Makala

Jinsi Tuju, Havi na Grand Mullah walivyokosesha Koome usingizi

December 23rd, 2025 Kusoma ni dakika: 3

MWAKA unaokamilika wa 2025 ulishuhudia mgogoro mkubwa wa kikatiba uliotamalaki tasnia ya sheria nchini huku majaji wa Mahakama ya Juu, akiwemo Jaji Mkuu Martha Koome, wakipambana kwa mara ya kwanza kabisa na kesi ya utovu wa nidhamu na shinikizo la walalamishi watatu kuwang’oa afisini.

Kilichoanza kama miaka kadhaa ya kushambuliwa na wakili Ahmednasir Abdullahi almaarufu Grand Mullah na kesi iliyozingirwa na utata kuhusu kupiga mnada mali ya mwanasiasa Raphael Tuju, kilibadilika kuwa mmoja kati ya mivutano ghali zaidi ya kitaasisi katika historia ya majuzi nchini.

Chimbuko la mgogoro huo ni misururu ya shutuma zilizotolewa kwenye mitandao ya kijamii na mawakili mashuhuri na wakuu akiwemo Nelson Havi.

Mawakili Havi na Bw Ahmednasir waliowahi kuwa marais wa LSK, waliwalenga majaji wakuu kupitia jumbe zao zilizovutia kauli kali kutoka kwa Mahakama ya Juu na kusababisha malalamishi yaliyochochea juhudi za ufurushaji kupitia kwa Idara ya Huduma za Mahakama (JSC).

Mnamo Januari 2024, mahakama ya juu ilimzuia Bw Ahmednasir na mawakili wanaofanya kazi katika shirika lake kufika mbele yake, ikinukuu kampeni iliyodaiwa kulenga “kuichafulia jina, kuidhihaki na kuitweza” taasisi hiyo.

Kaulimbiu yake iliyofahamika kama ‘jurispesa’ ilivutia umaarufu kwenye ulingo wa sheria nchini.

JSC, asasi ya kikatiba iliyotwikwa wajibu wa kudumisha nidhamu na utimuaji, iligeuka kiungo muhimu katika mivutano hiyo.

Januari 2025, Bw Havi, pamoja na waziri wa zamani Tuju na wakili Christopher Rosana, waliwasilisha kesi kwa JSC wakisema kwamba Jaji Mkuu Koome na wenzake wanapaswa kutimuliwa.

Kesi hizi zilitaja utovu wa nidhamu, mienendo isiyofaa na utendakazi duni katika majukumu yao yanayohusu idara ya mahakama.

Februari 2025, JSC iliwaamuru rasmi majaji wa Mahakama ya Juu kujibu kesi za kuwabandua, hatua iliyoashiria mwanzo wa mchakato wa nidhamu.

Jaji Mkuu na Mahakama ya Juu walijibu, si katika majengo ya JSC, bali katika Mahakama Kuu, wakikaidi msingi wa mamlaka ya JSC.

Chini ya Vifungu 171 na 172 vya Katiba, JSC ina mamlaka ya kuchunguza na kupendekeza maafisa wa Idara ya Mahakama kuondolewa kwa kushindwa kufanya kazi, utendakazi duni na utovu wa nidhamu.

Majaji na mawakili wanaoegemea idara ya mahakama walihoji kuwa JSC ilikiuka wajibu wake kwa kuchunguza maamuzi yaliyotolewa katika utekelezaji wa wajibu wa korti ya juu.

Athari za kisiasa na kisheria zilikuwa kubwa.

Bw Tuju alivuruga mambo zaidi kupitia msururu wa barua kwa Jaji Mkuu, akishutumu korti ya kilele kwa ubaguzi na kukosa uwajibikaji.

Katika barua moja, alilalamika kwamba jopo la majaji watano wa Mahakama ya Juu waliidhinisha mali yake ya ekari 27 iliyopo Karen, kupigwa mnada katika mzozo na benki ya East African Development.

Mahakama Kuu iliwapa afueni majaji hao kwa kuingilia kati.

Uamuzi wa Februari ulitoa amri ya muda kuzuia JSC kujibu kuhusu kesi za ufurushaji, ikisema mchakato huo usimamishwe kusubiri kesi hiyo kukamilika.

Pendekezo la utimuaji lilifichua mwanya wa kisheria ambao wengi hawakuwa wameona: jopo zima la korti ya juu linaweza kukata rufaa liking’atuliwa afisini?

Kifungu 168 cha katiba kinasema jaji anayetimuliwa afisini, baada ya uchunguzi wa jopo maalum ana haki ya kukata rufaa dhidi ya uamuzi huo moja kwa moja kwa korti ya juu katika muda wa siku 10, kuruhusu mahakama ya juu kutathmini upya udadisi wa jopo maalum na mapendekezo kuhusu ufurushaji.

Mbali na mivutano ya kisheria, mgogoro huo uliweka wazi taharuki kati ya uhuru wa idara ya mahakama na uwajibikaji katika mazingira yenye joto kali la kisiasa.

Wafuasi wa majaji wa mahakama hiyo ya kilele walilalamikia idara ya mahakama kushambuliwa mitandaoni, jambo ambalo Muungano wa Mahakimu na Majaji nchini ulitaja kuwa hila za kuhujumu utendakazi wa idara ya mahakama.

Japo mgogoro huo haujasuluhishwa, umebadilisha mdahalo wa umma kuhusu kugawanya mamlaka.

Idara ya mahakama ilishinda michakato muhimu, lakini maswali nyeti kuhusu mikakati yake ya uwajibikaji yangalipo.

Koome na wenzake wanapojiandaa kwa vikao zaidi vya kusikiza kesi hiyo na uwezekano wa mgogoro huo kutokota hata zaidi 2026, matokeo yataathiri katiba na mizani ya mamlaka kitaasisi.