Makala

Jinsi Ziwa Turkwel linang’ang’ana kufuta historia ya kuwa kitovu cha ujangili

May 29th, 2024 Kusoma ni dakika: 3

NA OSCAR KAKAI

KWA miongo mingi, eneo la Turkwel  kwenye mpaka wa kaunti za Pokot Magharibi na Turkana, limekuwa likigonga vichwa vya  vyombo vya habari kama kitovu cha wizi wa mifugo.

Ziwa Turkwel sasa limejizoea sifa si haba kama kivutio cha utalii eneo nzima la Bonde la Ufa.

Ziwani Turkwel kuna vivutio mbalimbali wakiwemo mamba, viboko, na ndege.

Ziwa Turkwel ni mojawapo ya maziwa ambayo yalitengenezwa na binadamu na huwa na mandhari ya kiasili ya kuvutia watalii wa humu nchini na wa kigeni.

Bwala la Turkwel ndani ya Ziwa Turkwel nalo lina umuhimu mkubwa kama uzalishaji umeme na pia huchangia maji ya unyunyiziaji maji mashamba na kuendeleza shughuli za uvuvi. Hivi vyote huwavutia watalii ama wa kujifurahisha au wa kutaka kuja kujifunza.

Wavuvi ndani Ziwa Turkwel katika Kaunti ya Pokot Magharibi. PICHA | OSCAR KAKAI

Lilijengwa baina ya 1986 na 1991. Linasaidia kama mtambo wa tatu wa kuzalisha umeme nchini baada ya kuwekwa megawati 106 za umeme.

Wakati wa ujenzi wa bwawa hilo miaka ya themanini (1980s), wakazi wengi eneo hilo walikumbwa na changamoto nyingi kama kupoteza makazi, kuvamiwa na mamba pamoja na mbu.

Hata hivyo, ziwa pamoja na bwawa hilo vimeanza kuzaa matunda ambapo biashara ya uchukuzi kwa mashua inanoga, waendeshaji wakiwabeba watalii wanaovutiwa na mazuri yaliyoko huko.

Mazingira ya eneo hilo ya milima na mabonde na mandhari mazuri ya kuvutia, ndani kwenye maji kukiwa na ndege na mamba ambao huota jua eneo la Tipett kando ya ziwa hilo, ni vuvutio tosha vya kumwaga noti kwa kaunti.

Watu wakijionea milima karibu na Ziwa Turkwel katika Kaunti ya Pokot Magharibi. PICHA | OSCAR KAKAI

Watalii hufurahia kuwaona mamba wakiwa wamepanua midomo na hata kutambaa.

Wakati mwingine, unaweza kubahatika kuona mamba wakitaga mayai kwenye milima na hata kuyaangua.

Shughuli nyingine za utalii zinahusisha watalii kufurahia lifti kwa boti, kupanda milima ya mawe, kupiga kambi, kuvua samaki, kutazama ndege wakiruka, kushiriki michezo ya pamoja, na kuwatazama wanyama, hasa viboko.

Pia watalii hutangamana na wakazi wa kiasili na kuelezwa kuhusu utamaduni wao eneo la Tippet. Wanajifunza mengi ikiwemo densi, nyimbo na mila za kijadi pamoja na vyakula vya kiasili.

Ukiwa kwenye ziwa pia utaona milima ya kuvutia ya Riting.

Bw Joel Lokomol ambaye ni mwendeshaji wa mashua, anasema kuwa ziwa Turkwel limekuwa baraka kwake sababu ameweza kutoka kwa mashua ndogo hadi akanunua mashua kubwa na sasa analisha familia yake wakati watu wanalipa fedha kuzunguka ndani ya maji na mashua yake.

“Vijana wengi wamepata shughuli za maana na biashara, huku visa vya wizi wa mifugo vikifikia kikomo,” asema Bw Lomukol.

Anasema kuwa kila wiki mamia ya wageni hufika katika eneo hilo wakiwemo wanafunzi na watu watu wakubwa kutoka kwa mashirika mbalimbali.

“Imetusaidia kujikimu kimaisha tofauti na awali ambapo tulikuwa hatuna ajira. Tumenufaika pakubwa na kazi ya kuendesha mashua,” asema.

Mtalii  wa nyumbani Bw Edwin Naitale, anasema kuwa amesafiri zaidi ya kilomita 80 kutoka mjini Kapenguria hadi eneo hilo kujionea na kujivinjari kwenye lami ambayo imewekwa kuingia kwenye bwawa hilo.

Anawashauri Wakenya kuzuru eneo hilo.

 “Ni raha kusafiri kwenye mashua. Wale ambao wamejaribu hawawezi kusahau,” asema Bw Naitale.

Mkazi mwingine, Bw Peter  Tout, anasema kuwa alipozuru Turkwel, ilikuwa ni mara yake ya kwanza kuenjou lifti ya mashua na alisikia vizuri kabisa.

Watu wakiwa kwa mashua ndani ya Ziwa Turkwel katika Kaunti ya Pokot Magharibi. PICHA | OSCAR KAKAI

Chifu wa eneo hilo Bw William Lomada anasema kuwa bwawa hilo limekuwa na shughuli nyingi sababu wakazi wanaweza kusafiri na kusafirisha bidhaa kutoka eneo moja hadi lingine na wakazi wanakarbisha wageni.

Karibu na bwawa la Turkwel pia kuna ikulu ndogo ambayo inakarabatiwa na mamlaka ya kustawisha eneo la Bonde la Kerio (KVDA).

KVDA ndio inamiliki na kusimamia bwawa hilo baada ya kukosa kutumika kwa muda mrefu.

Meneja Mkurugenzi wa KVDA Sammy Naporos anasema kuwa ikulu hiyo ndogo itakuwa ikibeba zaidi ya watu  3,000 wakati wa shughuli za serikali.

Anasema kuwa mpango huo utachochea maendeleo katika eneo hilo na kuwafanya wakazi kutangamana na maafisa wa serikali.

Gavana wa Kaunti ya Pokot Magharibi Simon Kachapin anasema kuwa kufunguliwa kwa eneo hilo kupitia utalii kutasaidia kuongeza mapato ya kaunti na serikali kuu.

“Kaunti ya Pokot Magharibi ni kaunti yenye mambo mema mazuri yaliojificha. Kaunti itapata mavuno kutoka kwa bwawa. Mashindano ya boti yatabuni nafasi za ajira kwa vijana ambao wameasi visa vya wizi wa mifugo,” asema gavana Kachapin.

Bw Kachapin anasema kuwa shughuli hizo zinanuia kuendeleza uchumi wa eneo hilo .

“Tunakaribisha watalii waje kwa fujo,” asema.

Anasema kuwa shughuli hizo zitafanya eneo hilo kuzipatia serikali za kaunti na kitaifa mapato na kupunguza visa wa utovu wa usalama.

Mbunge wa Kapenguria Samuel Moroto anasema kuwa kuna  haja ya kuanzisha utumizi wa mashua kwenye bwawa la Turkwel kama shughuli ya kila mwaka ambayo itakuwa ikivutia watalii katika eneo hilo.

“Mashua hiyo itasaidia kuvutia watu wengi ambao wanajua kutumia na kujifamamisha na  utamaduni ya jamii ya Pokot,” asema Bw Moroto.

Anawashauri wakazi kuzuru eneo hilo na kujionea milima ambayo inazingira bwawa hilo huku akiwataka waekezaji kuzuru eneo hilo ili kujionea mandhari yanayozingira bwawa hilo hata kujenga mikahawa katika eneo hilo

“Waekezaji wanakarishwa katika eneo hili na wanaweza kujenga mikahawa karibu na bwawa hili,” asema mbunge huyo.

Katika eneo hilo la Turkwel, kuna mbuga ya watalii ya Nasolot ambayo ina ndovu wakubwa zaidi duniani. Pia kuna milima ya Nasolot.

Kuwepo kwa watalii kumechangia biashara kunawiri kwenye kituo cha kibiashara cha Riting na pia amani ikiimarikana eneo hilo.

[email protected]