Joho mbishi wa siasa, siku hizi kimya, kunani?
NA MOHAMED AHMED
SIASA za ubabe na kujipiga kifua ndizo zilizompa umaarufu Gavana wa Mombasa Hassan Joho.
Ubabe wake aliouthibitisha kwa kumtupia cheche za maneno Rais wa nchi Uhuru Kenyatta zilimfanya Joho ajizolee sifa huku wengi wakimtaja kuwa shujaa na kiongozi jasiri.
Hata hivyo, licha ya kujulikana kupitia siasa hizo, Bw Joho sasa amewaacha wengi kwa mshangao akisema kuwa yeye hataki siasa za ubabe na zile za mbwembwe.
“Mimi siasa zangu ni za maendeleo na zile za kutafuta namna za kujadili masuala ambayo yanamhusu mkazi wa Pwani. Hilo ndilo lengo langu sasa. Mimi nataka kuongea kuhusu vile tutaleta maji, kazi na mambo mengine ya maendeleo kwa wakazi wala si siasa za kutupiana cheche,” alisema Bw Joho mapema wiki hii akiwa afisini kwake.
Gavana Joho alisema kuwa anashangazwa na siasa za hivi leo ambazo zimejaa mbwembwe na matusi.
“Unajua kwa nini mimi ni gavana? Ni kwa sababu mimi nataka kuongea kuhusu mambo ya maendeleo pekee na si mambo mengine ya kando ambayo hayana msingi,” akaongeza.
Alisema kuwa kuna haja ya viongozi kujihusisha na siasa za maendeleo ambazo zitaleta manufaa kwa wananchi.V
ile vile, Bw Joho alimshambulia hasimu wake; Naibu wa Rais William Ruto na kumkemea kwa kuja Pwani kufanya kile alichokitaja kuwa siasa bila ya kujali ugonjwa wa virusi vya corona.
“Inakuwaje wewe kama kiongozi unakuja katika kaunti ya Mombasa ambayo imeripotiwa kuwa na visa vya corona kuendeleza siasa? Kuna vitu vingi vya maana vya kufanya kwa sasa badala ya siasa,” akasema Bw Joho.
Hata hivyo, kuonyesha kuwa maneno yake yalikuwa ni makeke tupu, siku iliyofuata kinara wa chama cha ODM Raila Odinga naye alifululiza hadi katika kaunti ya Taita Taveta na kuonekana kutangamana na watu akiendeleza kampeni za BBI.
La kushangaza zaidi ni kuwa siku ya pili, Bw Joho pia aliungana na Bw Odinga katika siasa hizo eneo la Mwatate katika kaunti hiyo ya Taita Taveta.
Ni hali hii ya unduma kuwili ndiyo imeibua maswali miongoni mwa wachanganuzi wa siasa ambao wamemtaja Bw Joho kuwa kiongozi wa kujali maslahi yake binafsi sawa tu na wale wengine.Profesa Hassan Mwakimako asema kuwa matamshi ya Bw Joho hayafai kuchukuliwa na umuhimu wowote kwani ni wazi kuwa yeye ni kiongozi ambaye huendesha na siasa za ushabiki.
“Hawa ni viongozi ambao wanaendeshwa na siasa za ushabiki na si misimamo ya maadili yao kama viongozi. Leo watasema hili kesho waseme lile. Wao hulenga pale panapowafaa,” akasema Profesa Mwakimako.
Kuhusiana na kubadilika kwa siasa zake kutoka zile za mbwembwe na kujipiga kifua hadi zile ambazo Bw Joho amezitaja kuwa za maendeleo, Prof Mwakimako anasema kuwa hilo ni zingatio ambalo Bw Joho alifaa kuliweka maanani mapema kuanzia kuchaguliwa kwake miaka saba iliyopita.