Jinsi ajali ilivyosababisha vifo vya marafiki wa tangu utotoni
NA WYCLIFFE NYABERI
FAMILIA za wasichana wawili walioaga dunia katika ajali ya barabarani, Januari 26, 2024, katika eneo la Daraja Moja, Kaunti ya Kisii, zimetaja jinsi marafiki hao walivyokuwa na ukaribu ulioshangaza kila mtu aliyewajua.
Nicole Nyamoita,17, na Ivy Kerubo, 16, ambao walikuwa wakingoja kujiunga na vyuo vikuu, walikuwa hawatengani tangu utotoni mwao na hata walipokuwa wakikutana nyumbani wakati wa likizo.
Mara nyingi watu wasiowafahamu walidhani wawili hao walikuwa mapacha kutokana na jinsi usuhuba wao ulivyokolea, wakipendelea kufanya shughuli zao pamoja.
Lakini sasa wasichana hao wametenganishwa na kifo baada ya kugongwa na gari lililokuwa limebeba vifaa vya ujenzi katika makutano ya Daraja Moja, kwenye barabara ya Kisii-Keroka.
Nicole alifanyia KCSE katika Shule ya Upili ya Kisumu Girls. Alipata B+ huku Ivy akipata B kutoka shule ya Moi Tea Girls katika mtihani ambao matokeo yake yalitolewa mapema Januari na Waziri wa Elimu Ezekiel Machogu.
Nicole alikuwa mzaliwa wa pili katika familia ya wana wawili. Mamake, Bi Caroline Mogotu alijitwika peke yake mzigo wa kumpa elimu bora akiwa na matumaini kwamba bintiye angekuwa mtu mashuhuri siku za usoni. Alifanya hivyo kupitia mapato madogo ambayo angepata kutokana na kuendesha duka dogo katika kituo cha kibiashara cha Bobaracho.
Akiwa anasubiri kujiunga na chuo kikuu baadaye mwaka huu wa 2024, Nicole aliamua kujiandikisha kwa Mpango wa Ajiry- mpango ulioanzishwa na serikali ya kaunti ya Kisii kuwasaidia vijana kuboresha ujuzi wao wa kidijitali kama njia mojawapo ya kuwatia moyo kuchangamkia teknolojia katika utayari wa kupata kazi za mtandaoni.
“Nicole alikuwa na somo Ijumaa jioni katika uwanja wa Gusii ambapo kwa kawaida madarasa ya programu hiyo hufanyika. Alimaliza na akaja kwenye kioski changu mjini Kisii akiwa na rafiki yake (Ivy). Niliwanunulia njugu na wakaondoka kuelekea nyumbani,” Bi Eunice Mokeira, nyanyake Nicole alisema kwa uchungu Taifa Leo ilipozuru nyumbani kwao Jumamosi asubuhi.
Aliongeza: “Nikiwa mjini, nilisikia kwamba ajali mbaya imetokea katika eneo la Daraja Moja. Watu walikuwa wakisema kuwa wawili walioaga dunia walikuwa wanafunzi wa Kisii National Polytechnic kwa sababu taasisi hiyo iko karibu na eneo ambapo walikumbana na kifo. Sikujisumbua sana hadi saa nne usiku nilipopigiwa simu kuwa waliohusika katika ajali ile ni mjukuu wangu na rafikiye.”
Bi Mokeira alisimulia jinsi ilikuwa vigumu kwa mwanawe Mogotu kusomesha watoto wake kama mjane.
“Mume wa Bi Mogotu alifariki 2018 na kumwachia jukumu la kuwasomesha watoto. Mjukuu wangu amekuwa maua yangu. Ibilisi amenitia aibu. Nimehuzunika, sijui ninaweza kuficha wapi uso wangu,” nyanya ya Nicole alihuzunika.
Habari za vifo hivyo zilishtua vijiji vya Bobaracho na Nyanguru wanakotoka.Wale wanaowafahamu wawili hao wasioweza kutenganishwa walijitahidi kukubaliana na habari hizo zilizowavunja nyoyo.
Taifa Leo lilipotembelea familia za wahasiriwa, jamaa zao walikuwa wamefadhaika sana.
Mamake Nicole alilia kwa uchungu kimya kimya. Hakuwa na nguvu za kufanyiwa mahojiano.
“Inauma. Kama familia, tumepigwa sana. Kwa sababu hii ilikuwa ajali, tunadai majibu. Tunahitaji kumjua mtu aliyesababisha ajali na ikiwa kuna fidia yoyote,” shangazi yake Nicole, Bi Spinicah Makori alisema.
Aliongeza: “Huyu alikuwa msichana mtiifu ambaye alikuwa mcheshi. Mama yake alijitahidi kumsomesha. Alikuwa akituambia kuwa hatafanya maendeleo yoyote hadi watoto wake wasome wote. Na kweli alifanya hivyo kupitia biashara yake ndogo kwa kuwapeleka katika shule nzuri. Nicole alikuwa na matamanio ya kufanya kozi ya fani ya utabibu ikiwa angejiunga na chuo kikuu.”
Takriban umbali chini ya kilomita mbili kutoka kwa kina Nicole, familia ya Ivy pia inamwomboleza.
“Ametangulia mbele ya haki haraka sana,” mmojawapo wa waombolezaji waliofika kwao alisikika akisema.
Mamake Ivy, Bi Alice Mogaka, ambaye ni mwalimu alikumbuka nyakati za mwisho alizowasiliana na kitinda mimba wake.
“Nilikuwa shuleni aliponipigia simu kunijulisha kuwa alikuwa akitoka na rafiki yake. Aliniambia kuwa chuo kimoja ambacho angetamani sana kujiunga nacho kilikuwa kinatoa mwongozo kuhusu uchaguzi wa kozi katika mji wa Kisii na hivyo akaomba ruhusa ya kuhudhuria. Nilimwambia msichana wangu ajitunze lakini alinijibu kwa utani kwa kuniambia kuwa sasa yeye ni mtu mzima na angerudi nyumbani kabla ya giza kuingia. Alikuwa akiniambia jinsi alivyotamani kufanya taaluma ya uanahabari lakini niliposikia kifo chake, niliona giza mbele yangu,” alisimulia Bi Kwamboka huku akilia kwa kwikwi.
Alimtaja binti yake kama msichana mchapakazi na mwenye upendo.
“Alikuwa mzungumzaji sana na aliniahidi kunifanya nijivunie. Alikuwa msichana aliyekuwa makini sana ambaye alipenda kwenda kanisani. Nitakukosa kipenzi changu,” Bi Mogaka alilia.
Gavana wa Kisii Simba Arati ametuma risala za rambirambi kwa familia zilizoachwa na kuahidi kusimama nao katika kipindi hiki kigumu.