KAMAU: Serikali ishughulikie masaibu ya mwanahabari Yassin Juma
Na WANDERI KAMAU
SERIKALI yoyote ile duniani ina jukumu la kulinda mali na maisha ya raia wake.
Hili ni jukumu ambalo limekuwepo tangu mfumo wa utawala ulipokumbatwa duniani karne nyingi zilizopita.
Uwezo wa kiongozi katika tawala au falme hizo ungejulikana kutokana na juhudi alizoweka kulinda maslahi ya raia wake dhidi ya tishio lolote—iwe ndani ama nje ya himaya yao.
Uvamizi wa nchi husika ndio ulizua hali ya vita, kwani watawala walichukuliwa kama ‘miungu’ walioonekana kuwa na uwezo mkubwa wa kisiasa na kijeshi na watu waliowaongoza.
Hali imekuwa hivyo hadi leo, ambapo licha ya dunia kuongozwa kwa misingi ya sheria za kisasa, serikali zilizopo bado zinatilia maanani sana usalama wa raia wao.
Hata hivyo, cha kushangaza ni kuwa, serikali ya Kenya imekuwa ikilaumiwa kwa kuwatelekeza raia wake, hasa wale wanaoonekana kuwa wa hadhi ya chini.
Miongoni mwa wale wanaoteseka kwa sasa kutokana na hali ya kutojali kwa serikali ni mwanahabari Mkenya, Yassin Juma, anayeendelea kuzuiliwa nchini Ethiopia kwa tuhuma za “uchochezi.”
Bw Juma alikamatwa mapema mwezi uliopita na vikosi vya usalama vya Ethiopia, alipokuwa akiangazia maandamano yaliyotokea nchini humo kutokana na mauaji ya mwanamuziki maarufu, Hachalu Hundessa.
Ripoti zilisema Juma alikamatwa kwa madai ya “kushirikiana na upinzani kupanga njama za kuisambaratisha serikali.”
Hadi sasa, amefikishwa mahakamani mara tatu, lakini kesi yake bado haijaanza kwa kukosa wakili pamoja na changamoto za mawasiliano.
Vikao vingi vya mahakama katika taifa hilo huendeshwa kwa lugha ya Amhara.
Kwa wakati huu wote ambapo amekuwa mikononi mwa vikosi ya Ethiopia, kinachofadhaisha zaidi ni kimya cha serikali ya Kenya kuhusu masaibu ya mojawapo ya raia wake katika nchi ya kigeni.
Juma ni mwanahabari huru na anayejulikana sana eneo zima la Afrika Mashariki. Amekuwa akiangazia habari za kikanda ambazo hata hupeperushwa na mashirika ya habari ya kimataifa.
Wakati umefika kwa serikali ya Kenya kukoma kufumbia macho mateso anayopitia mmoja wa raia wake katika nchi ya kigeni.
Ubalozi wa Kenya nchini humo unapaswa kuwajibika kwa kumsaidia Juma kupata wakili, ili kumwezesha kujitetea kwa misingi ya sheria za nchi hiyo.
Hili huenda likawa hatua ya kwanza kuonyesha serikali inajali maslahi ya raia wake.