KAMAU: Ni wakati wa kukumbuka walimu wa chekechea
Na WANDERI KAMAU
MMOJA wa watu muhimu sana kwenye maisha ya kila mwanadamu ni mwalimu wa shule ya chekechea.
Mara nyingi, mwalimu huyo huwa kama mzazi wa pili kwenye ulezi wa mtoto.
Hili ni kwa kuwa baada ya mtoto kutoka mikononi mwa mzazi wake halisi anapoenda shuleni, yeye hushinda karibu kutwa nzima na mwalimu wake.
Wakati mwingine, baadhi ya watoto hupelekwa shuleni wakiwa wachanga sana kiasi kwamba, huwa hawajui kuzungumza ama kutamka baadhi ya matamshi.
Ni mwalimu wa chekechea huhakikisha wamefahamu kuyatamka maneno vizuri na hata wanajua kuandika kwa njia ifaayo.
Bila shaka, hili ni jukumu muhimu ambapo licha ya kuwa ni kazi kama zile zingine, lina mchango mkubwa kwenye maisha ya baadaye ya mtoto husika.
Walimu hao ni kama wazazi wetu, kwani kando na masomo, walitufunza nyimbo na maadili tunayopasa kuzingatia tunapoishi na kutangamana na watu kwenye maisha yetu ya kila siku.
Licha ya mchango huo wote, cha kusikitisha ni kuwa ni kama jamii imewasahau, hasa wakati huu wa janga la virusi vya corona.
Tangu kuzuka kwa janga hilo mnamo Machi, semi za wadau wengi wa elimu zimekuwa tu zikiangazia maslahi ya walimu wa shule za wamiliki binafsi na wale walioajiriwa na Bodi Simamizi za Shule (BOM) bila kutaja lolote linalohusu walimu wa chekechea.
Huu ni ubaguzi wa wazi na ishara ya kutokuwepo kwa watu wasio shukrani hata kidogo kwa walezi wao.
Ni dhahiri walimu wengi wa chekechea ni watu walio na familia zao zinazowategemea kwa mahitaji yao ya kila siku.
Wao ni wazazi walio na majukumu sawa na watu wengine katika jamii.
Ikizingatiwa masomo ya chekechea yamekuwa yakisimamiwa na serikali za kaunti tangu mfumo wa ugatuzi ulipoanza 2013, imefikia wakati kaunti zijitokeze wazi kueleza mikakati zilizoweka kuhakikisha walimu hao hawaathiriwi na makali ya janga hili.
Hili linafaa kwani kinyume na walimu kwenye vitengo vingine, wengi wao hawana wawakilishi maalum ama vyama vinavyoweza kutetea maslahi yao.
Binafsi, nilisomea vijijini utotoni mwangu ambapo kama kila mmoja, niliona namna walimu hao walijitolea kwenye kazi yao.
Huwa wanajituma sana kwa kuwachukulia watoto wanaowafunza kama wanao halisi.
Hivyo, kama ishara ya shukrani kwa mchango muhimu wanaotoa kwenye ulezi wa watoto, imefikia wakati tuwakumbuke.
Wao ni kama daraja kuu lililowavusha wengi wetu kutoka utotoni hadi ukubwani; na daraja ambalo bado linaendelea kutumika na makumi ya vizazi kuweka misingi ifaayo maishani mwao.
Lazima Kenya iziige nchi kama Amerika, Japan ama Denmark, ambapo walimu hao hulipwa mishahara mikubwa na kuheshimiwa pakubwa na jamii kutokana na michango wanayotoa.
Miongoni mwa jamii za Kiafrika, ilikuwa mwiko kuwasahau walezi wako. Katika baadhi ya jamii hizo, ilikuwa hatia kubwa kwa miungu, kwani walioikiuka waliadhibiwa vikali kwa kuandamwa na msururu wa mikosi. Tuwakumbuke walimu hawa. Ni walezi wetu.