Jinsi hospitali za Kenya zinavyovutia wagonjwa kutoka kote Afrika
ELIZABETH Mupako aliwasili jijini Nairobi Novemba 10, 2025 alfajiri kwa ajili ya matibabu.
Raia huyo wa Zimbabwe anayefanya kazi jijini Arusha, Tanzania, ana jeraha la goti.
Akizungumza na Taifa Dijitali, alisema alielekezwa Kenya kwa matibabu kwa sababu hapa ndipo anapopata wataalamu wote anaohitaji chini ya paa moja.
“Hapa, kuna Doctor’s Plaza yenye madaktari wataalamu wote ninaohitaji,” alisema.
Jeraha lake lilianzia mwaka 2016 akicheza kandanda. Matibabu aliyopata Arusha hayakusaidia, na hali yake ikazidi kuwa mbaya, hivyo akaelekezwa Nairobi ambako timu ya madaktari wataalamu, akiwemo daktari wa moyo, ubongo na mifupa, walianza kumtibu. Tangu wakati huo amekuwa akija Nairobi mara kwa mara.
Elizabeth ni miongoni mwa idadi ndogo ya raia wa kigeni wanaokuja Kenya kwa matibabu. Ripoti ya Utendaji wa Sekta ya Utalii ya mwaka wa Tourism 2024 inaonyesha kuwa watu 7,944 kutoka Jumuiya ya Afrika Mashariki walikuja Kenya kwa sababu za kiafya mwaka huo. Wengi walitoka Tanzania, wakifuatwa na Uganda, Sudan Kusini, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, Rwanda na Burundi.
Kenya inalenga kufikia mwaka 2030 kuwa kitovu cha matibabu maalum na utalii wa tiba barani Afrika. Wiki iliyopita, Hospitali ya Chuo Kikuu cha Aga Khan ilisaini makubaliano na Kenya Airways kurahisisha usafiri wa wagonjwa kutoka mataifa mengine ya Afrika.
“Mgonjwa anapopata matibabu karibu na nyumbani, ni rahisi zaidi kusafiri na kupona katika mazingira anayozoea,” alisema Mkurugenzi Mkuu wa hospitali hiyo, Bw Rashid Khalani.
Kenya Airways, kwa mujibu wa Dkt Ahmed Salat, hushughulikia takribani kesi 8,000 za wagonjwa kila mwaka, ikiwemo safari za wagonjwa wanaotibiwa au kupitishwa nchini kuelekea mataifa mengine. Shirika hilo hutoa huduma maalum kama oksijeni na machela ndani ya ndege, na madaktari au wauguzi huandamana na wagonjwa walio katika hali mahututi.
Hospitali ya Aga Khan hupokea maombi kutoka kote barani Afrika kwa wagonjwa wanaohitaji upasuaji tata, kupandikizwa figo, upasuaji wa moyo na majeruhi wa vita.
Vilevile, Hospitali ya Mafunzo, Rufaa na Utafiti ya Chuo Kikuu cha Kenyatta (KUTRRH) imekuwa kituo cha utalii wa tiba kwa kutumia teknolojia ya kisasa kama CyberKnife na cyclotron kwa matibabu ya saratani kwa usahihi mkubwa.
Kulingana na Dkt Zeinab Gura, Mkurugenzi Mkuu wa hospitali hiyo, wagonjwa kutoka zaidi ya nchi 27 za Afrika tayari wamepatiwa huduma, wengi wao wakiwa na matatizo ya saratani.
Hospitali ya Kenyatta National Hospital (KNH) pia imekuwa ikiwahudumia wagonjwa kutoka Afrika Mashariki na Kati.
KNH imefanya upasuaji tata ambao haujawahi kufanywa sehemu nyingine duniani, na ina kitengo maalum cha magonjwa ya figo na upandikizaji viungo, pamoja na maabara yanayopatikana humo pekee kote Afrika Mashariki.