Makala

KAMAU: Miguna, Makau wawe na mijadala pevu kiakademia

August 14th, 2020 Kusoma ni dakika: 2

Na WANDERI KAMAU

PROFESA Makau Mutua ni miongoni mwa wasomi ambao wamepata nafasi ya kukaa na kusomea ng’ambo.

Hivyo, ana ufahamu mkubwa wa masuala mbalimbali duniani na anawakilisha kundi kubwa la mamia ya wasomi kutoka Kenya ambao wamekuwa wakitoa michango mbalimbali nchini na katika mataifa wanamokaa kwa miaka mingi.

Hata hivyo, maswali yameibuka kuhusu michango halisi ya baadhi ya wasomi nchini, baada ya wengi kuonekana wakivutana baina yao kuhusu masuala mbalimbali yanayoiathiri jamii.

Mivutano hiyo imekuwa mikali kiasi kwamba, wengine hata wamezoea kurushiana cheche za matusi, bila kujali hisia za maelfu ya watu wanaowatazama.

Mfano halisi ni kati ya Profesa Mutua na wakili Miguna Miguna, anayeishi nchini Canada.

Wawili hao ni miongoni mwa watu walioondoka nchini zamani kwenda kukaa na kusomea ughaibuni.

Kutokana na tajriba zao pana kuhusu masuala muhimu kama siasa, sheria za kimataifa, mifumo ya kiutawala duniani, haki za binadamu kati ya mengine, wanaenziwa sana na wasomi chipukizi wanaolenga kufuata nyayo zao na kufikia walipo.

Licha ya hayo, inasikitisha sana wakati wawili hao wanapogeukiana na kuanza kutusiana mitandaoni kuhusu masuala ambayo yanapaswa kubuni midahalo pevu ya kuielimisha jamii.

Katika ulingo wa kiusomi, ni kawaida kwa wasomi ama wataalamu waliobobea katika masuala mbalimbali kutofautiana kimawazo. Kwa kawaida, mitazamo hiyo ndiyo huzaa mijadala muhimu, ambayo baadaye huchangia sana katika ukuaji wa jamii.

Ni mtindo ulioshuhudiwa katika miaka ya sitini, sabini na themanini katika ukanda wa Afrika Mashariki kati ya wasomi maarufu kama Ngugi wa Thiong’o na Taban Lo Liyong. Mfano halisi wa baadhi ya mijadala waliyozua katika miaka ya sitini ni uwezo wa Afrika Mashariki kuwa “chemichemi” ya uandishi wa kazi za fasihi.

Kwenye mojawapo ya kauli zake maarufu sana, Liyong alilitaja eneo hili kuwa “jangwa kifasihi.” Waandishi kama Ngugi walimjibu kwa kulitaja eneo kama “mtoto ambaye alikuwa anakua kifasihi”, hivyo halingelinganishwa na maeneo mengine kama Ulaya, Amerika ama Uarabuni, kwani yalipata uhuru wake karne nyingi zilizopita.

Mdahalo huu ndio unatajwa kuchangia waandishi wengi kujituma kuandika kazi nyingi ili kudhihirisha kauli ya Liyong kutokuwa ya kweli. Vile vile, ndio unatajwa kuchangia kuchipuka kwa kundi la wasomi wa “kukosoa ama kuhakiki” mawazo ya wasomi wenzao katika mawanda ya historia, fasihi, falsafa, uanahabari kati ya mengine.

Bila shaka, mielekeo hii miwili inaashiria kuwa mijadala na mitazamo tofauti kati ya wasomi wanaotazamwa na maelfu ya watu yana athari kubwa katika mwelekeo wa kijamii.

Hivyo, wasomi kama Prof Makau na Dkt Miguna wanafaa kutumia majukwaa waliyo nayo kuendeleza mijadala itakayoathiri mielekeo itakayochangia maendeleo na ustawi wa nchi.

Ni muhimu wakumbuke kuwa mawazo yao yatarejelewa na vizazi vijavyo ili kuvipa mwanga kuihusu jamii.