Makala

KAMAU: Tuombe radhi wafu wa corona

September 11th, 2020 Kusoma ni dakika: 2

Na WANDERI KAMAU

MOJAWAPO ya mambo muhimu katika maisha ya kila mwanadamu duniani ni kuagwa kwa njia ya heshima na jamaa, marafiki na jamii nzima kwa jumla.

Kifo huwa ni awamu ya mwisho kwa wafiwa kumwona mpendwa wao.

Hivyo, ni hafla ambayo huandamwa na majonzi mengi kwa wale walioachwa.

Duniani kote, jumbe zote ambazo hutolewa kwenye mazishi ya mfu-awe mzuri ama mbaya-huwa ni za kuifariji na kuiliwaza jamii.

Sababu kuu ni kwamba, mwanadamu ni kiumbe maalumu na mwenye utofauti mkubwa kimaumbile na viumbe wengine.

Alipomaliza uumbaji wake, Mungu alimpa mwanadamu uwezo na mamlaka kuwasimamia wanyama na mimea yote kote duniani.

Kauli hiyo ndiyo inamweka mwanadamu kwenye nafasi maalumu kama kiumbe anayestahili hekima kutoka kuzaliwa hadi siku yake ya mauti.

Hata hivyo, kinachoshtua ni kwamba, licha ya kuthaminiwa sana na Mungu kwa kupewa usimamizi wa uumba wake, mwanadamu amejigeuza kuwa kiumbe duni, asiyejali na mwenye tamaa.

Tamaa yake imekuwa kubwa kiasi hata cha kutojali athari za baadhi ya vitendo vyake kwa wanadamu wenzake.

Mfano bora zaidi ni tangazo la Wizara ya Afya, mnamo Jumatatu, kwamba maiti za watu waliofariki kutokana na virusi vya corona haziwezi kuvisambaza hata kwa wale wanaozishughulikia. Ni tangazo lililowapata wengi kwa mshangao. Sababu ni kuwa, tangu virusi hivyo kugunduliwa nchini mnamo Machi, wale wanaohofiwa kufariki kutokana navyo wamekuwa wakizikwa kama wanyama.

Tangu Machi, hafla za mazishi zimegeuka kuwa chemichemi kuu za majonzi na mahangaiko ya kimawazo kwa kila mmoja anayehudhuria.

Taswira ambazo tumekuwa tukishuhudia hazikuwepo hata kwa wale waliouawa kwa kushukiwa kuwa wahalifu enzi za mababu zetu. Walizikwa kwa heshima.

Mababu zetu walitambua thamani ya maisha ya mwanadamu.

Wale waliodhaniwa kufariki kutokana na corona wamekuwa wakizikwa na watu wachache waliovalia magwanda ya kutisha.

Kwenye kanuni kali zilizotolewa na Serikali kuhusu hafla za mazishi, ni watu 15 pekee ambao wamekuwa wakiruhusiwa kumzika aliyeaga.

Katika baadhi ya matukio, familia za marehemu hata zimenyimwa nafasi kuwatazama wapendwa wao! Sababu kuu? Hatari ya kuambukizwa corona!

Bila shaka, imebainika wazi kuwa, huenda hii ilikuwa tu sarakasi iliyobuniwa kimakusudi na baadhi ya watu wenye ushawishi serikalini kuwapa nafasi kupora fedha zilizotolewa kuisaidia Kenya kukabili janga hilo.

Maswali yaliyopo ni je, ni baada ya miezi hiyo yote ambapo Wizara ilibaini maiti haziwezi kusambaza corona? Mbona tangazo hilo limetolewa tu baada ya kashfa kuhusu uporaji wa fedha za kukabili virusi kufichuka? Ilikuwa njama ya makusudi kuwapumbaza Wakenya?

Haya ni maswali mazito yanayohitaji majibu kutoka kwa wale wote ambao wametajwa kuhusika kwenye sakata hiyo.

Kwa marehemu wote waliozikwa kama wanyama, deni lao kubwa tulilo nalo sisi tulio hai ni kuwaomba msamaha kwa kuwakosea hekima. Twaomba msamehe nafsi zetu kwa udhalimu tuliowatendea. Amin.

[email protected]