Makala

Jinsi himaya ya ulanguzi wa bangi ilivyosambaratishwa akasukumwa jela miaka 10

April 18th, 2024 Kusoma ni dakika: 3

NA KALUME KAZUNGU

KWA zaidi ya miaka sita, Lucas Opondo Muguna, 45, amekuwa akiendesha biashara yake ya ulanguzi wa dawa za kulevya Lamu.

Amekuwa akijihusisha sana na usafirishaji na usambazaji wa mihadarati hiyo, hasa bangi, akifanya kila jitihada za kijanja ilmradi akwepe mkono wa sheria.

Muguna alitambulika na kuvuma sana miongoni mwa jamii ya Lamu kutokana na biashara hiyo mbaya.

Ila kwa muda wote huo, jamii haingefanya lolote kumkataza kutokana na vitisho na woga kumhusu.

Yaani hakuna aliyetamani siku moja kujipata pabaya mbele ya jamaa huyo waliyemuona kuwa hatari kwa usalama wao.

Alikuwa akifanya biashara hiyo haramu ya usafirishaji na uuzaji bangi, wakati mwingi akitumia sana mabasi ya usafiri wa umma yanayohudumu kwenye barabara kuu ya Mombasa-Garsen-Witu-Lamu, ilmradi mzigo ufike alikotaka.

Kupitia njia zake za kikora, ikiwemo kuabiri huduma za bodaboda, Bw Muguna alikuwa akikabidhiwa mzigo wake kila mara kutoka kwa mabasi aliyotumia kwenye stendi ya Moa iliyoko kati ya Gamba na Witu, ambapo baadaye alitumia pikipiki kusambaza bangi hiyo vijiji atakavyo Lamu.

Ikumbukwe kuwa mihadarati ni donda sugu miongoni mwa vijana Lamu kwani wengi wamegeuzwa kuwa goigoi na bila faida maishani kutokana na athari za mihadarati.

Kila mara viongozi wa serikali, ikiwemo kaunti kamishna, manaibu wao, machifu, wazee wa mitaa na pia viongozi wa kisiasa, ikiwemo Gavana wa eneo hilo, Issa Timamy, wamekuwa wakilalamikia janga la mihadarati lililoathiri vijana eneo hilo.

Zawadi ya Sh50,000 mshukiwa anaswe

Sehemu mojawapo ya Mahakama wa Mpeketoni, Lamu Magharibi ambapo hukumu ya Bw Muguna ilitolewa. Picha|Kalume Kazungu

Kuna wakati ambapo Gavana Timamy alisimama jukwaani na kutoa ahadi ya kumlipa Sh50,000 afisa yeyote wa polisi atakayefaulu kumnasa, kumfikisha kortini na kuhakikisha amefungwa msambazaji na mtumiaji yeyote wa dawa za kulevya eneo hilo.

Licha ya kuwepo kwa ahadi ya donge nono hilo, hakuna afisa yeyote wa polisi kufikia sasa ambaye amewahi kutunukiwa fedha hizo na Bw Timamy kwa kufaulisha juhudi za kumnasa na kumshtaki mhusika yeyote wa mihadarati, ikiwemo Muguna ambaye amekuwa akiendelea kunogesha biashara yake bila fujo.

Kwa idara ya polisi, Muguna alitambulika kuwa mtu ‘mwerevu’ ambaye hata polisi wenyewe alikuwa akiwapiga chenga au danadana, katu wasifaulu kumkamata na kuthibitisha uhusiano wake na biashara hiyo haramu.

Baada ya miaka yote ya kumfukuzia Muguna, mwishowe Idara ya Polisi Nchini (NPS) iliafikia kuhusisha huduma za polisi wa kitengo cha kukabiliana na matukio ya dharura (RDU) katika kumsaka na kumkamata Muguna aliyedhihirisha wazi kuwa mtu mponyokaji wa mitego iliyoko mbele yake si haba.

Ikumbukwe kuwa RDU ni kitengo ambacho mara nyingi kimetumiwa Lamu kukabiliana na magaidi wa Al-Shabaab.

Ni kupitia kuhusishwa kwa maafisa hao ambapo Bw Muguna alitegewa mtego wa aina yake, hivyo hatimaye kunaswa mzimamzima eneo hilo hilo la stendi ya Moa, tayari akiwa ameabiri mojawapo ya pikipiki na mzigo wake mnamo January 23, 2019.

Baada ya kufikishwa mahakamani na kufunguliwa mashtaka ya ulanguzi wa dawa za kulevya, Bw Muguna baadaye alifaulu kuachiliwa kwa dhamana lakini baadaye akatoweka katika hali tatanishi asiitikie kesi yake mahakamani tangu Novemba 9, 2022.

Hatua hiyo ilimlazimu wakili wake, ambaye alikuwa Bw Alfred Omwancha kujiondoa mnamo Aprili 6, 2023 baada ya juhudi za kuwasiliana na mteja wake huyo kushindikana.

Baada ya mara kadhaa ya kuahirishwa kusikilizwa na kuamuliwa kwa kesi yake kutokana na kukosa kufika mahakamani kwa Muguna, mwishowe ya Mpeketoni, Lamu Magharibi, ilitoa amri ya kukamatwa kwa mara nyingine kwa jamaa huyo.

Hii ni baada ya mdhamini wake aliyetambulika kwa jina Mzee Mark Otieno pia kujiondoa kwa kushindwa kutafuta na kumwasilisha Muguna mahakamani kama alivyokuwa ameihakikishia mahakama hiyo awali.

Baada ya ujanja wa mlanguzi huyo wa bangi, uliojumuisha kusafiri kutoka nchini kwenda kuishi nchi jirani ya Uganda, mwishowe alikamatwa na mafisa wa polisi punde alipofaulu kurudi nchini kwa mara nyingine na kujificha mjini Mombasa.

Alikamatwa tena mnamo Februari 10, 2024.

Hakimu Mkaazi Mwandamizi wa Mahakama ya Mpeketoni, Lamu Magharibi Eugene Pascal Nabwana. Alimpata Muguna na hatia ya ulanguzi wa bangi, hivyo kumhukumu miaka 10 gerezani au faini ya pesa taslimu Sh1 milioni. Picha|Kalume Kazungu

Ni juma hili ambapo alifikishwa mbele ya mahakama ya Mpeketoni iliyoko Lamu Magharibi.

Mbele ya Hakimu Mkaazi Mwandamizi, Pascal Eugene Nabwana, Muguna alipatikana na hatia ya ulanguzi wa dawa za kulevya aina ya bangi, ambacho ni kinyume cha sheria.

Alihukumiwa miaka 10 jela au alipe faini ya pesa taslimu Sh1 milioni, hivyo kupewa siku 14 za kukata rufaa.

Na hivyo ndivyo himaya ya miaka mingi ambayo alikuwa ameijenga na kuipalilia Muguna, ya biashara ya mihadarati, ilitiwa kikomo ghafla na kusambaratishwa kabisa, hivyo kuacha funzo la kimsingi kwa watu wengine wenye nia sawa na yake katika jamii ya Lamu, Kenya na ulimwengu kwa jumla.