KAMAU: Uhuru aeleze nchi ukweli kuhusu hali ya uchumi
Na WANDERI KAMAU
MOJAWAPO ya jukumu kuu la Serikali ni kuwaeleza wananchi ukweli kuhusu hali ilivyo katika nchi yao.
Huu ndio umekuwa mtindo kwa karne nyingi tangu mfumo wa uongozi na utawala ulipoanza kuwepo duniani.
Kimsingi, Serikali huwa kama “mlinzi” au “baba” wa wananchi husika, hivyo huwa wanaitegemea kuwaeleza uhalisia uliopo kuhusu nyanja zote nchini mwao.
Nchini Amerika, miongoni mwa majukumu muhimu ambayo Serikali hutakiwa kuwatimizia wananchi ni kuwaeleza ukweli kuhusu mwelekeo wa taifa katika sekta zote–uwe wa kuridhisha ama kutoridhisha.
Ingawa Rais anapewa mamlaka ya kikatiba kuchukua baadhi ya hatua, huwa ni lazima kwake kulieleza Bunge kuhusu sababu za kuchukua mwelekeo huo.
Mtindo huo huhakikisha kuwa kiongozi yeyote anayechukua mamlaka nchini humo, anawajibika kuhusu kila kitendo anachokifanya.
Hilo vile vile hujenga imani kati ya raia na watawala wao; kwamba uendeshaji wa nchi si jukumu la mtu mmoja ama kundi la watu wachache pekee.
Natoa urejeleo huo kufuatia ripoti za kukanganya kuhusu kiwango cha deni ambacho Kenya inadaiwa na nchi za nje, hali halisi ya kiuchumi nchini na uwezo wetu kulipa madeni tunayodaiwa.
Kwa mujibu wa taarifa za Wizara ya Fedha, deni la taifa lilikuwa Sh7.1 trilioni kufikia Agosti.
Licha ya kiwango hicho kuendelea kuongezeka kadri siku zinavyosonga, Rais Uhuru Kenyatta amenukuliwa mara kadhaa akisema Wakenya hawapaswi kuwa na hofu kuhusu mwelekeo huo, kwani hata mataifa yaliyostawi kiuchumi kama Amerika, Uingereza na Japan pia yana madeni makubwa.
Kwa wakati mmoja, Rais alitetea mtindo wa serikali yake kuendelela kukopa, kwani fedha hizo zinaelekezwa katika ufadhili wa miradi ya maendeleo, ambayo baadaye itaisaidia Kenya kulipa madeni inayodaiwa.
Bila shaka, kauli hiyo ni ya kuridhisha, lakini uhalisia uliopo unaachilia taswira tofauti sana.
Kwa mfano, ni kinaya kwa Serikali kuendelea kuzindua miradi ya mabilioni ya fedha, wakati wafanyakazi katika sekta muhimu nchini wanaendelea kugoma wakilalamikia kutolipwa mishahara na marupurupu yao.
Mnamo Jumatano wiki iliyopita, Waziri wa Fedha, Bw Ukur Yatani alifichua kuwa mwelekeo wa nchi kifedha si mzuri hata kidogo.
Katika kauli iliyo nadra sana kutolewa na waziri, Bw Yatani alisema “atakuwa akiidanganya nchi ikiwa atasema hali ya uchumi ni ya kuridhisha.”
Ilivyo sasa, imebainika kuwa Kenya inapanga kurejea tena kwa Benki ya Dunia na Shirika la Fedha Duniani (IMF) kuomba mkopo wa pili mwaka huu, baada ya kupata mkopo wa Sh107 bilioni Mei, kuisaidia kukabiliana na athari za janga la virusi vya corona.
Alipoondoka uongozini hapo 2013, miongoni mwa hatua muhimu alizopiga Rais Mstaafu Mwai Kibaki katika utawala wake ni kuiwezesha Kenya kutochukua mikopo kutoka kwa taasisi hizo, kwani huwa zina masharti magumu.
Yasikitisha tumerejea hapo baada ya miaka saba pekee.
La muhimu sasa ni Rais Kenyatta awaeleze Wakenya ukweli kuhusu hali ya uchumi nchini, ili taifa lisizame bila wananchi kufahamu.