• Nairobi
  • Last Updated May 8th, 2024 8:55 PM
KAMAU: Trump anairejesha dunia enzi za giza

KAMAU: Trump anairejesha dunia enzi za giza

Na WANDERI KAMAU

SI siri tena kwamba dunia inaelekea katika nyakati hatari; nyakati za mizozo ya kisiasa ambayo inahatarisha mustakabali wake.

Tangu alipochukua uongozi mnamo 2016, Rais Donald Trump wa Amerika alishinda kwa kaulimbiu ya “Kurejesha hadhi ya Amerika tena.”

Baada ya kuanza kuhudumu kama rais, Bw Trump alianza kutangaza vitisho vikali dhidi ya Waamerika Weusi wanaoishi nchini humo, akisema kuwa wengi wao waliingia humo kama wakimbizi haramu.

Alianza sera kali ya kuwarejesha makwao watu hao, akiwataja kuwa “tishio” kwa usalama wa Amerika.

Bw Trump pia alitangaza mkakati wa kujenga ukuta mkubwa kwenye mpaka kati ya Amerika na Mexico, akisisitiza kuwa lengo kuu ni kuimarisha usalama wa raia wa Amerika.

Haya yote yaliwiana na ahadi ya kurejesha hadhi ya Amerika.

Hata hivyo, nyakati za hatari zimeanza kujitokeza wazi baada ya kudhihirika wazi kuwa nia ya Trump na washirika wake ni kuirejesha dunia chini ya udhibiti wa Wazungu.

Ni wazi kuwa Trump hayuko pekee kwenye mkakati huo, ila ana uungawji mkono wa viongozi kama Boris Johnson wa Uingereza na kiongozi wa Upinzani nchini Ufaransa Marie Le Pen.

Kwenye hotuba kadhaa ambazo wametoa, wawili hao wamesema kuwa wanatamani hali ambapo “dunia itakuwa chini ya udhibiti wa Wazungu.”

Aliyekuwa mshirika wa karibu wa Trump, Bw Steve Bannon, pia amenukuliwa akisema kuwa nia kamili ya Trump si kurejesha hadhi ya Amerika tena tu, bali hata washirika wake.

Wachanganuzi wa kisiasa wanasema kuwa mkakati huo ndio umechangia nchi kama Uingereza kutangaza kujiondoa kutoka Muungano wa Ulaya (EU) ili kuwianisha mikakati yake na ile ya Trump.

Kilicho wazi ni kuwa kwa mkakati huu, viongozi kama Trump na Johnson wanairejesha dunia katika miaka ya 1930, walipoibuka viongozi kama Adolf Hitler (Ujerumani) na Benitto Musollini (Italia).

Kwa kutumia msimamo wao mkali na ushawishi mkubwa waliokua nao, wawili hao walieneza propaganda kali dhidi ya Wayahudi kuhusu vile “walikuwa tishio kwa usalama wa dunia.”

Walianza mikakati ya “kuwaondoa” Wayahudi katika mataifa yao, wakitumia wanajeshi kuwaua.

Wayahudi waliokuwa sehemu mbalimbali duniani walijikuta kama adui wa kila mtu. Waliuawa na kudhulumiwa popote walipokuwa. Hiyo ndiyo ilikuwa mojawapo ya sababu kuu zilizosababisha Vita Vikuu vya Pili vya Dunia kutokea baina ya 1939 na 1945.

Vivyo hivyo, mkakati wa Trump si tofauti, kwani lengo lake ni kupata uungwaji mkono wa viongozi Wazungu watakaomuunga mkono.

Ili kuonyesha “ubabe” wake, inaelezwa kuwa hiyo ndiyo sababu ambapo yeye na viongozi wengine wanaomuunga mkono wamekuwa wakitumia mtandao wa Twitter kueleza misimamo yao mikali ili kuzua hofu duniani.

Na ikiwa ni dhahiri kuwa Waafrika na Weusi ndiyo walengwa wakuu kwenye mkakati huo, funzo ni kwamba lazima wawe macho wanaposafiri nchi kama Amerika kutafuta makao ya kudumu.

[email protected]

You can share this post!

Gurudumu la ndege ya Silverstone Air ladondoka ikiwa imepaa

OBARA: Serikali ifunge madhehebu yanayoletea waumini maafa

adminleo