWANGI MUIRURI

MTINDO wa viongozi na watunga sera nchini kupenda siasa, magendo na rushwa umeibuka kuwa kizingiti kikubwa zaidi katika kufanikisha utajiri katika sekta ya kilimo.

Makateli ambayo hujumlisha wanasiasa waliochaguliwa kwa ahadi ya kuimarisha kilimo wakishafika vyeoni, wanasemwa kwamba huwa wanakimbizana na biashara za udalali wa mavuno, uuzaji vifaa vya kilimo, wizi wa bidhaa za ruzuku, wizi wa vitita vya miradi na kusambaratisha mavuno ndio waagize chakula cha kuuzia wahanga wa njaa.

Sekta ya kilimo huletea taifa kiwango cha asilimia 33 cha utajiri wake wa kijumla hivyo basi kuwa uti wa mgongo wa uchumi na mara kwa mara hali huibuka ambapo wanasiasa wanapigana kuhusu sera za kuimarisha kilimo kwa msingi wa manufaa ya kibinafsi.

Badala ya taifa kuonekana likijizatiti kusaka uwiano wa sera za kustawisha sekta hiyo, kile kimejitokeza kwa kiwango kikuu ni muungano wa makateli ambao hutawala sekta hiyo katika kila safu yakielekeza faida kwao lakini wakulima wakibakia katika utumwa.

Kila serikali ikiingia mamlakani huwa na ahadi tele kuhusu vile sekta hiyo itaimarishwa kwa manufaa ya mkulima na uchumi wa kitaifa lakini wagombeaji wakishapata kura na kuunda serikali, wanazindua misiruru ya kutoa vijisababu vya ni kwa nini haiwezekani.

Kulainisha masoko

Kwa sasa, serikali ya Rais William Ruto imerithi hatamu za uongozi ikiahidi bei bora za sekta ya kilimo, kulainisha masoko na kuondoa utekaji nyara wa madalali na kutoa ruzuku za kusaidia wakulima kupata mavuno na pia faida katika soko.

Aidha, Rais Ruto ameahidi kwamba atabatilisha hali ambapo taifa la Kenya huagiza hata chakula kutoka nje kwa kima cha Sh500 bilioni akiapa kupunguza biashara hiyo kwa asilimia 50.

Lakini tayari Naibu wa Rais Rigathi Gachagua ameteta kwamba madalali na makateli katika sekta ya kilimo yanazima juhudi za kulainisha sekta hiyo kiasi kwamba sasa anaomba wakulima wawe na subira huku serikali ikisaka mbinu muafaka za kukabiliana na hali hiyo.

“Haya makateli huwa na ushawishi mkubwa na kwa sasa hata tunajadiliana nayo jinsi ya kugawana faida zao za juu kabla ya tupate mbinu bora ya kuwaondoa katika sekta hii ya kilimo. Makateli hayo hununua uungwaji mkono katika awamu za kutunga sera, huteka nyara mahakama na hata huwa yanaingilia na kudhibiti chaguzi za wakulima ndani ya mashirika yao. Ni kama virusi ambavyo vimesambaa hadi kwa masoko yetu ng’ambo,” Bw Gachagua akateta akiwa Murang’a mnamo Februari 10, 2024.

Waziri wa kilimo Mithika Linturi aliambia Taifa Leo Dijitali kwamba “kinyume na serikali zingine, hii ya Rais Ruto itaibuka kama iliyoahidi ikiwa na nia ya kutekeleza kila awamu ya mkondo wa kugeuza kilimo kuwa kivutio cha wengi na kitega uchumi”.

Alisema kwamba kwa sasa serikali imefanikiwa kupandisha bei ya macadamia kutoka Sh30 kwa kilo hadi Sh130 kwa sasa katika kipindi cha miezi 10 iliyopita. Aidha, anasema kwamba bei ya kahawa, majani chai na maziwa zinazidi kupanda huku serikali ikijizatiti kutoa ruzuku za fatalaiza, mbegu za mifugo na pia kuimarisha uthabiti wa masoko.

Kuchimba mabwawa

Aidha, alisema serikali iko mbioni kutekeleza ahadi ya kuchimba mabwawa 100 kabla ya 2027 ili kuimarisha kilimo cha unyunyiziaji maji na hivyo basi kupiga jeki uthabiti wa chakula cha lishe na cha kibiashara.

Lakini huku ikibainika kwamba serikali itahitaji ushuru wa kutekeleza hali hizo, tayari mvutano wa wanasiasa umeibuka huku kwa mfano, viongozi wa Mlima Kenya wakisema hawako tayari kukubalia wakulima wao kulipa ushuru huo kwa mapato ya mavuno.

Mnamo Februari 27 katika uwanja wa Kandara, Mbunge wa Gatanga Bw Edward Muriu akiandamana na mwenzake wa Kandara Bw Chege Njuguna pamoja na kinara wa walio wengi katika bunge la Kaunti ya Murang’a Bw Kibe Wasary walionya kwamba hawatakubali kushirikisha wakulima kwenye ushuru.

Akiwajibu, kinara wa walio wengi katika bunge la Seneti Bw Aaron Cheruiyot amesema kwamba “wakulima wote wanafaa kusawazishwa katika mikakati ya ushuru kwa kuwa hakuna walio wa kipekee kuliko wengine”.

Alisema kwamba yeye amekuwa akipigia debe wakulima wa kwake walipe ushuru “na sioni ni kwanini wengine wanajihisi kuwa wa kipekee kiasi kwamba wanapinga kutozwa ushuru”.

Seneta wa Murang’a Bw Joe Nyutu anasema kwamba mvutano kama huo ndio umekithiri tangu uhuru wa taifa na hapo ndipo sera husambaratika.

“Tungekuwa watu wa kujadiliana bila kuweka masilahi ya kisiasa na kibinafsi mbele, tungekuwa tumepata jibu kuhusu kulemewa kwetu kuimarisha mapato katika sekta ya kilimo. Tunatumia kilimo kama ajenda ya kisiasa badala ya kuwa ya kiuchumi na katika hali zote, wengi wanaonekana wazi wakikimbizana na manufaa yao wenyewe badala ya yale ya kuwafaa wakulima,” akasema.

Ufutaji madeni ya wakulima

Aidha, alisema kuna ufisadi mkuu katika ufutaji madeni ya wakulima ambapo “vitita hutolewa na huingia kwa mifuko ya wachache…hali ambayo ni lazima tuikalie ngumu ili kila sera ya kumfaa mkulima iwe inamfikia”.

Mbunge mwakilishi mwanamke wa Kaunti ya Nakuru Bi Liza Chelule aliambia Taifa Leo Dijitali kwamba maovu kama ya watu walio mamlakani kuiba fatalaiza ya ruzuku, pesa ya miradi ya kustawisha kilimo na pia kupinda sheria ili kuwafaa washirikishi wa makateli ni ushahidi tosha wa kazi ngumu inayokabili utawala wa Rais Ruto kufanikisha ajenda ya kilimo.

Mhadhiri katika Chuo kikuu cha Nairobi Prof Karuti Kanyinga anasema kwamba umefika wakati wa kuchukulia suala la makateli katika sekta ya kilimo kama janga la kitaifa.

Alisema kwamba maadui wa wakulima tangu taifa lijinyakulie uhuru wamekuwa ni baadhi ya maafisa wa serikali wakiungana na wafanyabiashara tajika ambao huunda mtandao wa kuhujumu hali na kuweka taifa katika biashara ya faida ya uagizaji chakula, uombaji wa chakula cha misaada na pia uuzaji wa vifaa.

[email protected]

  • Tags

You can share this post!

Tarajieni mvua nyingi Machi hadi Mei – MET

Tanzania yaongoza Afrika Mashariki kwa idadi kubwa ya watu...

T L