Kalameni alivyopoteza jogoo watatu akibashiri ushindi wa Tanzania AFCON
NA MWANGI MUIRURI
KALAMENI kutoka Nyeri anajuta kwa kubashiri ushindi wa timu ya kandanda ya Tanzania katika dimba la Timu Bora Barani Afrika (Afcon) linaloendelea nchini Ivory Coast.
Jamaa huyo ambaye ni dalali wa kuku alijitoza kwenye mchezo huo wa pata potea na mwenzake katika bezi ya jaba (miraa), akiahidi kwamba angetoa jogoo watatu wenye thamani ya Sh4, 500 iwapo Tanzania ingeshindwa na Taifa la Morocco katika mtanange wa Januari 17, 2024.
Kwa upande wake, mwenzake alikuwa ameahidi kutoa kiasi sawa na hicho, Sh4,500, zikiwa pesa tasilimu iwapo Tanzania ingeshinda.
“Ogopa jaba. Kilichokuwa kimempa kalameni matumaini ya Tanzania kushinda mechi hiyo hakijulikani. Alikuwa tu akisema kati ya Morocco na Tanzania hakukuwa na ushindani kamwe. Hata alisema Tanzania ingeshinda kwa magoli 3 kwa 1,” akasema mdokezi.
Soma pia: https://taifaleo.nation.co.ke/makala/afcon-2019-kenya-ilivyopepeta-tanzania-3-2
Wakati mechi ilianza na Tanzania wakapigwa goli la kwanza kunako dakika ya 30, polo alisema kwamba hilo ndilo lilikuwa goli la kipekee la timu hiyo, akiambia mwenzake atulie sasa ashuhudie Tanzania ikifunga mabao matatu ya ubashiri wake.
Lakini mambo yalienda mrama wakati Tanzania ilipata kadi nyekundu katika dakika ya 70 na kubakia wachezaji 10 ugani.
Kipenga cha mwisho kilipata Tanzania ikiwa chini kwa magoli 3-0.
“Kamari ni kamari na jombi hakuwa na lingine ila tu kumwachia mwenzake jogoo hao watatu lakini akionekana kufedheheka sana. Hata alilia akisema kwamba timu hiyo – Tanzania inafaa kuvunjwa na iundwe upya,” akasema shahidi aliyekuwa hayo yakifanyika.
Kwa sasa, kalameni ameapa kwamba hatawahi kuingia katika kamari ya kuahidiana mali baada ya kuona jogoo wake watatu wakienda na mwingine pasipo hata kutoa hata kipande cha sigara kama malipo.