Kaburi la Raila lageuka mlima wa maua
ZAIDI ya wiki moja baada ya mazishi ya aliyekuwa Waziri Mkuu Raila Odinga, kaburi lake limeendelea kuvutia maelfu ya wageni wanaoendelea kuweka shada za maua, jambo lililofanya mazishi yake kuwa kati ya yale ya kipekee zaidi katika historia ya Kenya.
Mbali na mazishi ya kitaifa yaliyoandaliwa ndani ya saa 72, wafuasi waliovamia Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Jomo Kenyatta (JKIA) kupokea jeneza lake, na Wakenya waliopanga foleni ndefu kuutazama mwili wake, mlima wa maua uliotanda juu ya kaburi lake umekuwa kivutio kikubwa kwa wengi.
Kwa kipindi cha wiki moja iliyopita, nyumba ya Bw Odinga katika Opoda Farm na eneo la Kang’o Ka Jaramogi ambako alizikwa, zimekuwa zikipokea wageni kutoka sehemu mbalimbali nchini na hata mataifa jirani.

Kila kundi linalofika huweka shada la maua, kiasi kwamba wafanyakazi wa nyumbani wamekuwa wakilazimika kuyatoa kila baada ya siku mbili ili kutoa nafasi kwa wageni wengine.
“Baada ya kila siku mbili tangu mazishi ya Jakom, tumekuwa tukiondoa maua kaburini ili kutoa nafasi kwa wageni wengine. Ni jambo la kipekee kwa sababu watu wamekuwa wakija kila siku wakiwa na maua,” alisema mmoja wa wafanyakazi ambaye hakutaka jina lake litajwe.
Aliongeza kuwa, “Kama tungeliacha maua yote pale, sijui sehemu hiyo ingekuwaje. Kutokana na mvua inayoendelea, mengine yangekuwa yameanza kuoza kwa sababu yote ni maua mabichi.”
Mnamo Jumatatu, Oktoba 20, ujumbe wa watu 70 kutoka Uganda, hasa kutoka jamii ya Acholi ulifika katika makazi ya familia na kuweka shada za maua.
Rais mstaafu Uhuru Kenyatta alizuru kaburi hilo siku moja baada ya mazishi na tangu ziara yake, wageni wameendelea kumiminika nyumbani kwa familia ya Odinga.

Seneta wa Siaya, Dkt Oburu Oginga, alitangaza rasmi kumalizika kwa kipindi cha maombolezo siku nne baada ya mazishi, lakini wageni bado wanaendelea kuwasili kwa wingi.
Baadhi ya wageni mashuhuri waliotembelea kaburi la Bw Odinga ni wazee wa jamii ya Kikuyu ambao walifika na kundi la ng’ombe na kuweka maua kaburini.
Ujumbe kutoka Kaunti ya Kilifi, Magavana wakiongozwa na Gavana wa Wajir Ahmed Abdullahi, na aliyekuwa waziri wa Usalama wa Dkt Fred Matiang’i na ujumbe wa kutoka Kisii pia walifika nyumbani kwa Bw Odinga kuweka maua na kutoa pole zao.
Aliyekuwa Mbunge wa Rangwe, George Oner, akiwa na kikundi cha wanadensi cha Kagan Kochia, walifika Kang’o Ka Jaramogi wakiimba nyimbo za kumtukuza Bw Odinga na kuweka shada za maua.

Mbunge wa Uriri, Mark Nyamita, naye alifika na viongozi kadhaa akiwa na lori lililojaa ng’ombe na wakaweka maua kaburini sawa na mashabiki wa Asernal.