Makala

KAMAU: Kifo cha Dkt Mogusu kichochee Wakenya kushinikiza mageuzi

December 11th, 2020 Kusoma ni dakika: 2

Na WANDERI KAMAU

TANGU jadi mageuzi ya utawala katika nchi mbalimbali duniani yametokana na ukakamavu wa wanajamii kupinga dhuluma zinazoendeshwa dhidi yao na watawala husika.

Ni kutokana na juhudi hizo ambapo viongozi hubadili mienendo yao au kuondolewa mamlakani na mawimbi ya mageuzi.

Taswira hiyo ndiyo ilijitokeza nchini Amerika mnamo Mei, baada ya polisi Weupe kumuua kikatili Mwamerika Mweusi, George Floyd. Baada ya video iliyoonyesha ukatili huo kusambaa mitandaoni, mamilioni ya watu duniani kote waliamka na kuanza kukashifu utawala wa Rais Donald Trump kwa ukatili na maonevu yake dhidi ya raia Weusi.

Alipochukua uongozi 2016, Trump aliahidi “kurejesha ushawishi na ubabe wa Amerika” duniani. Kwa ahadi hiyo, Weupe nchini humo walimchagua kwa kishindo, baada ya mtangulizi wake, Barack Obama, kuonekana kuwapendelea Weusi, ikizingatiwa ni mwenye asili ya Kiafrika.

Kile ambacho kiligeuka kuwa mshtuko kwa wengi ni kwamba “ahadi” ya Trump ilikuwa kuwadhalilisha Weusi na watu wa rangi zingine ambao si wazaliwa halisi wa Amerika.

Akaanza kutekeleza sera kali na za kibaguzi; ambazo lengo lake kuu lilikuwa kupunguza idadi ya raia wenye asili ya kigeni nchini Amerika.

Kilichofichika katika harakati hizo ni kwamba utawala wa Trump ulikuwa tayari kutumia mbinu zote kuhakikisha “wageni” wameondoka Amerika na kurejea makwao.

Hata hivyo, kile serikali yake ilisahau ni kwamba dunia nzima ilikuwa ikitazama. Aliokuwa akidai “warejee makwao” walikuwa wakifuatilia vitendo vyake kwa kina.

Kichapo na ‘tiba’ kwa ukatili wa Trump zilidhihirika kwenye uchaguzi wa urais mnamo Novemba 3, ambapo alipigwa kumbo na mwaniaji wa chama cha Democratic, Joe Biden.

Biden, ambaye sasa ndiye rais mteule wa Amerika, ameahidi kulainisha na kufutilia mbali baadhi ya sera katili ambazo Trump alianzisha kwa kisingizio cha “kuikomboa Amerika.”

Urejeleo huu mrefu unafuatia ghadhabu ambayo imedhihirika nchini Kenya kufuatia kifo cha Dkt Stephen Mogusu, aliyefariki mapema wiki hii kutokana na makali ya virusi vya corona.

Inadaiwa Dkt Mogusu alifariki katika hali ngumu, kwani hangeweza kugharamia matibabu ambayo alihitaji kwa dharura ili kukabili makali hayo. Kinaya ni kuwa, marehemu aliaga dunia kwa kukosa huduma ambazo yeye mwenyewe alikuwa akitoa kwa Wakenya.

Kifo cha Dkt Mogusu kinadhihirisha kutojali kwa viongozi nchini, kwani baadhi waliungana na maelfu ya Wakenya kutoa rambirambi kwa familia ya marehemu ilhali wana uwezo wa kuhakikisha hospitali zetu nchini zina vifaa na huduma muhimu za matibabu alizohitaji.

Huu ni unafiki mtupu ikizingatiwa pia kwamba ni wao wamefeli kusuluhisha malalamishi na vilio vya madaktari na wahudumu wa afya. Tangu Machi, wametizama tu wahudumu hao wakifariki mmoja baada ya mwingine kutokana na corona. Je, tiba ya unafiki huu ni ipi?

Kama Waamerika, ni wakati kifo cha Dkt Mogusu kiwaunganishe Wakenya kumaliza hali hii ya kutojali kwa viongozi. Kifo chake kinafaa kuchochea ghadhabu aliyokumbana na kile cha Floyd, kiasi cha Rais Trump kuondolewa uongozini.

Kwa mujibu wa Kipengele 1 cha Katiba, wananchi ndio wenye nguvu. Amkeni kujikomboa!

[email protected]