KAMAU: Kilimo kingine kitawafaa waliotegemea majanichai na kahawa
Na WANDERI KAMAU
KABLA ya kuaga mnamo 1998, babu yangu, Mzee Maathai Ndegwa, alikuwa na mazoea ya kunisimulia jinsi kilimo cha kahawa na majanichai kilivyowafaa sana wakati wa ujana wao.
Tukiwa malishoni, mbali na hadithi kuhusu vita vya Maumau, babu alisifu sana mimea hiyo miwili, akisema kuwa ndiyo iliyowawezesha kuwalipia karo watoto wao bila matatizo yoyote.
“Kahawa na majani chai vilikuwa kama dhahabu. Hakuna aliyechezea kilimo chake hata kidogo. Wakulima wake walikuwa matajiri walioheshimika,” alisema babu.
Babu alifariki kwa imani hiyo hiyo kuwa mazao hayo ndiyo yaliyokuwa daraja la ukombozi kwa wakulima.
Hata hivyo, mimea iliyoonekana kama ‘dhahabu’ imebadilika kuwa kilio kwa wakulima wenyewe.
Wengine wameanza kuilaani. Wanaitaja kuwa ‘laana’ kutoka kwa miungu. Nashangaa ikiwa babu angekuwa na msimamo wake ikiwa angefufuka leo. Imani yangu ni kwamba angebadilisha msimamo wake mara moja.
Ni dhahiri kuwa enzi ambapo mimea hii ilionekana kama dhahabu imepita. Usimamizi mbaya umewafanya wakulima wengi kupoteza imani nayo.
Kijijini kwetu, tuliamini kwamba ilikuwa mwiko kuing’oa mimea hiyo. Tuliogopa kuidhuru kwa namna yoyote ile, kwani tuliamini kuwa miungu wangetugeukia kwa ghadhabu kuu.
Ni kilimo kilichoheshimika na kuenziwa sana. Nyakati ambazo zilifurahiwa sana ni msimu wa bonasi, kwani ni wakati huu ambapo watoto wangevalia mavazi mapya.
Nyakati hizo zilikuwa kama ‘Krismasi’ ya mapema vijijini. Watoto walifurahia. Wazee walisherehekea huku akina mama wakiimba nyimbo za kumshukuru Mungu kwa “kuwakumbuka.”
Ni wakati kama huu ambapo vyakula kama chapati vingepatikana vijijini kwani kila familia ingemudu kununua unga bila kukopa.
Hata hivyo, nyakati hizo zimeisha. Hazipo tena. Bonasi iliyoonekana kama Krismasi imegeuka chanzo cha vilio na manung’uniko.
Hali ya ghadhabu imefikia kiasi cha baadhi ya wakulima kujutia kupanda mimea hiyo.
Kiwango cha bonasi kimekuwa kikishuka tangu mwaka wa 2017. Wakulima wamekuwa wakipata malipo duni licha ya kutumia fedha nyingi kuitunza mimea hiyo.
Upeo wa ghadhabu hizo ni pale ambapo baadhi yao wamekaidi ‘miiko’ iliyokuwepo na kuanza kuing’oa!
Baadhi ya wakulima wanalaumu Halmashauri ya Usimamizi wa Majani Chai Kenya (KTDA) kwa masaibu yao.
Wakulima wa kahawa wanalaumu Bodi ya Kahawa Kenya (CBK) kwa kufuja fedha zao, huku wengine wakielekeza lawama zao kwa wakurugenzi wa viwanda mbalimbali vya mazao hayo.
Cha kushangaza ni kuwa, serikali ya Rais Uhuru Kenyatta inaonekana kutia masikio yake nta kuhusu vilio vya wakulima.
Ingawa Rais Kenyatta mwenyewe ametangaza mikakati kadhaa ya kufufua sekta hizo mbili, hali haijabadilika hata kidogo.
Wiki iliyopita, zaidi ya wabunge 20 kutoka ukanda wa Mlima Kenya, ambako mazao hayo yanakuzwa kwa wingi, waliandaa kikao katika Bunge, wakilalama kwamba serikali imewasahau wakulima hao.
Kimsingi, huu si wakati wa kulaumiana. Wakulima wanalia. Imefikia wakati wakulima wenyewe wanafaa kuanza kilimo cha mazao mbadala kwani vilio vyao vya muda mrefu vinaonekana kutomfikia yeyote.