KAMAU: Ngugi akuze walezi wa utamaduni wa Kiafrika
Na WANDERI KAMAU
KATIKA kila kampeni au mchakato wowote, lazima kuwe na kinara pamoja na naibu wake.
Hatua hiyo inalenga kuhakikisha shughuli hiyo itaendelea kama kawaida, endapo kiongozi husika hatakuwepo au labda akumbwe na tatizo fulani.
Ili kuhakikisha hakuna pengo linalotokea, huwa ni jukumu kuu la viongozi waliopo kuwakuza watu wanaowaamini wataendelea kuwa manahodha bora kwa mchakato huo.
Hata hivyo, inasikitisha wakati kiongozi anakosa mtu ama watu wa kutosha kuendeleza shughuli hiyo, hata ikiwa manufaa yake ni makubwa kwa jamii.
Mlinganisho huu unaakisi juhudi za msomi Ngugi wa Thiong’o kuendelea kupigania ukumbatiaji wa matumizi ya lugha asili za Kiafrika katika majukwaa tofauti duniani.
Licha ya kuendeleza harakati hizo tangu miaka ya themanini alipoacha kuandika vitabu vyake kwa lugha ya Kiingereza, Ngugi ameibuka kuwa jenerali anayeongoza jeshi ambalo halijajihami vizuri.
Alhamisi iliyopita, Ngugi alitunukiwa Tuzo ya Fasihi ya Kimataifa ya Catalonia nchini Uhispania, kwa mchango mkubwa ambao ametoa kuhamasisha jamii kukumbatia matumizi ya lugha asili.
Kwenye hafla hiyo, aliwachangamsha wengi alipoamua kutoa hotuba ya shukrani kwa lugha asili ya Gikuyu.
Washiriki walilazimika kutegemea wafasiri kuwafafanulia kauli za msomi huyo.
Licha ya ushindi huo, wasiwasi wangu ni kuwa, kizazi cha sasa bado hakijakumbatia harakati za Ngugi vyema na wanaharakati wengine wachache ambao wamejitokeza kupigia debe lugha za Kiafrika.
Kimsingi, Ngugi si mtu wa kwanza kusisitiza umuhimu wa Afrika kukumbatia tamaduni zake.
Aliyekuwa rais wa DR Congo, Mobutu Sese Seko, alichukua mkondo uo huo alipolitawala taifa hilo kati ya 1965 na 1997.
Kwenye utawala wake, Mobutu alisisitiza kuwa njia ya pekee kwa Waafrika kudumisha utamaduni wao ni kuacha kutumia majina ya Kiingereza, Kifaransa, Kireno au Kihispaniola kujitambulisha.
Kama hatua ya kuonyesha mfano wake, Mobutu alibadilisha jina la taifa hilo kuwa Zaire kutoka DR Congo.
Ni katika enzi ya utawala wake ambapo muziki aina ya Lingala ulivuma Afrika kote na kushabikiwa na mataifa mengine, Kenya ikiwepo.
Ni kutokana na juhudi za Mobutu pia ambapo wanamuziki maarufu kama Franco Luambo Makiadi walichipuka na kujizolea ufuasi mkubwa barani na duniani kote.
Miaka 23 baada ya kifo chake, juhudi zake zinaonekana kujikita tu kwenye tasnia ya muziki.
Kama jamii yoyote ile, taifa hilo linaendelea kushuhudia mabadiliko makubwa kwenye mfumo wa maisha kutokana na mwingilio wa kiteknolojia duniani.
Nchini Kenya, Mzee Jomo Kenyatta na mwanasiasa Jaramogi Oginga Odinga ni miongoni mwa viongozi ambao pia watakumbukwa kuonyesha juhudi hizo.
Hata hivyo, kosa kuu walilofanya ni kutoendeleza juhudi hizo kwa kuwalea viongozi ambao wange rithi mipangilio yao.
Bila shaka, hilo linahatarisha mustakabali wa tamaduni za Kiafrika ikiwa hakutakuwepo na juhudi za kuwakuza ‘mabalozi’ wake katika kizazi cha sasa.
Hilo ndilo jukumu kuu analopaswa kufanya Ngugi na wanaharakati wachache waliobaki.