Makala

Jinsi Maraga anapanga kujipatia uungwaji wa vijana kuelekea 2027

Na BENSON MATHEKA September 3rd, 2025 Kusoma ni dakika: 2

ALIYEKUWA Jaji Mkuu na mwaniaji urais katika uchaguzi mkuu wa 2027, David Maraga, ameahidi kutumia ubunifu wa vijana katika mpango wake wa kufufua uchumi.

Bw Maraga ameapa kugeuza ubunifu wa Wakenya kuwa chanzo cha ajira na utajiri iwapo atachaguliwa kuwa rais.

Kupitia chapisho katika akaunti yake rasmi ya X Jumanne, Septemba 2, 2025, Bw Maraga alisema kuwa mpango wake wa Rebuild the Economy (kujenga upya uchumi)umebuniwa kufungua fursa ambazo bado hazijagunduliwa miongoni mwa vijana, kwa kuhakikisha kuwa mawazo na ubunifu unatambuliwa, kulindwa, na kugeuzwa kuwa mali inayoweza kuingiza mapato.

“Ninakubaliana kuwa kuna fursa kubwa ambazo bado hazijatumika kwa vijana. Mpango wangu unaonyesha jinsi ya kubadili ubunifu kuwa mali halali na yenye thamani ya kibiashara. Serikali yangu itahakikisha kuwa ni rahisi kulinda, kuthamini, kuuza, kufadhili na kutekeleza haki za ubunifu zilizobuniwa humu nchini,” Bw Maraga alieleza.

Alisisitiza kuwa vijana wa Kenya wameonyesha vipaji vya kipekee katika nyanja mbalimbali kama vile teknolojia, utayarishaji wa maudhui ya kidijitali, sanaa, kilimo na ujasiriamali wa kisasa.

Hata hivyo, alisema kuwa nchi inaendelea kupoteza rasilimali kwa kukosa mifumo ya kulinda ubunifu na ukosefu wa msaada wa kifedha.

“Vijana wetu wameonyesha uwezo mkubwa, lakini bila ulinzi wa kisheria na upatikanaji wa fedha, ubunaji wao huishia kupotezwa au kuibwa. Hali hii lazima ibadilike,” aliongeza.

Kulingana na mpango wake, analenga kuimarisha sheria za hakimiliki, kupunguza gharama za kusajili hakimiliki, na kuweka mifumo ya kuwasaidia wavumbuzi chipukizi kupata masoko na ufadhili wa miradi yao.

Bw Maraga alihusisha pendekezo lake na maendeleo ya kiuchumi kwa upana zaidi, akisema kuthamini ubunifu si kwa vijana pekee bali ni njia ya kugeuza Kenya kuwa taifa lenye ushindani wa kimataifa.

Alidai kuwa kwa sera sahihi, Kenya inaweza kuuza teknolojia, sanaa, muziki na kazi nyingine za ubunifu nje ya nchi huku ikiunda ajira kwa mamilioni ya wananchi.

“Huu ni mkakati wa kiuchumi. Tukilinda, kufadhili na kuuza mali ya ubunifu, tutajenga ajira, utajiri, na heshima ya Kenya kimataifa,” Maraga alieleza.

Kauli yake inajiri wakati ambapo ukosefu wa ajira na hali ngumu ya kiuchumi vinazidi kuwa gumzo kuu nchini, huku vijana wakionyesha kukata tamaa kutokana na ukosefu wa fursa.