Makala

KAMAU: Binadamu ni mwepesi wa kusahau akifanikiwa

December 15th, 2020 Kusoma ni dakika: 2

Na WANDERI KAMAU

MWANADAMU ni kiumbe msahaulifu. Ni kiumbe ambaye husahau alikotoka pindi tu anapopata mamlaka, au anapopiga hatua fulani maishani inayompa jukumu la kuwaongoza ama kuwasimamia wenzake.

Pengine ni kutokana na sifa hiyo ambapo Mungu alikasirishwa naye na hatimaye kumfukuza kutoka Shamba la Edeni.

Usahaulifu ndilo kosa kuu lililozizamisha jamii, mashirika, nchi au hata falme zilizosifika awali.

Usahaulifu ndio uliwaangusha watawala maarufu kama Mfalme Sulemani, Mfalme Saulo, Juliasi Kaizari (aliyekuwa mtawala wa falme ya Roma) kati ya wengine.

Hilo ndilo pia limewapaka tope baadhi ya viongozi waliochukua mamlaka kwa ahadi za kuwakomboa watu wao kama Yoweri Museveni (Uganda), Paul Bbiya (Cameroon) na Donald Trump (Amerika).

Katika Biblia, Mfalme Sulemani alichukua uongozi wa Waisraeli kwa ahadi kuwa ndiye angemjengea Mungu hekalu baada ya babake, Mfalme Daudi, kushindwa kufanya hivyo.

Mungu alisema Mfalme Daudi hangefanya hivyo kwani alishiriki kwenye vita vingi, hali iliyomfanya kumwaga damu ya watu wengi.

Ingawa Mfalme Sulemani alifanikiwa kutimiza ahadi ya Mungu, utawala wake ulilaumiwa pakubwa kwa kutumia dhuluma dhidi ya raia.

Kutokana na usahaulifu, alikiuka maagizo yote aliyokuwa amepewa na Mungu, kwa mfano, kuhakikisha aliwaongoza Waisraeli kwa usawa na mapendeleo.

Nchini Uganda, moto wa kisiasa unaoendelea kuwaka kati ya Rais Museveni na barobaro Robert Kyagulanyi (maarufu kama Bobi Wine) unatokana na kosa la kiongozi huyo kusahau alikotoka.

Rais Museveni alichukua uongozi wa taifa hilo mnamo 1986 kupitia kwa vuguvugu la National Resistance Movement (NRM), kwa ahadi ya kuwakomboa Waganda dhidi ya changamoto za kisiasa na kiuchumi zilizokuwa zikiwakabili.

Baada ya kuleweshwa na mamlaka ya urais, Museveni amegeuka kuwa kama hayawani, kiumbe asiye na huruma hata kidogo.

Amekuwa akitumia kila mbinu kujaribu kuzima ndoto ya Wine kuwania urais kwenye uchaguzi mkuu uliopangiwa kufanyjka Januari.

Nchini Amerika, Rais Trump alisahau kutekeleza ahadi yake ya “kulikomboa tena” taifa hilo na kuanza kuwabagua Weusi na watu wengine ambao si wenyeji.

Utawala wake uliwataja kuwa “wageni” na kuanza sera kali kuwaagiza warudi makwao. Hii ni licha ya maelfu ya raia hao kuwa na vibali halisi vya kufanyia kazi, kusomea au hata kuwa raia wa taifa hilo.

Hilo ndilo lilikuwa mojawapo ya sababu zilizochangia kushindwa kwake.

Vivyo hivyo, mifano hiyo, kati ya mingine inapaswa kutufungua macho kuhusu athari za kusahau misingi iliyotuweka kwenye nafasi tulizo nazo maishani.

Mara nyingi, Mungu hutupa majukumu hayo ili kuendeleza uumbaji wake.

Ndivyo alivyomwambia Nuhu, alipomwokoa kutoka kwa mafuriko yaliyoikumba dunia yote.

Hivyo, vitendo vyetu daima vinapaswa kuendana na mkataba tuliobuni na Mungu alipotupa majukumu kuhudumu kwenye nyadhifa hizo.

Hilo linapaswa kuwa miongoni mwa maazimio yetu mapya tunapokaribia kuumaliza mwaka huu, ambao umekuwa wenye changamoto tele kwa kila mmoja kote duniani.

Kwa kuzingatia msingi huo, bila shaka tutaepuka baadhi ya adhabu ambazo huenda zikatuandama kwenye safari zetu maishani.

[email protected]