Makala

Kadinali Besungu kutoka DRC Mwafrika wa kipekee kupigiwa upatu kumrithi Papa Francis

Na CHARLES WASONGA April 22nd, 2025 Kusoma ni dakika: 2

KADINALI Fridolin Ambongo Besungu ndiye wa kipekee kutoka bara la Afrika aliye kwenye orodha ya makadinali wanane wanaopigiwa upatu kumrithi Papa Francis aliyekufa Jumatatu, Aprili 21, 2025.

Jina la Kadinali Besungu, 65, ni miongoni mwa yale yaliyonakiliwa kwenye kitabu cha Edward Pentin “The Next Pope: The Leading Cardinal Candidate” na hata mitandaoni.

Besungu aliteuliwa kuwa kadinali mnamo 2019 na marehemu Papa Francis.

Kadinali huyo, ambaye ni Rais wa Muungano wa Maaskofu wa Kanisa Katoliki Afrika na Madagascar, anasemekana kupinga baadhi ya sera zilizotekelezwa na Francis.

Kwa mfano, alipinga sera ya “Fiducia supplicans” inayoruhusu makasisi kuwabariki makapera na wanandoa wa jinsia moja.

Wengine kutoka nje ya Afrika kwenye orodha ya wanaopigiwa upatu kumrithi Francis ni wafuatao:

  1. Kadinali Pietro Parolin

Kadinali Parolin, 70, ni raia wa Italia na aliteuliwa na Papa Francis kuwa Kadinali mnamo 2014.

Wakati huu yeye ni mwanadiplomasia, anayehudumu kama Waziri wa Masuala ya Kigeni wa Vatican.

 2. Kadinali Wim Eijk

Kadinali Eijk, mwenye umri wa miaka 71 ni raia wa Uholanzi. Jina lake pia limetajwa kama miongoni mwa wale wanaopigiwa upatu kuchaguliwa kuwa Papa.

Kadinali Eijk alihudumu zamani kama daktari na ni miongoni mwa makadinali wanaochukuliwa kuwa wahafidhina.

Aliteuliwa kuwa Kadinali na Papa Benedict XVI mnamo 2012.

3. Kadinali Peter Erdo

Kadinali huyu mwenye umri wa miaka 72 ni raia wa Hungary na pia anachukuliwa kuwa kadinali mhafidhina. Kadinali Erdo ni Rais wa zamani wa Baraza la Maaskofu wa Kanisa Katoliki Uropa.

Aliteuliwa kuwa Kadinali mnamo 2003 na Papa John Paul II.

4. Kadinali Luis Antonio Tagle

Ni raia wa Ufilipino na aliteuliwa na Papa Benedict XVI mnamo 2012.

Akichaguliwa kuwa Papa, Kadinali Tagle, 67, atakuwa mtu wa kwanza kutoka bara Asia kushikilia wadhifa huo mkubwa zaidi katika Kanisa Katoliki.

5. Kadinali Raymond Burke

Raymond Burke anatoka jimbo la Wisconsin nchini Amerika.

Burke, 76, ni Askofu Mkuu wa zamani wa Kanisa la St Louis.

Aliteuliwa Kadinali na Papa Benedict XVI mnamo mwaka wa 2010. Kwa mara si moja amepinga baadhi ya sera za Papa Francis.

6. Kadinali Mario Grech

Aliteuliwa kuwa Kadinali mnamo 2020 na Papa Francis na ni raia wa Malta.

Wakati huu, Kadinali Grech ni Katibu Mkuu wa Kamati ya Maskofu na itikadi yake ni ile ya kati.

Kadinali Grech ni mwenye umri wa miaka 67 na ndiye mwenye umri mdogo zaidi kwenye orodha ya makadinali wanaopigiwa upatu kuchaguliwa kuwa warithi wa Papa Francis.

7. Kadinali Matteo Zuppi

Aliteuliwa kuwa Kadinali na Papa Francis mnamo 2019.

Kadinali Zuppi mwenye umri wa miaka 69 atatoka Italia na wakati huu ndiye Rais wa Muungano wa Maskofu wa Kanisa Katoliki Italia.

Kulingana na kanuni kuhusu uchaguzi wa Papa, kiongozi huyo huchaguliwa na Kundi la Makadinali, wote wakiwa wanaume.

Wao huteuliwa na Papa na aghalabu huwa ni Maaskofu waliotawazwa rasmi.

Wakati huu, Kanisa Katoliki lina jumla ya Makadinali 252. Lakini ni makadinali 138 pekee ambao wamehitimu kuchagua Papa kwani wale wenye umri wa zaidi ya miaka 80 hawaruhusiwi kushiri zoezi hilo.

Mnamo 2013 ni Makadinali 115 walioshiriki uchaguzi wa Papa Francis japo baada ya wawili kutoshiriki zoezi hilo.

Papa Francis alichaguliwa kufuatia kujiuzulu kwa Papa Benedict XVI.