Makala

KAMAU: Tutathmini upya suala la urithi kuzuia mizozo

November 20th, 2020 Kusoma ni dakika: 2

Na WANDERI KAMAU

TANGU dunia ilipoumbwa, hakuna anayefahamu kuhusu asili kuu ya kifo miongoni mwa wanadamu.

Kifo kimebaki kuwa tukio la siri ambalo haijawahi kuvumbuliwa na yeyote. Si madaktari, wanasayansi, wahahistoria au wasomi wa kiwango chochote kile. Ni tukio lisiloeleweka hadi sasa.

Kuna wale wasemao kwamba mwanadamu anapofariki “roho yake humrudia Mungu.”

Hilo ndilo pia funzo la madhehebu tofauti ya kidini. Ndilo funzo la msingi kwa kila mtoto anayeanza kufahamu kuhusu uhalisia wa maisha hapa duniani.

Zamani, wazee katika jamii za Kiafrika walishikilia kwamba ni lazima mtu, hasa mzee, ajitayarishe anapofahamu kuwa siku za maisha yake hapa duniani zinakaribia kufikia kikomo.

Ingawa ni kauli ya kutamausha, hilo lilikuwa kuepuka mtindo wa mizozo isiyofaa k miongoni mwa jamaa za mzee husika kuhusu urithi wa mali yake. Hii ni ikizingatiwa kuwa wazee wengi nyakati hizo walikuwa wakiwaoa wanawake wengi.

Hadi sasa, ni mwiko katika jamii nyingi kuzungumza kuhusu kifo. Ni vibaya zaidi kutoa kauli kwamba “mtu anapaswa kujitayarisha” kwani zinaamini Mungu pekee ndiye ajuaye hatima ya maisha ya mwanadamu hapa duniani.

Lakini maswali yanaibuka: Ni muhimu kwa wanajamii kujitayarisha wanapofahamu wanakaribia kuondoka duniani? Kuna umuhimu wowote? Licha yetu kukumbatia usasa na mafunzo ya kidini, mbona mtu ajiandae kwa safari hii isiyojulikana?

Kimsingi, hayo ni maswali mazito. Ni maswali ambayo huenda yakazua hisia, msisimko na kumbukumbu chungu nzima miongoni mwa wanajamii. Hata hivyo, nahisi yanapaswa kutiliwa mkazo, hasa kutokana na mizozo ambayo tumekuwa tukishuhudia kuhusu urithi wa mali za marehemu.

Kwa mujibu wa imani za Kiafrika, anayefariki anapaswa kuwaunganisha jamaa zake. Kwa kawaida, jamaa hao huungana ili kumuaga mwenzao kwa hekima kutokana na maisha aliyoishi hapa duniani.

Hata hivyo, imekuwa kinaya katika familia nyingi kuwa badala ya kuungana, kifo cha mmoja wao huwa mwanzo wa mafarakano na mivutano isiyoisha. Mizozo hiyo mara nyingi huhusisha taratibu za urithi wa mali inayoachwa na wazee wao.

Jamaa hao huchukiana, hupelekana mahakamani au hata huuana. Wenye nguvu hata huwatumia mawakili kuwashtaki wenzao ili ‘kuwapa funzo.’

Tumeshuhudia mivutano ya mali za watu waliokuwa matajiri ikijikokota mahakamani kwa muda wa hata zaidi ya miaka kumi.

Kinaya ni kwamba, wale hufurahia sana mizozo hiyo inapokuwepo huwa ni mawakili, kwani ndio huhusika pakubwa katika “kuwatetea” wateja wao.

Kwenye taswira ya kutamausha inayohusisha mvutano wa mali ya mwanasiasa maarufu, ililipotiwa baadhi ya jamaa zake wanaishi katika hali za kimaskini.

Katika kisa cha kutamausha, iliibuka jamaa yao mmoja alizikwa katika nchi ya kigeni baada ya familia hiyo kukosa ada ya kusafirisha mwili wake Kenya ili kuuzika. Hili ni sikitiko kuu!

Ni imani yangu kuwa hata akiwa kwenye wafu, si furaha ya mwanasiasa husika kuwaona wanawe wakiteseka kiasi hicho.

Hii ndiyo sababu ambapo ni lazima turejelee taratibu za awali kuhusu kifo ili kuepuka matukio kama haya. Hayafai hata kidogo!

[email protected]