Jinsi ya kutambua pombe salama na ile itakayokuua au kukupofusha
NA LABAAN SHABAAN
POMBE (aina ya methanol) kijiko kimoja cha jikoni sawa na mililita 10 inaweza kumfanya mnywaji kuwa kipofu wa maisha mbali na kusababisha kifo.
Shirika la Afya Duniani (WHO) linakisia angalau robo ya pombe inayouzwa duniani ni haramu.
Lakini utafiti umeonyesha kuwa takwimu hizi ni kubwa sana katika nchi zinazoendelea kama vile Kenya.
Zaidi ya asilimia 33 ya pombe inayouzwa Afrika inatengenezwa na kuuzwa kinyume cha sheria.
Pombe ya magendo husababisha vifo kwa jamii maskini ambazo haziwezi kumudu bei ya bidhaa halali.
Athari ya vileo hivi huwa mbaya sana kwa wasioweza kupata chakula na hata kufikia huduma bora ya afya.
Baadhi ya pombe hizi hutengenezewa nyumbani.
Vinywaji hivi huwa haramu na hususan havikidhi viwango vya ubora na uwazi.
Pengine mnywaji anaweza kudhani pombe mbovu huuzwa katika mabaa ya vichochoroni tu ambavyo havina vibali vya kuhudumu.
Ripoti zimeeleza kuwa pombe zilizotengenezwa kwa njia haramu pia hupatikana katika maduka na maeneo ya burudani yaliyoidhinishwa kisheria.
Maruerue yasiyoisha
Wakora wanatengeneza pombe mbaya zinazosababisha maruerue yasiyoisha, upofu na hata maafa.
Viungo vibaya vinavyowekwa katika pombe hizi ni vile vinazohusisha, methanol, kishushamgando (antifreeze) na kemikali zinazotumika kuondoa rangi ya kurembesha kucha na rangi mbalimbali.
Pombe salama na halali huwa na kemikali ya ethanol ambayo hutengenezwa kwa viwango vilivyokubalika na Bodi ya Kutathmini Ubora wa Bidhaa nchini (KEBS).
Wanaoghushi pombe na kuuza vileo vya magendo hupunguza gharama ya uzalishaji kwa kutumia viungo vya bei ya chini ambavyo ni sumu kwa binadamu.
Vigezo ambavyo hutofautisha pombe salama na hatari ni inakouziwa, bei, upakiaji na sifa yake.
Ili uwe salama mtumiaji anafaa kununua pombe kutoka kwa maduka yanayojulikana kama mabaa na supamaketi.
Wataalamu wanashauri kutonunua pombe kutoka kwa wachuuzi, wauzaji wasio na leseni ama kutoka kwa wateja walio ndani ya baa.
Bei ya chini
Iwapo pombe inauzwa kwa bei ya chini ya viwango vya kawaida huenda ni feki.
Pombe hizi aghalabu pia hukosa kuhusisha matozo ya ushuru katika bei yake.
Vile vile, upakiaji wa pombe feki huwa bayana na yenye maandishi yasiyo sahihi.
Wakati mwingi hukosa kuwa na maelezo ya mawasiliano ya kampuni inayoitengeneza.
Itamhitaji mtumiaji pia kutumia apu ya simu kutambua msimbo upao (barcode) kwenye kifurushi kama ni bidhaa halali.
Kadhalika, vileo hivi huwa na ladha na harufu tofauti kama ya rangi na kemikali nyingine.