Jinsi ya kujiepusha na madeni
Na MARGARET MAINA
MARA nyingi watu hujikuta katika madeni makubwa.
Kwa kiasi kikubwa watu wengi huingia kwenye madeni kutokana na kuwa na kiwango kikubwa cha matumizi kuliko kipato.
Madeni sio kitu kizuri hasa ikiwa hayatalipwa kwa wakati unaofaa.
Jiwekee bajeti
Bajeti binafsi ni muhimu kwani hukuwezesha kupanga juu ya mapato na matumizi yako. Bajeti itakuongoza juu ya matumizi yako ya pesa ili usije ukatumia kuliko kipato chako.
Epuka matumizi yasiyo ya lazima
Kuna matumizi mengi ya pesa, lakini matumizi ya lazima ni machache. Ikiwa kipato chako ni kidogo, hakuna haja ya kufanya mambo yenye gharama kubwa.
Epuka kukopa bila mpango
Watu wengi hushindwa kurejesha mikopo kutokana na kukopa bila mpango. Inatakiwa kabla ya kukopa, uhakikishe una mpango mzuri unaoonyesha jinsi utakavyotumia na kurejesha mkopo huo.
Tumia vizuri huduma na bidhaa
Kutumia vizuri huduma kama vile maji, simu, umeme, gesi au hata mafuta kutakuwezesha kuokoa kiasi kikubwa cha pesa.
Hakikisha kila kiasi cha hela unazoweka kwenye huduma hazipotei. Hili litakuokolea pesa nyingi ambazo utazitumia kwa mahitaji mengine na kuepuka madeni.
Tumia kidogo kuliko unachopata
Mara nyingi matumizi huwa makubwa kuliko kipato; na hii ndiyo sababu kubwa ya watu kukopa pesa. Hakikisha unajitahidi kutumia pesa kidogo kuliko zile unazozipata ili ujiwekee akiba na uweze kukidhi mahitaji yako ya msingi.
Weka akiba
Kwa njia ya kujiwekea akiba utaweza kuwa na pesa hata wakati huna kipato.
Lipa madeni kwa wakati
Kutolipa deni kwa wakati hukufanya ujiwekee mzigo mkubwa na wala si kupunguza chochote.
Hakikisha unalipa madeni kwa wakati, hasa madeni ya taasisi za kifedha kwani kutolipa kwa wakati kutakufanya uongeze riba ya mkopo zaidi.
Tafuta chanzo kingine cha kipato
Mara nyingi milango ya kutoa pesa ni mingi kuliko ile inayoleta pesa. Ni muhimu kutokutegemea chanzo kimoja cha pesa kwani kikikwama au kuzidiwa itakubidi ukope.