• Nairobi
  • Last Updated May 9th, 2024 6:40 PM
KAMAU: Tumejitia utumwani kwa kuasi mila na desturi zetu

KAMAU: Tumejitia utumwani kwa kuasi mila na desturi zetu

Na WANDERI KAMAU

HATUA ya klabu ya kandanda ya AS Roma kutoka Italia kufungua akaunti ya mtandao wa Twitter kwa lugha ya Kiswahili imeonyesha jinsi lugha hiyo inavyozidi kukua.

Hilo pia linaashiria jinsi tamaduni za Afrika zilivyo na thamani na uzito mkubwa sana kwa jamii mbalimbali duniani.

Kinaya ni kuwa, utambuzi huo wa Kiswahili unajiri wakati ambapo Waafrika wenyewe wameendelea kudunisha tamaduni zao, badala yake wakiabudu mielekeo ya kimaisha ya nchi za Magharibi.

Baadhi ya miigo hiyo ni kudunisha Kiswahili na lugha asili za Afrika, wakiabudu Kiingereza na lugha nyingine kama Kijerumani, Kihispania, Kichina kati ya nyingine ili kuonekana kuwa “wasomi”.

Kabla ya kuja Afrika kuanza kutawala jamii zilizokuwepo, hatua ya kwanza ya nchi za Ulaya ilikuwa kuwatuma wamishenari kusambaza dini ya Kikristo na lugha zao.

Walipofika humu mwishoni mwa karne ya 19, wamishenari hao walianza kwa kubuni makanisa mbalimbali yenye vituo vya kuwafunzia Waafrika lugha kama vile Kiingereza ili kuwawezesha “kusambaza dini ya Kikristo” kati ya nyinginezo.

Cha kushangaza ni kwamba ujio wa wamishenari haukumaanisha kuwa Waafrika wenyewe hawakuwa na dini zao asilia. La hasha!

Licha ya kutokuwa na ufahamu mkubwa wa masuala kama teknolojia, Waafrika walikuwa jamii yenye misingi ya kimaadili.

Walikuwa na miungu wao. Walikuwa na dini zao asilia. Walikuwa na tamaduni zao walizodumisha na kuzizingatia katika kila hatua ya maisha yao.

Hivyo, ujio wa wamishenari haukubadilisha umuhimu wa tamaduni hizo miongoni mwa Waafrika.

Hata hivyo, kosa kuu lilianza kudhihirika wakati wale waliobadili dini zao na kuwa Wakristo ama Waislamu walipowageukia vikali wale waliokwamilia Uafrika.

Pengine walipofushwa na kasumba za Kizungu kwamba tamaduni za Kiafrika zilikuwa za ‘kishetani.’

Kutokana na “imani” yao kubwa, walizibandika tamaduni za dini asili za Kiafrika kuwa “potovu na zisizozingatia uadilifu hata kidogo.”

Hapo ndipo utumwa wa kitamaduni miongoni mwa Waafrika wenyewe ulipoanza.

Watu waanza kukumbatia mafundisho ya Wazungu

Kizazi baada ya kizazi kilianza kukumbatia mafundisho ya Wazungu na kukubali kuwa miungu mbalimbali walioabudiwa na jamii za Kiafrika walifanana na shetani.

Utumwa huo umekuwa janga kuu kwa sasa. Kwa mantiki ya ‘uhalisia’ huo, azungumzaye lugha asili kama Gikuyu, Dholuo, Kiturkana ama Kiswahili ni ‘mjinga’ naye anayefahamu kuzungumza lugha za kigeni kama Kiingereza akiwa ‘msomi’.

Kinaya ni kuwa, nchi kama Japan, China, Ujerumani kati ya mataifa mengine ambayo ni kama ‘tunayaabudu’, lugha zao huwa zinatumia lugha zao asili kwenye mawasiliano yao!

Kinaya kingine ni kuwa, Wazungu wenyewe wameona thamani kuu ya Uafrika na kuanza kukumbatia lugha asili kama Kiswahili.

Kiswahili kinafunzwa katika vyuo vingi vikuu vya Ulaya. Mataifa hayo pia yameanza vituo vya redio vinavyopeperusha matangazo yao kwa Kiswahili.

Kijumla, Kiswahili ni sehemu ya utamaduni wa Kiafrika. Lazima Waafrika wafunguke macho na kutambua kuwa wanajitia utumwani kwa kupuuza tamaduni zao. Lazima tuzinduke!

 

[email protected]

You can share this post!

Mwanafunzi atoweka shuleni mara baada ya umeme kupotea

Wabunge wamkejeli Ruto kwa kuhujumu BBI

adminleo