Makala

Kalonzo achumbia Gema kupiga jeki azma yake

Na BENSON MATHEKA August 19th, 2024 Kusoma ni dakika: 2

KIONGOZI wa Chama cha Wiper Kalonzo Musyoka ameanzisha mikakati ya kisiasa inayolenga kuunganisha ngome yake ya Ukambani na Mlima Kenya na ambayo hatimaye itaishia jamii ya Wakamba kujiunga na muungano wa Gema unaoleta pamoja jamii za Gikuyu, Embu, Meru.

Duru zinasema kuna uwezekano wa Bw Musyoka kuungana na Bw Gachagua katika uchaguzi mkuu ujao, hatua ambayo wadadisi wanasema inaweza kupiga jeki azma ya urais ya kiongozi huyo wa Wiper akiungwa na Gema.

Bw Musyoka anataka kutumia hali ya sasa ya malalamishi ya wakazi wengi wa eneo la Mlima Kenya dhidi ya Rais William Ruto kwa kushindwa kutimiza ahadi za kabla ya uchaguzi mkuu wa 2022 na tetesi za njama ya kumhujumu Naibu Rais Rigathi Gachagua ili kujipendekeza katika eneo hilo kabla ya Uchaguzi Mkuu wa 2027.

Makamu rais wa zamani ambaye anaongoza mrengo wa upinzani wa Azimio baada ya wanasiasa wanne wakuu kutoka chama cha ODM cha Bw Raila Odinga kuteuliwa kuwa Mawaziri katika utawala wa Ruto amezuru kaunti za Kiambu, Nyeri, Kirinyaga na Embu kama sehemu ya mikakati yake.

Seneta wa Kitui Enoch Wambua, mshirika wa karibu wa Bw Musyoka, aliambia Taifa Leo kwamba ajenda yao ni kuhakikisha eneo la Ukambani linamuunga mkono Bw Musyoka na kuunganisha eneo hilo na Gema.

“Hivi karibuni kutakuwa na sherehe kubwa ya kurudisha mto kwenye mkondo wake. Tumetenganishwa na kaka na dada zetu ili kudhulumiwa. Ni wakati wa kurejea na kudai nafasi yetu halali,” akasema Bw Wambua.”Tutapigana vita vyovyote kuhakikisha tunachukua nafasi yetu halali na kupata sehemu yetu ya haki ya rasilimali. Tumeanza kuungana na ndugu zetu kutoka mlimani na nchi itakuwa ikishuhudia mengi zaidi.”

Aliyekuwa Gavana wa Kiambu Ferdinand Waititu, ambaye amekuwa akihudhuria baadhi ya hafla za Bw Musyoka maeneo ya Mlima Kenya, alithibitisha kwamba kuna mipango ya kuifanya jamii ya Wakamba kuwa sehemu ya GEMA.

Alimtaja Bw Musyoka kuwa mwanasiasa aliye na rekodi safi, na kutoa mfano wa ukuaji wa uchumi wakati wa utawala wa Rais Mwai Kibaki, ambapo Bw Musyoka alihudumu kama Makamu wa Rais kati ya 2008 hadi 2013.

“Tunataka kuwa na GEMA ya zamani kwa kuwajumuisha Wakamba. Mpango wetu ni jamii kuwa na sauti moja kisiasa kabla ya uchaguzi ujao,” akasema Bw Waititu.

Naibu Rais alisema katika mahojiano na televisheni wiki jana kwamba Bw Musyoka hajadhulumu eneo hilo.

Pia amekuwa akishinikiza kujumuishwa kwa eneo la Ukambani kuwa sehemu ya GEMA.

Naibu Gavana wa Machakos Francis Mwangangi alimtaja Bw Musyoka kuwa kiongozi wa kitaifa ambaye ana mitandao ya kisiasa kote nchini.

Alisema mpango huo ni kuunganisha ngome yake huku akifufua upya mitandao yake ya zamani katika maeneo yote ya nchi, ikiwa ni pamoja na eneo Mlima Kenya lililo na wapiga kura wengi.

“Kama mgombea urais katika Uchaguzi Mkuu wa 2027, inabidi aunganishe ngome yake kwanza kabla ya kwenda kutafuta kuungwa mkono na maeneo mingine. Pia ameweka wazi kuwa atasimama na vijana, ambao wamelalamika kuhusu jinsi nchi inavyotawaliwa,” akasema Bw Mwangangi.