• Nairobi
  • Last Updated May 19th, 2024 7:52 PM
Jinsi misako ya kushtukiza inavyonasa ‘mapedi’ wa dawa za kulevya

Jinsi misako ya kushtukiza inavyonasa ‘mapedi’ wa dawa za kulevya

NA KALUME KAZUNGU

WAHUSIKA wengi wa biashara haramu ya dawa za kulevya, Kaunti ya Lamu wamekuwa na ujanja wa kukwepa mitego ya maafisa wa usalama.

Hali hiyo kwa miaka mingi imefanya juhudi za polisi kuwasaka na kuwatia mbaroni wahusika wa mihadarati eneo hilo kugonga mwamba.

Licha ya washukiwa wengi wanaoaminika kuwa walanguzi wakuu wa dawa za kulevya kujulikana, yamkini hata na wana jamii wenyewe wa Lamu, wengi wamekuwa wakiishia kutawala soko huru bila ya mkono wa sheria kuwafikia.

Aidha mbinu ya hivi punde iliyozinduliwa na maafisa wa usalama, hasa wale wa kisiwa cha Lamu, ya kutekeleza misako ya ghafla na isiyotarajiwa, iwe ni ya vichochoroni au nyumba hadi nyumba, imedhihirisha wazi kwamba vita dhidi ya dawa za kulevya Lamu vinaelekea pazuri.

Misako hiyo isiyo ya kawaida ilianzishwa juma hili na kushirikisha maafisa wa polisi wa kitengo maalum cha kupambana na mihadarati (ANU), wenzao wa Masuala ya Mipangilio na Kupambana na Jinai (TOCU) na idara ya Jinai nchini (DCI).

Ni mara ya kwanza kwa operesheni ya namna hiyo kutekelezwa kisiwani Lamu na viunga vyake.

Usiku wa kuamkia Jumanne kwa mfano, walinda usalama walifanya msako wa ghafla usiku wa manane.

Hali hiyo iliwapata wengi bila taarifa, hivyo kupelekea kunaswa kwa walanguzi, wasambazaji na watumiaji wakuu wa mihadarati ambao kwa miaka mingi wameshinda kabisa ujanja au rada ya walinda usalama.

Kwenye operesheni, walinda usalama walinasa jumla ya washukiwa saba wa usambazaji wa mihadarati kisiwani Lamu usiku wa kuamkia Jumanne wakiwa na gramu 928 za kokeni inayokadiriwa kuwa ya kima cha Sh3.7 milioni.

Katika mahojiano na Taifa Leo mnamo Jumanne, Kaimu Kamishna wa Kaunti ya Lamu Charles Kitheka alithibitisha kukamatwa kwa saba hao na kiwango hicho cha kokeni.

Alisema washukiwa hao, akiwemo mwanamke mmoja, tayari wako mikokoni mwa walinda usalama wakisubiri kufikishwa mahakamani wakati wowote.

Kulingana na Bw Kitheka, nyumba kadhaa zilizoshukiwa kuwa ngome kuu katika kuendeleza kichinichini biashara ya mihadarati, ndizo zilizopewa kipaumbele kwenye msako huo wa usiku wa manane.

Katika nyumba ya kwanza, walinda usalama walipata mizani na tembe tano za kokeni ambazo uzito wake ni gramu 85.

Katika nyumba ya pili, maafisa wa polisi walipata gramu 164 za kokeni zilizokuwa zimefichwa kwenye mfuko.

Kwenye nyumba ya tatu kulipatikana mfuko uliofichwa ukiwa umehifadhi karibu gramu 354 za dawa hiyo hiyo ya kokeni.

Msako pia uliendelezwa kwenye nyumba nyingine, ambapo gramu 325 za kokeni pia zilinaswa.

“Ni kutokana na msako huo wa usiku mmoja ambapo maafisa wetu walifaulu kuwanasa washukiwa hao wakuu saba wa dawa za kulevya kwenye mitaa mbalimbali ya kisiwa cha Lamu. Ni operesheni tunayoifanya kufuatia amri ya serikali wamba tukabiliane vilivo na kumaliza mihadarati,” akasema Bw Kitheka.

Kaimu Kamishna huyo alisema sababu kuu iliyopelekea idara ya usalama kutumia mbinu ya ushirikiano wa vitengo kadhaa vya polisi, ikiwemo maafisa wa vitengo maalum kama vile ANU na TOCU ni kutokana na kwamba baadhi ya washukiwa waliotafutwa walikuwa sugu na hatari.

“Kati ya washukiwa saba waliokamatwa, kuna mmoja anayefahamika kuwa mponyokaji sugu na hatari ambaye amekuwa kwa rada yetu kwa muda mrefu. Twashukuru kwamba mbinu mpya inazaa matunda. Misako itaendelezwa kote Lamu hadi eneo hili likombolewe kutoka kwa janga la mihadarati,” akasema Bw Kitheka.

Wakati huo huo, washukiwa wengine watatu wa ulanguzi wa dawa za kulevya pia walinaswa mtaani Kashmir, kisiwani Lamu usiku huo huo wa kuamkia Jumanne.

Naibu Kamishna wa Divisheni ya Amu, Bw Bravin Akolo, alisema washukiwa hao walikamatwa wakiwa na misokoto ya bangi.

“Watatu hao wako kituo cha polisi cha mjini Lamu wakisubiri kufikishwa mahakamani kukabiliwa na shtaka la ulanguzi wa mihadarati,” akasema Bw Akolo.

Aliwasihi wananchi kushirikiana na walinda usalama kwa kutoa taarifa za kusaidia kukamatwa kwa wahusika zaidi wa dawa za kulevya.

“Azma yetu kama serikali ni kupiga vita na kumaliza kabisa hili donda sugu la mihadarati kote Lamu. Twawasihi wananchi wema wenye taarifa kuwahusu wanabiashara wa mihadarati kutujulisha habari hizo ili kufaulisha hivi vita dhidi ya mihadarati,” akasema Bw Akolo.

Baadhi ya wakazi, ikiwemo viongozi wa dini, wazee na akina mama waliozungumza na Taifa Leo waliisifu idara ya usalama kwa kuibuka na mbinu ya misako ya kushtukiza wakisema ni kiboko yao katika kuwanasa ‘mapedi’ wa dawa za kulevya eneo hilo.

“Twaunga mkono kabisa juhudi za walinda usalama wetu katika kuwasaka na kuwanasa hawa wasambazaji na watumiaji mihadarati Lamu. Twaipokea kwa mikono miwili mbinu ya kusakanya dawa za kulevya na wahusika majumbani bila ya watu kutarajia, iwe ni usiku au mchana. Lazima tukomeshe mihadarati na kuokoa kizazi chetu,” akasema Mzee Omar Ahmed, mkazi wa mtaa wa Jua Kali kisiwani Lamu.

Bi Fatma Aboud alisema angalau kuna mwanga wa matumaini kwamba vita dhidi ya dawa za kulevya vitafaulu.

“Ninawasihi wanajamii wenzangu kwamba tuungane na hawa walinda usalama wetu ili kumpiga na kummaliza huyu adui anayeangamiza vijana wetu kupitia mihadarati,” akasema Bi Aboud.

Kwa miaka mingi, dawa za kulevya zimesalia kuwa changamoto Lamu, ambapo zimewaacha au kuwageuza vijana wengi goigoi kwa kuendeleza uraibu huo.

Miongoni mwa maeneo yanayotambulika kwa ulanguzi wa mihadarati Lamu ni Mtangawanda, Tchundwa, Mbwajumwali, na Kizingitini, kisiwani Pate, Lamu Mashariki.

Maeneo mengine ni Milano, Kashmir, Kijitoni, Gadeni, Bajuri na Wiyoni, Lamu Magharibi.

Miongoni mwa dawa zinazotumiwa sana ni bangi, heroni na kokeni ambazo kwa jina la mtaa zinatambulika kama ‘unga’.

  • Tags

You can share this post!

Eliud Kipchoge: Simwamini mtu yeyote… hata kivuli changu

Kagwe Mungai: Wanaoponda mahusiano yangu ya kimapenzi, kazi...

T L