KAMAU: Ni kosa kutowatambua mashujaa wetu nchini
Na WANDERI KAMAU
MKASA wowote katika nchi ama jamii yoyote ile ni kuwasahau mashujaa wake.
Kosa hilo huwa kama mtoto anayemsahau mzazi wake, licha ya juhudi alizoweka katika ulezi wake.
Hilo pia huwa kama kuisahau na kuitupialia mbali historia yake.
La kushangaza ni kuwa, licha ya historia kuwa muhimu katika uwepo wa mataifa mbalimbali duniani kote, inasikitisha vizazi vilivyopo havitilii maanani michango iliyotolewa na waanzilishi wa mataifa hayo.
Hivyo, hata katika uhai wao si wengi wanaojali maslahi yao; wanavyoishi ama hata matamanio yao wanapokaribia siku zao za mwisho hapa duniani.
Hilo ndilo lililodhihirika wiki iliyopita baada ya jamaa wawili wa karibu wa mashujaa walio tetea watu maskini nchini, kufariki bila utambuzi wowote maalum kutoka kwa serikali.
Wala hawakutambuliwa na idara zinasosimamia taratibu za kuwatambua na kuwaheshimu watu waliotoa michango mbalimbali katika ustawi wa nchi.
Nazungumzia mkewe mwanaharakati Pio Gama Pinto, Bi Emma Pinto, na mwanawe mwanasiasa maarufu, JM Kariuki, Bw Tony Kariuki.
Bi Pinto alifariki nchini Canada Jumatano iliyopita akiwa na umri wa miaka 92. Naye Bw Kariuki alifariki Jumapili, ila familia yake haikutoa sababu maalum iliyosababisha kifo chake.
Bila shaka, vifo vya wawili hao vinaonyesha kuwa bado tunaendeleza mwenendo wa kutowatambua mashujaa waliojituma katika harakati za ukombozi nchini.
Kwa mfano, Bi Pinto amekuwa akiishi uhamishoni nchini Canada kwa muda mrefu, mara tu baada ya mumewe kuuawa kikatili mnamo Februari 1965.
Pinto alipigwa risasi na vikosi vya usalama sababu ya kuikosoa serikali ya Mzee Jomo Kenyatta kwa tuhuma za kuwatenga baadhi ya watu walioshiriki vita vya ukombozi.
Pinto pia alikuwa katika mstari wa mbele kutetea haki za Wahindi dhidi ya maonevu kutoka kwa serikali ya Mzee Kenyatta.
Baada ya unyama huo, ilibidi mkewe na familia watorokee ughaibuni kusudi wasifikiwe na ukatili wa serikali kama alivyofanyiwa mumewe.
Marehemu JM naye alifariki katika hali kama hiyo baada ya kuonekana kupata umaarufu mkubwa miongoni mwa Wakenya kutokana na harakati zake za kutetea maskini.
Aliuawa katika mazingira tatanishi huku mwili wake ukitupwa katika msitu wa Ngong, Kaunti ya Kajiado. Ulipatikana Machi 1975 ukiwa katika hali mbaya na mchungaji mmoja wa Kimaasai.
Bila shaka, kando na wanasiasa walioshiriki harakati za Ukombozi wa Pili miaka ya tisini, hawa ni mashujaa ambao daima wanapaswa kukumbukwa kwa harakati zao za kutetea maskini bila kuogopa vitisho vya serikali.
Kama marehemu Mahatma Gandhi, utetezi wao ulikuwa wa amani wala hawakutumia ghasia ama uchochezi.
Kama kumbukumbu na heshima kwa michango waliyotoa, ni muhimu kwa idara husika serikalini kutambua jamaa zao.
Hili litahakikisha tunaendelea kukuza na kuhifadhi historia yetu bila kupendelea baadhi ya watu na kusahau wengine. Hili pia lilatoa mwanga kamili wa kihistoria kwa vizazi vijavyo.